In Summary

Kiapo hicho kwa viongozi hao wapya wa TFF kilisimamiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.


Dodoma. Rais mpya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia baada ya kuibuka na ushindi wa kishindo wa kura 95 na kuwabwaga wapinzani wake wanne alikuwa wa kwanza kula kiapo cha utiifu akifuatiwa na Makamu wake Michael Wambura aliyepata kura 85 akiwapiga bao wapinzani wake watatu.

Kiapo hicho kwa viongozi hao wapya wa TFF kilisimamiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.

Zoezi hilo limefanyika mara baada ya Kamati ya Uchaguzi chini ya Mwenyekiti Wakili Revocatus Kuuli kutangaza majina ya wagombea waliochaguliwa kuongoza Shirikisho hilo kwa miaka minne

Baada ya viongozi hao wa juu kuapishwa wajumbe 13 wa Kamati ya Utendaji walifuatia kula kiapo.

Karia alikuwa kwenye kinyang'anyiro hicho pamoja na Shija Richard, Ally Mayay aliopata kura tisa (9) kila mmoja, Fredrick Mwakalebela aliyepata kura tatu (3), Imani Madega kura nane (8) na Emmanuel Kimbe kura moja (1).

Nafasi ya Makamu wa Rais, Wambura alipata kura 85, alishindana na Mulamu Ngh'ambi aliyepata kura 25, Mtemi Ramadhan kura 14, Richard Selasela kura mbili.

Wajumbe wa kamati ya utendaji walioshinda kutoka katika Kanda 13 ni pamoja na  Kanda 13(Dar es Salaam) mshindi ni Lameck Nyambaya aliyepata kura 41. Kanda 12 (Kilimanjaro&Tanga) mshindi ni Khalid Abdallah aliyepata kura 70.

Kanda ya 11(Pwani&Morogoro) mshindi ni Francis Ndulane aliyepata kura 70, Kanda ya 10 (Dodoma&singida) mshindi ni Mohammed Aden aliyepata kura 35, Kanda ya 9 (Lindi&Mtwara) mshindi ni Dastan Mkundi amepata kura 74.

Kanda ya 8 (Njombe&ruvuma) mshindi ni James Mhagama aliyepata kura 60, Kanda ya 7 (Mbeya & Iringa) mshindi ni Elias Mwanjala aliyepata kura 61, Kanda ya 6 (Katavi&Rukwa) mshindi ni Kenneth Pesambili aliyepata kura 72

Kanda ya 5 (Kigoma&Tabora) mshindi ni Issah Bukuku aliyepata kura 80, Kanda ya 4  (Arusha&Manyara) Sarah Chao aliyepata kura 57, Kanda ya 3 (simiyu&shinyanga) mshindi Mbasha Matutu aliyepata 67, Kanda ya 2 (Mwanza&Mara) Vedastus Lufano alipata kura 67, Kanda ya 1 (Kagera&Geita) mshindi alikuwa Salum Chama alipata kura 90.                       

Ahadi 11 za Karia

Karia alizindua kampeni  na kutaja vipaumbele vyake 11 atakavyohakikisha anavisimamia kikamilifu.

Vipaumbele hivyo vilivyotajwa ni nidhamu ya muundo na mfumo, maendeleo ya vijana, wanawake na soka la ufukweni, mafunzo na ujenzi wa uwezo, mapato, uwezeshaji na nidhamu ya fedha, miundombinu na vifaa na maboresho ya bodi ya ligi.

Vingine ni ushirikiano wa wadau, udhamini na masoko, maboresho ya mashindano, uimarishaji mifumo ya kumbukumbu na ufanisi wa waamuzi.

Karia alisema kuwa atahakikisha vipaumbele hivyo vinafanyiwa kazi muda mfupi baada ya yeye kuingia madarakani.