In Summary

Miamba hiyo ya soka Ulaya imeshindwa kufuzu kwa Kombe la Dunia

Rome, Italia.  Timu ya taifa ya Italia ‘Azzurri’ haitashiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 60 katika historia ya nchi hiyo.

Nahodha na kipa nguli wa Italia, Gianluigi Buffon alishindwa kujizua kumwaga chozi hadharani baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa katika mchezo waliotoka suluhu na Sweden.

Mbali na kipa huyo wa klabu ya Juventus, wachezaji wa timu hiyo walilia uwanjani baada ya kuduwazwa na Sweden. Italia imeng’oka baada ya wapinzani wao kusonga mbele kwa faida  ya bao 1-0 ililopata katika mchezo wa kwanza.

Licha ya kutawala mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa San Siro, Italia ilishindwa kufua dafu mbele ya Sweden.

Muuaji wa Sweden dhidi ya Italia, alikuwa Jakob Johansson aliyefunga bao hilo katika mchezo wa kwanza.

Buffon mwenye miaka 39, aliyekuwa akilia muda wote wakati akihojiwa na vyombo vya habari, ametangaza kustaafu soka ya kimataifa baada ya kuitumikia Italia katika mechi 175 akiipa ubingwa wa dunia mwaka 2006.

Nyota wengine waliotangaza kutundika daluga ni Andrea Barzagli, Daniele De Rossi na Giorgio Chiellini. Italia imetwaa Kombe la Dunia mara nne.

“Siyo bahati mbaya kwangu, lakini kwa familia yote ya mpira. Tumeshindwa kupata kitu Fulani chenye umuhimu mkubwa,” alisema Buffon akibubujikwa machozi.

Mashabiki wa soka katika mitaa tofauti ya nchini humo waligubikwa na simanzi, baada mpira kumalizika.

Italia ni moja ya nchi vigogo duniani yenye historia katika mchezo wa soka, kukosekana kwake kunaweza kupunguza msisimko wa fainali hizo zilizopangwa kuchezwa mwakani nchini Russia.

Mara ya mwisho Italia ilishindwa kukata tiketi kucheza fainali hizo ilikuwa mwaka 1958 kabla ya juzi usiku kukaliwa kooni na Sweden iliyofuzu fainali hizo.

Kocha wa Italia, Gian Ventura, amejiwekea rekodi mbaya katika historia yake ya soka kwa kushindwa kuipeleka katika fainali hizo baada ya miaka 60.