Moscow, Russia. Misri imewasili Russia kwa fainali za Kombe la Dunia, lakini nyota Mohamed Salah ameiweka njia panda.

Licha ya kuanza mazoezi mepesi, uamuzi wa Salah kucheza au kutocheza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Uruguay Ijumaa utajulikana baada ya saa 24 zijazo.

Daktari wa timu hiyo, Mohamed Abou al-Ela, alisema mchezaji huyo wa Liverpool hawezi kucheza hadi awe fiti kwa asilimia 100.

“Hatuwezi kusema kwa sasa kama atacheza hadi baada ya siku mbili (moja), tutatoa taarifa rasmi. Hatuwezi kumtumia hadi apone kabisa,” alisema daktari huyo.

Misri inashiriki fainali hizo, baada ya kupita miaka 28 ambapo mara ya mwisho ilicheza mwaka 1990.

Mabingwa hao mara saba wa Kombe la Afrika, wamepangwa Kundi A na Juni 15 watafungua pazia kwa kuumana na Uruguay.

Kocha wa Misri Ihab Lehata alisema wachezaji wana ari nzuri ya kucheza kwa kiwango bora fainali hizo baada ya kufanya maandalizi.

Salah aliumia bega katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuchezewa madhambi na nahodha wa Real Madrid Sergio Ramos katika mchezo waliofungwa mabao 3-1. Nyota huyo alitakiwa kuwa nje ya uwanja wiki mbili au tatu.