In Summary

Kati ya sehemu ambayo mambo haya yamejadiliwa kwa kina katika siku za karibuni ni kwenye kitabu kilichoandikwa katika mradi wa utafiti wa mambo ya kodi uitwao Taxation, Institutions and Participation (TIP), mradi wa utafiti wa miaka minne (2014 mpaka 2018) chini ya ufadhili wa Tume ya Utafiti ya Norway.

        Masuala ya kodi na maficho yake kimahususi ni kati ya mambo makuu ya kimjadala kwa sasa unaojumuisha mtiririko wa mtaji duniani. Afrika inashuhudia mitiririko haramu wa mtaji.

Kati ya sehemu ambayo mambo haya yamejadiliwa kwa kina katika siku za karibuni ni kwenye kitabu kilichoandikwa katika mradi wa utafiti wa mambo ya kodi uitwao Taxation, Institutions and Participation (TIP), mradi wa utafiti wa miaka minne (2014 mpaka 2018) chini ya ufadhili wa Tume ya Utafiti ya Norway.

Mradi huo unatekelezwa Tanzania, Angola na Zambia. Nchini, mradi unasimamiwa na Chuo Kikuu Mzumbe ukiratibiwa na taasisi ya utafiti ya Chr. Michelsen Institute (CMI) ya Norway. Maficho ya kodi na mtiririko wa mtaji Afrika, ni hoja zilizojadiliwa kwa kina katika kitabu hicho.

Kodi na maficho

Kodi ni moja ya njia kuu za kupata fedha za kugharamia huduma na bidhaa za umma zinazotolewa na Serikali. Huduma hizi ni pamoja na elimu, afya, maji, ulinzi, usalama, miundombuni kama barabara, viwanja vya ndege, bandari, reli na mawasiliano.

Licha ya kodi, nchi inaweza kugharamia huduma hizi kutokana na mikopo, misaada na mapato mengine yasiyo ya kodi. Hata hivyo kodi ndiyo chanzo endelevu na cha uhakika kwa nchi. Mikopo inaongeza deni la taifa na changamoto za kulilipa wakati misaada inaweza kuwa na masharti magumu.

Kodi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi. Kati ya mambo yanayopunguza mapato ya kodi ni maficho ya kodi.

Kwa lugha rahisi maficho ya kodi ni nchi zinazotoa fursa na mianya kwa watu na kampuni kutoka nje ikiwamo kutolipa kodi kabisa. Mifumo ya nchi hizi huruhusu kampuni na watu binafsi kupata huduma kwa siri kuhusu fedha zao. Wanaoficha hawaulizwi na nchi wenyeji kuhusu walivyozipata fedha hizo.

Nchi hizo pia hazitoi taarifa za wahusika kwa mamlaka yoyote ya nje. Kati ya nchi zinazotajwa kuwa maficho ya kodi duniani ni Andorra, Bahamas, Belize, Bermuda, British Virgin Islands, Cayman Islands, Channel Islands, Cook Islands, Hong Kong, Isle of Man, Mauritius, Lichtenstein, Monaco, Uswisi na Panama.

Manufaa

Usiri unaofanywa huzinufaisha nchi zinazopokea fedha hizi kwa njia mbalimbali. Mojawapo ni kuwapo kwa fedha nyingi kwani hazikai tu katika benki bali zinazunguka kama mtaji na ni muhimu katika shughuli za biashara na uchumi.

Faida hizi kwa nchi wenyeji ni kati ya mambo yanayofanya vita dhidi ya maficho haya kuwa ngumu.

Nyuma ya maficho haya kuna faida za kibiashara na mapato makubwa kwa wadau mbalimbali. Fedha zinazofichwa ni moja ya vyanzo vikubwa vya mtaji na masoko ya fedha yaliyo imara.

Watu binafsi na kampuni hunufaika kwa kodi ndogo au kutokuwepo kabisa kwa kodi ukilinganisha na nchi nyingine. Nchi zisizo za maficho huweza kuwa na kodi za hadi tarakimu mbili, maficho huwa na kodi sifuri au tarakimu moja.

Katika mijadala ya maficho ya kodi, kati ya maswali yanayoweza kuulizwa na yanayohitaji kufafanuliwa ni changamoto na matatizo yatokanayo na maficho ya kodi. Kimsingi na kwa ujumla wake, maficho ya kodi ni tatizo kwa nchi zinazoendelea na masikini kama Tanzania.

Fedha zinapotoka katika nchi hizi na kwenda mafichoni maana yake ni kuwa hazitaweza kuchangia katika kugharamia bidhaa na huduma za umma. Matokeo yake ni wananchi kukosa huduma na bidhaa za umma kwa wingi na ubora unaotakiwa.

Kinachojalisha zaidi ni matokeo ya ukosekanaji huu yakiwemo vifo kwa kukosa huduma za afya, maji, ubovu wa miundombinu au kutokuwapo kwa watoa huduma. Matokeo mengine ni udumavu kutokana na lishe duni na ujinga kutokana na ukosefu wa elimu stahiki. Kinachosikitisha zaidi ni kuwa wahanga wakuu ni masikini na watu walio pembezoni.

Mtiririko wa mitaji

Kama ilivyo kwa maficho ya kodi, suala la mtiririko wa mtaji ni jambo kuu la kimjadala vilevile. Dhana ya mtiririko wa mtaji inamaasha hali ya fedha kutoka sehemu moja ya dunia kwenda nyingine.

Inaweza kuwa hali ya fedha kutoka nchi moja hadi nyingine au bara moja hadi jingine. Mtiririko huu unaweza kuwa kwa sababu mbalimbali. Sababu hizi zinaweza kuwa za kiuwekezaji, kiuzalishaji au kibiashara. Mtiririko unaweza kuwa ndani ya kampuni au kutoka kampuni moja hadi nyingine kwa malengo mbalimbali.

Kati ya jambo muhimu la kuelewa ni kuwa si kila mtiririko wa mitaji ni mbaya, haramu na wa uvunjifu wa sheria. Katika muktadha wa mradi wa utafiti wa TIP, mtiririko wa mitaji unaojadiliwa ni ule haramu.

Mtiririko halali na unaofuata sheria haupaswi kuwa na matatizo. Mtiririko wenye matatizo katika muktadha wa mradi wa TIP na kitabu tajwa ni ule haramu. Huu ni mtiririko wa mtaji kupitia fedha zinazopatikana isivyo halali, kuhamishwa isivyo halali hata kutumika isivyo halali.

Huweza kuwa fedha zinazotokana na ukwepaji kodi, rushwa, biashara haramu kama ya binadamu, dawa za kulevya, ujangili au utekaji nyara. Mtiririko huu unachangia umasikini wa Afrika na watu wake.

Mtiririko haramu ukichanganyika na maficho ya kodi, hufanya nchi waathirika kuwa katika hali ngumu sana kiuchumi.

Hivyo ni muhimu kupambana na hali hizi. Kuelewa dhana hizi kama ilivyoelezwa katika makala haya ni mwanzo wa mchango katika mapambano haya.