In Summary
  • Bahati mbaya sana kuanzisha biashara kumeonekana kana kwamba hakuhitaji kujifunza wala kusomea. Madhara ya kutojifunza biashara ni makubwa. Kujifunza si lazima iwe kwa kwenda chuo, inaweza kuwa kwa kusoma vitabu na majarida ya biashara au kutembelea tovuti za biashara.

Wajasiriamali na wafanyabiashara wanatakiwa kujifunza ili kufanya shughuli zao kwa weledi unaohitajika katika kila hatua.

Bahati mbaya sana kuanzisha biashara kumeonekana kana kwamba hakuhitaji kujifunza wala kusomea. Madhara ya kutojifunza biashara ni makubwa. Kujifunza si lazima iwe kwa kwenda chuo, inaweza kuwa kwa kusoma vitabu na majarida ya biashara au kutembelea tovuti za biashara.

Hilo pia linaweza kufanywa kwa kujiunga makundi ya wafanyabiashara yenye tija na kutembelea kurasa za biashara mtandaoni, kuangalia na kusikiliza vipindi vya biashara kwenye televisheni na redio. Kuhudhuria semina, makongamano ya biashara na mafunzo ya muda mfupi ni nji anyingine. Unaweza kwenda chuoni kujifunza ikibidi.

Chochote utakachofanya kati ya hivyo itakuwa umejifunza na utapata ufahamu utakaokuwezesha kufanya vyema katika biashara zako. Unaweza kuomba ushauri kutoka kwa wataalam au ukaajiri wasomi kuendesha kampuni yako.

Elimu ya ujasiriamali ni muhimu ili kujua misingi ya kuendesha biashara na kupata mafanikio yanayostahili. Misingi hiyo ni pampja na uendeshaji na usimamizi wa biashara, wafanyakazi, fedha na masoko.

Mitandao ya kijamii inawezesha watumiaji wake kuwasiliana na kutumiana taarifa kwa njia ya meseji, sauti na picha au video. Ukiitumia kujifunza biashara ni mizuri na itakupa faida kwenye biashara yako.

Yapo mengi unayoweza kuyafanya kwenye mitandao hii. Unaweza kufungua ukurasa wa biashara yako ambao utatembelewa na wateja wa huduma au bidhaa ulizonazo hivyo kuongeza mauzo.

Mitandao ya kijamii inawezesha kuwasiliana na wateja, kuwapa wateja fursa ya kuuliza na kujibiwa kwa urahisi, bila gharama.

Mitandao hii hufanikisha kujitangaza. Unapoweka picha ama video ya bidhaa zako inasaidia kupata mawazo mbalimbali ya watu wanatembelea ukurasa wako na huenda wakashawishika kufanya kununua.

Kubadilishana mawazo na wateja wako katika ukurasa wa mtandao wa kijamii kunaleta imani kwa wateja na kuona wanathaminiwa. Hali hii hubaki vichwani mwa wateja na hukumbuka haraka bidhaa au kampuni yako.

Ni rahisi kutoa maelezo kwa wateja wengi katika mitandao ya jamii endapo kuna uzushi ama hitilafu kuhusiana na bidhaa ama huduma zako.

Kama umebanwa na majukumu mengine, kuendesha kurasa zako za biashara katika mitandao lakini unaweza kuingia mikataba na wataalamu ambao wanaweza wakasimamia kurasa zako kila siku kwa makubaliano maalum.

Wataalamu hawa, watakuwa wanajibu maswali na meseji mbalimbali za wateja wako. Wanaweza kutuma picha na video za bidhaa ama huduma zako kwa niaba yako pia.

Ikumbukwe, wengi wetu wenye kufanya biashara na ujasiriamali tumejiunga huko na tuna marafiki wengi lakini hatutumii majukwaa hayo kunufaika kibiashara. Marafiki 100 au 2,000 ulionao unaweza ukawafanya wateja wa biashara zako.

Kila siku wajulishe biashara na bidhaa zako, wakaribishe wanunue, wape ofa maalum, waalike wakuunge mkono pamoja na mengi mengineyo. Kwa kufanya hivyo utakuwa unatumia muda wako na majukwaa hayo kwa manufaa na faida.

Wakizoea na kurasa zako zikawa zinatembelewa na watu wengi, unaweza ukaongeza kipato kutokana na matangazo ya mtandaoni pia. Yaani wakati unatangaza bidhaa zako ukawavutia na wengine kuja kujitangaza na wakakulipa.

Yapo malipo yanayotolewa na kampuni kubwa kama Youtube kwa watumiaji wakubwa wa mtandao huo. Hizi zote ni furs amuhimu ambazo unaweza kunufaika nazo kwenye mitandao hii ya kijamii ambayo mara nyingi inaonekana inakiuka maadili ya jamii yetu.