In Summary

Serikali imedhamiria kuongeza mchango wa sekta ya viwanda kwenye Pato la Taifa (GDP) mpaka ufike asilimia 40 kutoka wastani wa asilimia 20 uliopo sasa hivi. Sambamba na hilo, kipato cha kila mwananchi kiwe cha kati, wastani wa Dola 3,000 za Marekani (zaidi ya Sh6.6 milioni) kwa mwaka.

Maji ni kila kitu. Bila uhakika wa upatikanaji wa rasilimali hiyo, ndoto ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda haiwezi kutimia.

Serikali imedhamiria kuongeza mchango wa sekta ya viwanda kwenye Pato la Taifa (GDP) mpaka ufike asilimia 40 kutoka wastani wa asilimia 20 uliopo sasa hivi. Sambamba na hilo, kipato cha kila mwananchi kiwe cha kati, wastani wa Dola 3,000 za Marekani (zaidi ya Sh6.6 milioni) kwa mwaka.

Katika kutekeleza mkakati huo, imeutaka kila mkoa kujenga walau viwanda 100 ndani ya mwaka mmoja ujao.

Wakati mpango huu ukitekelezwa, wadau wanatahadharisha kuhusu upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali huku viwanda vikipewa kipaumbele. Matokeo ya utafiti wa Benki ya Dunia hata uliofanywa hivi karibuni na Taasisi ya Twaweza, yanapendekeza kuchukuliwa kwa hatua za ziada kukabili changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo.

Kwenye ripoti yake ya tathmini ya mwaka huu ya mwenendo wa uchumi wa Tanzania iliyojikita kwenye matumizi sahihi ya maji ijulikanayo kama Tanzania Economic Update; Managing Water Wisely, Benki ya Dunia imesema hazina ya maji imepungua japo si kwa kiasi kikubwa.

Mkurugenzi mkazi wa benki hiyo nchini, Bella Bird anasema kwa miaka 25 iliyopita, mahitaji ya rasilimali hiyo yamekuwa yakiongezeka wakati upatikanaji wake ukiendelea kupungua.

Ndani ya kipindi hicho, ripoti inasema uwiano umepungua kutoka zaidi ya mita 3,000 za ujazo mpaka takriban mita 1,600 kwa kila mwananchi hivyo kuweka Tanzania kwenye orodha ya nchi zenye uhaba duniani.

       “Maji ni muhimu kwa mabadiliko ya kiuchumi Tanzania. Yanahitaji kuangaliwa kwa umakini ili kuchangia maendeleo yanayotarajiwa,” anasema Bella.

Mchango wa maji kwenye maendeleo ya kiuchumi ni makubwa hivyo, benki hiyo inasema sera na taasisi imara za usimamizi zinahitajika kuongeza tija ya matumizi kwenye shughuli za kiuchumi, kijamii na kimazingira.

Benki hiyo inasema kutokana na mikakati dhaifu ya kudhibiti rasilimali hiyo, GDP ya baadhi ya nchi itashuka kwa asilimia sita ifikapo mwaka 2050 ikiwa ni athari zitakazojitokeza kwenye kilimo, uzalishaji umeme, kipato cha wananchi na taifa kwa ujumla pamoja kuongezeka kwa umasikini.

“Umuhimu wa maji kuchangia maendeleo unajidhihirisha kwenye kilimo, uzalishaji umeme na uchimbaji madini. Mafuriko au ukame ni miongoni mwa majanga yanayoweza kutokea. Mikakati isipowekwa, mlipuko wa magonjwa huweza kuathiri uchumi wa taifa,” anasema Bella.

Kuwa na mipango ya uhakika ni lazima taarifa sahihi ziwepo. Benki hiyo inashauri takwimu ziwepo ili kusaidia kukabili upotevu na mgawanyo sawa kwa jamii mbalimbali pamoja na majanga ya mafuriko na ukame. Serikali iwekeze kutambua hazina ya maji hasa yaliyopo ardhini, ubora na matumizi.

Utafiti wa sauti za wananchi uliofanywa na taasisi ya Twaweza mwaka huu unaonyesha kuna changamoto tatu ambazo zinahitaji kutafutiwa suluhu ya kudumu. Zinajumuisha gharama kubwa ya upatikanaji wa maji, usambazaji usio wa uhakika na uhaba wa vyanzo.

Matokeo ya utafiti huo yanaeleza kwamba ni asilimia 54 ya Watanzania wanapata maji kutoka kwenye vyanzo vilivyoboreshwa; asilimia 46 vijijini na asilimia 74 mjini.

Alipokuwa akizindua jukwaa la usimamizi na utunzaji wa maji la Bonde la Pangani, katibu mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema Tanzania ina vyanzo vingi vya lakini inakabiliwa na uhaba wa maji.

Upungufu uliopo, alisema unaongeza ulazima wa kutunza vyanzo vilivyopo kwa kutoa elimu kwa wananchi ili wasiendelee kuvivamia na kuwaondoa wanaofanya shughuli zao kwenye vyanzo hivyo.

“Maji yanachangia ukuaji wa kila sekta, bila maji kwa mfano, hakuna viwanda, kilimo, ufugaji wala huduma nyingine za kijamii. Maji ni injini ya uchumi, lakini kwa bahati mbaya maji yamepungua wakati matumizi yake yakiongezeka kila siku,” alisema.

Kukauka kwa vyanzo vya maji, kwa mfano Bonde la Mto Pangani kunachangia kuongezeka kwa uhaba katika mikoa inayolitegemea kupata maji hivyo juhudi za makusudi kuhitajika kuvitunza.

Arusha

Arusha ni miongoni mwa majiji makubwa nchini yenye watu wengi lakini lenye changamoto ya upatikanaji wa uhakika wa maji safi na salama.

Mkazi wa Mianzini, Safina Jailos anasema kuna wakati anatumia hadi Sh5,000 kwa siku kununua maji ya kutosha matumizi ya familia yake kuepuka kupoteza muda mwingi kuyatafuta.

“Kuna muda unalazimika kutumia maji yoyote unayopata bila kujali usalama wake, na hapo magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu huibuka. Tatizo ni kubwa na linahitajika ufumbuzi wa haraka,” anasema Safina.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Arusha, (AUWSA), Ruth Koya anasema changamoto hiyo inatokana na ongezeko la watu ilhali miundombinu ikiendelea kubaki ile ile. Lakini, baada ya mapendekezo ya muda mrefu, Serikali inatekeleza mradi mkubwa utakaoongeza uzalishaji kutoka lita milioni 40 hadi lita milioni 200 kwa siku.

Mradi huo utagharimu Sh476 bilioni zilizotolewa kwa ushirikiano wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na Serikali. Mradi utahusisha utafutaji wa vyanzo, uchimbaji wa visima virefu, ujenzi wa matenki na ulazaji wa mabomba ya maji safi na maji taka. Vilevile kutakuwa na ujenzi wa mitambo ya kutibu na mabwawa ya kusafisha maji taka.

Utekelezaji wa mradi huo, Koya anasema utasaidia kupunguza maji yanayopotea njiani kutoka wastani wa asilimia 40 hadi asilimia 25 kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ubovu wa miundombinu.

“Endapo maji yote yangefika kwa wananchi, ingesaidia kukabiliana na uhaba uliopo. Kupitia mradi huu tunakwenda kuweka miundombinu mizuri itakayozuia upotevu wa maji. Tutafanya ukarabati wa miundombinu na kuzuia uvujaji na kuziba kwa mabomba,” anasema Koya.

Anasema mradi huo ukikamilika utaongeza idadi ya watu wanaopata maji katika mji huo kutoka 325,000 hadi 600,000. Vilevile, utaongeza mtandao wa kukusanya majitaka kutoka asilimia 7.6 hadi asilimia 30 katika jiji hilo.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe alikuwa miongoni mwa wageni walioshuhudia utiaji saini wa mkataba wa mradi huo utakaotekelezwa kwa ushirikiano wa kampuni za Shanxi Construction Engineering Corporation, Mineral Company na Jiangxi Geo-engineering Group Company.

Kamwelwe aliwataka wakazi wa Arusha kuweka kando itikadi za kisiasa na kuhakikisha mradi huo na mingine iliyopangwa inatekelezwa kwa ufanisi kwa kuzingatia kwamba maendeleo hayana vyama.

Kwa uendelevu wa huduma hiyo, Kamwelwe anasema ni muhimu kwa kila mkazi wa jiji hilo kuwa mlinzi wa miundombinu itakayowekwa na kutoa taarifa inapobainika viashiria vyovyote vya uhujumu.

“Mradi huu umegharimu fedha nyingi, ni jukumu letu kuhakikisha miundombinu haiharibiwi au kuhujumiwa kwa namna yoyote ile. Isiwe umepishana kauli na mwenzako ukaona hasira zako uzimalizie kwa kuharibu miundombinu. Maji ni rasilimali muhimu sana tunayotakiwa kuitunza,” anasema Kamwelwe.

Ujumbe huo ulitua vyema masikioni mwa meya wa jiji hilo, Kalist Lazaro ambaye ameahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali na kusimamia kwa ukamilifu kuhakikisha mradi huo unatekelezwa.

“Maji yakipatikana itatuondolea adha ya wananchi kuzunguka, maji safi na salama yatasaidia kupunguza mlipuko wa magonjwa ikiwemo kipindupindu. Nitasimamia kwa ukamilifu kuhakikisha mradi unafanikiwa na kukamilika kwa wakati na miundombinu inatunzwa,” anasema.