In Summary
  • Baada ya muda mfupi unasikia watu wamevamiwa katika vibaraza wanapokutana miaka nenda miaka rudi na kupigwa mikwaju au mapanga au kuvunjiwa milango ya nyumba zao, wakapigwa vibaya sana kuporwa fedha na vitu vya thamani.

        Sitaki kuamini ninayosikia na sitaki kuamini ninayoona mara kwa mara Zanzbar hivi sasa. Kwa mara nyengine imekuwa kawaida kuona magari yaliojaa watu, baadhi yao wakiwa wamejifunika uso (Ninja) waliovalia sare kama za vikosi vya ulinzi na kiraia, wengine wakiwa na mikwaju au silaha za moto wakizurura mitaani.

Baada ya muda mfupi unasikia watu wamevamiwa katika vibaraza wanapokutana miaka nenda miaka rudi na kupigwa mikwaju au mapanga au kuvunjiwa milango ya nyumba zao, wakapigwa vibaya sana kuporwa fedha na vitu vya thamani.

Watu wanaofanya mambo kama haya visiwani miaka ya nyuma waliitwa Janjaweed, baadaye wakapewa jina la Mazombi na sasa nasikia wanatambuliwa kwa maelezo ya watu wasiojulikana.

Mtokeo haya yameongezeka kwa kasi siku za karibuni na hali imekuwa ya kusikitisha na kutisha.

Katika mitaa mingi kama Mlandege, Mchangani, Mkamasini Mtendeni, Vikokotoni, Mwembetanga na Barastekipande, mjini Unguja, watu hujifungia majumbani kuanzia saa tatu usiku na bado hawana uhakika wa usalama wao.

Hofu kubwa imetanda na wau wengi niliozungumza nao wanaonekana kuhofia usalama wao na wa familia zao.

Wiki iliyopita nilikuwa eneo la Mchangani kama saa mbili na nusu usiku nikijiburudisha na kikombe cha kahawa na watu niliojuwa nao tokea nikisoma shule ya msingi.

Mara niliona wanaume na wanawake wanakimbizana mbio na nilipouliza ni kimetokea niliambiwa Mazombe wapo mtaani na wanapiga watu ovyo na kuwapora fedha, saa na simu.

Haraka haraka niliondoka barazani, nikapita kwa mwendo wa kasi kwa marafiki zangu vijana wa Tanga wanaoshona nguo, nikawasalimu na kwenda zangu.

Siku ya pili nilipofika eneo hilo ili kwenda katika baraza yangu ya kahawa nilikuta kiduka chao kimefungwa na kuambiwa mara baada ya kusalimiana nao jana yake walivamiwa na kupigwa vibaya na kuporwa fedha, simu na nguo za wateja.

Ujahili kama huu unasikika kutokea sehemu nyengine za mjini Unguja kama Mtoni, Daraja Bovu, Kinuni na kwengineko. Hii imepelekea baadhi ya vijana ikifika saa mbili usiku na wapo mjini kutoudi makwao kwa kuhofia kukutana na watu wasiojulikana na kuhatarisha usalama wao. Wengi wao hulala misikitini.

Vile vile zipo taarifa za watoto wadogo kutekwa nyara na wengine kutupwa maeneo ya mashamba, eneo moja likiwa Msitu wa Jozani, Kusini Unguja, baada ya kudhalilishwa.

Taarifa za mitaani na katika mitandao zinadai gari inayotumika kuwateka nyara watoto ni a Noah ya rangi nyeupe. Hili linafaa kufuatiliwa na Jeshi la Polisi.

Kwa bahati mbaya haya husikii kuelezwa katika vyombo vya habari vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Badala yake habari zinazopewa umuhimu ni za kiongozi huyu kasema hili, mwengine katoa pongezi, wanachama wa Saccos wamekutana kuweka mkakati au polisi wamekamata watu wanaodaiwa kutumia au kuuza dawa za kulevya.

Habari za Mazombi waliozusha taharuki mjini Unguja huzisikii kama vile hapana matokeo hayo ni mambo ya kawaida.

Lakini, habari za watu kupigwa na kuuawa zinatoka katika vyombo va habari vya Bara, katika misikiti, nchi jirani na mitandao ya nyumbani na nje.

Ninakumbuka Rais Ali Mohamed Shein baada ya uchaguzi uliodaiwa na wapinzani kuwa ulikuwa kiini macho, aliahidi kutandika mazingira ya utawala bora wa haki na sheria na ambao hautazusha hisia za maonevu.

Niliamini kauli ya huyu sahiba wangu niliyejuana naye tokea tukiwa wadogo na kuelewana naye vyema hadi leo, lakini kwa bahati mbaya sidhani ninayoyaona na kuyasikia ndio vigezo vya utawala bora.

Siku moja nilimuelezea hali hii katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Ikulu na alisema hakuwa na taarifa hizo na kuahidi kufuatilia. Sijui kilichoendelea.

Sasa ninayoyaona na kuyasikia ni yale yale na yananipa hofu kama Zanzibar ya sasa ina mazingira ya utulivu na utawala bora. Sijui wanaopanga na kutekeleza haya watasemaje kwa Mola wao.

Kila mtu mwenye kuvitakia amani visiwa vya Unguja na Pemba anayo haki ya kuuliza Zanzibar inaelekea wapi na kwa nini wanaovunja sheria na kuonea watu hawakamatwi na kuwajibishwa kisheria?

Sitaki kuamini wanaofanya haya ni popobawa kwani uzoefu umeonyesha popobawa hawatumii magari na hawabebi silaha.

Hali hii inanikumbusha watu waliovunja sheria, kama za kupandikiza mbegu za chuki, uhasama na ubaguzi wanavyofumbiwa macho Visiwani.

Kwa mfano utatoa maelezo gani yaeleweke kwa kutowashughulikia waliobeba bango lililiochochea uhasama wa kikabila wakati wa kuadhimisha miaka 52 Mapinduzi katika uwanja wa Amani.

Hatujasikia hata kuambiwa: “Mfanyavyo ni vibaya” wakati watu wa ainahii walipasa kushitakiwa kwa kufanya uchochezi.

Nimesema mara nyingi na ninarudia kuwa huu mwenendo wa kuruhusukikundi cha watu kufanya watakavyo, ikiwa pamoja na kupiga watuvibaya, kuwavunjia nyumba zao na kuhatarisha maisha yao ni wa hatari.

Mwenendo hautoi sura nzuri ya utawala bali unawapa nafasi watuwachache kuipaka matope serikali na kuwashajiisha wengine kusisitizahoja ya kwamba utawala bora Visiwani ni wa nyimbo na siovitendo.

Hali kama hiiona wakati wa utawala wa Rais mstaafu, komandoo SalminAmour. Wengi tulitarajia siasa chafu kama zile zimepita na kuwasehemu ya historia. Lakini kumbe tunaanza alifu kwa ujiti kuruhusumaonevu na udhalilishaji.

Nawaambia kwa mara nyengine wanofikiri kugeuza migongo ya watu ngomani jambo zuri waelewe wanapandikiza mbegu za chukina uhasama na watu kuviona visiwa hivi si vya amani na utulivu.

Labda nikumbushe kwamba mikong’oto iliotumika mitaani na majumbani nawatu kuuliwa kwa kupandisha bendera ya CUF wakati wa ufunguzi wa tawilao Pemba na mamia ya watu kufunguliwa mashitaka siku za nyumakumepandikiza mbegu za chuki zinazohitaji utaalamu kurudisha imani yawananchi walodhulumiwa.

Ubabe sio mwenendo mzuri. Kinachotakiwa ni amani ya kweli na walewanaovunja sheria kuwajibishwa.

Vitisho vinavyoonekan Zanzibar hivi sasa vitaimarisha uhasama wakisiasa Visiwani.

Kama ni muhimu kupata madunzo basi tumepata mengi na tujifunze nakuelimika. Vyenginevyo tutajuta kwa kutaa kujifunza.

Wenzetu katika nchi nyingi waliokataa kujifunza ubaya wa kupanga nakushabikia maovu wanajuta, wamejirekebisha na wasonga mbele.

Suala ni lini watu wa Zanzibar watajifunza na kuachana na vitisho nakutoruhusu hao wanaoitwa watu wasiojulikana kufanya watakavyo?.

Kwa hali ninayoiona sasa ya watu kupigwa ovyo mitaani na majumbani nakuporwa fedha na mali zao bado hapana dalili sio tu za kujifunzabali hata kuwepo nia thabiti inayotoka moyoni ya kutaka kujifunza.

Tupeane pole watu wa Zanzibar huku tukimoba Mungu atupe imani,aturudishie utu wetu na kupendana na atuepushie shari na kutufungulianjia itayotupa amani,k heri, raha na furaha.