In Summary
  • Kumekuwa na hisia tofauti kuhusu mada hii wengine wakiunga mkono maoni ya makala na wengine wakipinga hoja hii. wengine walienda zaidi na kudai kuwa mwandishi wa makala yale alikuwa anatumiwa na wageni.

Jumatano iliyopita tulitazamna baadhi ya athari ambazo zinaweza kuletwa na ujenzi wa bwawa la maji la kuzalisha umeme katika stiegler’s gorge katika pori la akiba la Selous.

Kumekuwa na hisia tofauti kuhusu mada hii wengine wakiunga mkono maoni ya makala na wengine wakipinga hoja hii. wengine walienda zaidi na kudai kuwa mwandishi wa makala yale alikuwa anatumiwa na wageni.

Mara nyingi ni rahisi kupinga hoja kwa kurukia dhana ya kutumiwa, lakini tunachosahau ni kwamba Tanzania ya sasa ina wasomi wengi waliobobea pia katika sayansi ambao wana uwezo wa kujua madhara na faida ya vitu mbalimbali na kwamba mara nyingi mawazo haya siyo ya kigeni bali ya watu ambao wanaelewa, kisayansi, wanachokisema.

Kuna dhana kwamba maisha yote ni siasa na mtu huwezi kukwepa siasa. Wengine wanasema siasa ni mchezo mchafu na kwamba hakuna adui au rafiki wa kudumu katika siasa. Na siasa inakuwa na faida pale inapotumiwa kuleta maendeleo. Lakini, siasa inapogekuwa kuwa “Siasa” inakuwa haina maana yoyote ile. Ni bahati mbaya kwamba hapa Tanzania tunaelekea kuishi kisiasa, badala ya kuitumia siasa kuleta maendeleo.

Bahati mbaya vijana wetu wamedumbukia katika dimbwi hili la kuishi kisiasa na kuishi kishabiki. Ni wazi tumefanya kosa kubwa kama Taifa na gharama yake ni kubwa. Badala ya vijana wetu kushiriki shughuli za kuleta maendeleo na kulisogeza Taifa letu mbele, wanabaki kuishi maisha ya kisiasa na ushabiki. Vijana wetu hawana uwezo wa kujenga hoja na kuzitetea. Vijana wetu hawana uwezo wa kufanya utafiti na kuusimamia. Vijana wetu wanazikimbia hoja kwa kufuata mifano ya wazi kama vile Serikali kuyafungia magazeti. Sote tunajua sheria hizi za kufungia magazeti ni za kikoloni. Walizitunga sheria hizi kukimbia hoja za wananchi waliokuwa wakitaka uhuru wao. Hivyo bado tunaendeleza mifumo ya kikoloni ndani ya Taifa huru! Bado tunaogopa kujenga hoja na kuzitetea.

Mfano mzuri ni hoja hii ya sasa ya kutaka kujenga bwawa la kuzalisha umeme kwenye pori la akiba la Selous. Kuna wanaounga mkono hoja hii na wale wanaoipinga. Wale wanaounga mkono hoja hii, wanatumia mfumo wa kikoloni; wanafikiri wanaopinga ni wasaliti. Ukweli ni kwamba wote wanaopinga hoja hii na wale wanaoiunga mkono kama wanataka kuleta maendeleo katika Taifa letu, ni muhimu hoja zao zilenge kuitumia siasa kuleta maendeleo na wala si kuingiza siasa kwenye mambo ambayo yanahitaji utafiti na utaaalamu. Ni dhambi kuingiza ushabiki wa kisiasa kwenye mambo ambayo yanagusa uhai wa Taifa.

Kwamba wanaopinga ujenzi wa bwawa la umeme kwenye pori la akiba la Selous ni wasaliti, au kwamba wanalipwa na mashirika ya kigeni, kwamba wanampinga Mheshimiwa Rais Magufuli, ni kutaka kuishi kisiasa. Hoja hii si ya kibinafsi, hoja hii si kutaka kumfurahisha mtu mmoja, hii ni hoja ya Taifa letu, hii ni hoja ya kizazi hiki na kizazi kijacho. Maendeleo ni ya Taifa zima, hivyo mipango ya kuendeleza tiafa ni muhimu watu washirikishwe na wajadiliane kwa uhuru. Watanzania sasa hivi tuko zaidi ya milioni 50, hawa ni watu wengi ambao bila majadiliano ya uwazi na uhuru hatuwezi kufika mbali.

Mfano, sisi tunaopinga ujenzi wa bwawa hili, tunasema kwamba endapo Serikali itaamua kulijenga bwawa hili katika stiegler’s gorge, basi lazima tufanye utafiti mkubwa wa kisayansi unaojulikana kama Strategic Environmental Assessment,(SEA) utafiti ambao utatupa kwa kina, matatizo yanayoweza kuletwa na uchimbaji wa bwawa hilo. Ufaiti ni uchochezi? Utafiti ni kulipwa na mashirika ya nje? Utafiti ni usaliti? Tusipende kuishi kishabiki kwenye dunia ya leo ya sayansi na teknolojia.

Uzuri wa SEA ni kwamba ni utafiti wa kina ikilinganizwa na kile ambacho kinataka kufanywa na hivi sasa ambacho hakiendi ndani sana. Pia uzuri wa SEA ni kwamba ufatifi huo hauzuii ujenzi wa bwawa hilo, ila unawapa wajenzi na serikali matatizo ambayo yanaweza kuepukika au kupunguzwa wakati wa ujenzi wa bwawa hilo.

Ni muhimu tukajua faida na hasara za kulijenga bwawa. Tupime ili kuona ni kipi cha kuchagua. Lakini hata tukichagua upande wa hasara, tufahamu mapema njia za kufanya kupambana na hasara hizo. Watu wote duniani wanafanya hivyo kabla ya kuanza miradi mkubwa kama huu wa kujenga bwawa la kuzalisha umeme. Sisi hatuwezi kuwa tofauti.

Hata kama hatutaki kusikia kwamba pori la Selous ni urithi wa dunia na liko chini ya UNESCO kwa kuomba sisi wenyewe, basi tufanye SEA, ili tuwe tunajua yale yatakayojitokeza tukiendelea na mapango wetu na tujue jinsi ya kutanzua matatizo hayo. Kukubali kufanya SEA, ni kuitumia siasa kuleta maendeleo na kinyume chake ni kuishi kisiasa na matokeo yake si mazuri. Athari zake kama hazijaonekana leo, basi ni za vizazi vijavyo.

Kwa mfano moja athari inayoyakabili mabwawa ya aina hii na ambayo siyo tu yametengenezwa na binadamu, lakini yanatumia maji ya mto, ni kujaa kwa mchanga (siltation) na hivyo kupunguza kwa kina cha maj,. hii tayari iko katika bwawa la Mtera na maana yake ni kupungua kwa maji ya kuzalisha umeme.

Tatizo hilo hulioni kwa mabwawa kama yale ya Jinja, Uganda na yale ya Ethiopia kwa kuwa kwanza, vyanzo vya maji vya mabwawa hayo ni vya uhakika, kutoka mto Nile unalishwa pia na ziwa Victoria. kwa hiyo kuna uwepo mdogo sana wa mchanga, yaani siltation katika mabwawa hayo.

Mabwawa ya Mtera, Kidatu na Kihansi yanayotegemea, kwa kiasi kikubwa maji kutoka mto Ruaha mara kwa mara yamekuwa yakikabiliwa na kupungua kwa maji hata wakati wa mvua kutokana na uharibifu ambao umekuwa ukifanywa na binadamu kupitia kilimo cha umwagiliaji kisichozingatia utaalamu na uharibifu wa vyanzo vya mto huo unaotokana na mifugo.

Hali hii imekuwa ikitokea mara kwa mara katika eneo la vyanzo vya mto huo la Ihefu, mkoani Iringa na wakulima wa mpunga. ikiwa Serikali itaendelea na mpango wake wa kuchimba bwawa la maji la stiegler’s gorge, katika Mto Rufiji, inapaswa kuzingatiwa kuwa bwawa hilo litategemea maji kutoka Mto Rufiji.

Vyanzo vya Mto Rufiji ni pamoja na Mto Kilombero ambao unalishwa na maji kutoka vyanzo mito mbalimbali pamoja na vile kutoka bonde la Uoevu la Kilombero. Bonde hilo lina vijito zaidi ya 100, lakini hivi sasa sehemu kubwa ya vijito hivyo vimeanza kukauka kwa ajili ya shughuli za binadamu kupitia mifugo.

Kabla bonde hilo la Kilombero halijaingiliwa na kilimo cha miwa na shughuli zingine za binadamu, lilikuwa na wanyama pori wengi, pamoja na tembo jambo lililopelekea kuwapo kwa zaidi ya kampuni 12 za kitalii za uwindaji.

Lakini, baada ya kuingiliwa na shughuli hizo za kibinadamu, wanyama siyo tu wametoweka, lakini hata kampuni hizo za kitalii zimetoweka. hali hii ni mbaya hasa kwa nchi yenye maeneo makubwa ya kufanya shughuli za kibinadamu lakini watu wanang’ang’ania maeneo ya uoevu ambayo ndio vyanzo vya mito mingi hapa nchini.

Ninajua wazo hili la kujenga bwawa la kuzalisha umeme stiegler’s gorge limeshika kasi na ukizingatia Tanzania ya Viwanda tunayaoitamani, utaonekana msaliti ukiwa na mawazo tofuati, mimi binafsi sipingi hatua hiyo ya Serikali, lakini kama mwandishi na mtu anayelipenda Taifa lake, sipendi historia ituhukumu sote, hivyo ninatoa angalizo, ikiwa hatuwezi kudhibiti mifugo na shughuli zingine za kibinadamu katika vyanzo vya mito vinavyolisha mabwawa yetu ya kuzalisha umeme, ujenzi wa bwana la maji katika stiegler’s gorge hautotusaidia kupata kile tunachotaka, kwani kama tunapenda mifugo na bwawa, tutakachopata ni sifuli.

Kwani lazima tukumbuke kuwa maji ya Mto Rufiji yanafika mpaka kwenye Rufiji Delta, mdomo wa mto huo ambako kuna mikoko mingi ambayo ustawi wake unatokana na vitu mbalimbali ikiwemo uwepo wa maji ya kutosha kutoka katika Mto Rufiji.

Faida ya mikoko hiyo ni mazalia ya samaki wajulikanao kwa jina la kamba ambao tukiwatumia vizuri watatuletea fedha nyingi za ndani na nje ya nchi. Ujenzi wa bwawa la stiegler’s gorge una maana utaleta upungufu mkubwa wa maji katika Mto Rufiji chini ya bwawa hilo, yaani down stream. Hiyo moja tu ya athari ambazo zinaeleweka, lakini SEA ikifanyika, basi tunaweza kupata majibu ya athari nyingi ambazo zinaweza kuzuiwa wakati wa ujenzi.

Kwa hiyo kama tunataka kuendelea na mradi huo, basi tusilipue katika utafiti kwani itakula kwetu na hatuta kwepa lawama kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo. Lakini, kama tunataka kuondokana na lawama ya aina yoyote ile, basi tuachane kabisa na ujenzi wa bwawa hilo, kama nilivyosema katika makala yangu ya awali, hivi sasa tuna vyanzo vingi vya nishati kama vile gesi. Kwanini tunataka kuingia katika mradi huu wakati tuna gesi zaidi ya kutosha? mbali ya kuwa na gesi ya kutosha, tayari tunamaeneo tosha ya kupata nishati ya upepo, huko mkoani Singida na Makambako, mkoani Iringa. Ukiacha maeneo ya kutosha ya kuzalisha nishati kwa njia ya upepo, tunajua la kutosha kuzalisha nishati kwa kutumia solar.

Hizi ni hoja, na wala si kwamba tunatunga msaafu. Hoja hizi zijibiwe na hoja na wala si matusi na kujificha nyuma ya kivuli cha uzalendo. Pia si vizuri kumpotosha Rais wetu, kwa kujificha kwenye kivuli cha kumpenda na kumuunga mkono. Kumpenda Rais ni kumwambia ukweli. Sote kama Taifa tuna kazi ya kuitunza Tanzania na kuirithisha kwa vizazi vijavyo ikiwa salama na yenye tija kwa watu na viumbe vyote. Ndugu zangu watanzania tufanye siasa kuleta maendeleo, lakini tusiishi kisiasa!

Padre Privatus Karugendo.

pkarugendo@yahoo.com

+255 754633122.