In Summary

Ukiwa ni muda mfupi tangu iliposifiwa kwenye Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) ambao ni wa aina yake kwa nchi nyingi kusini mwa Jangwa la Sahara, sasa inatolewa mfano mwema kwenye uunganishaji wa umeme utokanao na wazalishaji wadogo au mini-grids.

Baada ya miaka mingi ya Afrika kuonekana ni bara lenye giza kwa wananchi wengi kutounganishwa na nishati ya umeme, Tanzania imetajwa kuokoa jahazi.
Ukiwa ni muda mfupi tangu iliposifiwa kwenye Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) ambao ni wa aina yake kwa nchi nyingi kusini mwa Jangwa la Sahara, sasa inatolewa mfano mwema kwenye uunganishaji wa umeme utokanao na wazalishaji wadogo au mini-grids.
Matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya kimataifa ya World Resources Institute (WRI) kwa kushirikiana Shirika la Kuendeleza Nishati Asilia (Tatedo) yamebainisha kuwa Tanzania ina sera bora zaidi za uzalishaji wa nishati Afrika.
Utafiti huo unaonyesha kuwa ifikapo mwaka 2040, zaidi ya Wafrika milioni 140 vijijini watakuwa wameunganishwa na umeme kutoka kwa wazalishaji wadogo 100,000 watakaokuwa na miradi ya aina tofauti inayozalisha chini ya megawati 10 kwenye maeneo husika.
Miradi hiyo, inaelezwa itasaidia kufikisha umeme wa gharama nafuu kwa wananchi hivyo kuwawezesha wananchi kuimarisha uzalishaji kwa kuongeza thamani mazoa yao.
Kwenye mpango huo, Tanzania ina zaidi ya wazalishaji wadogo 100 wengi wakiwa ni wajasiriamali binafsi, mashirika ya dini pamoja na baadhi ya vyama vya ushirika.
“Viongozi wa umma wanapaswa kujifunza kutokana na mafanikio ya Tanzania,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo iliyozinduliwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.
Ilibainishwa kwamba, Tanzania ina miradi midogo 109 yenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 157.7. Kwa miradi iliyoanza kutoa huduma, ripoti inasema zaidi ya wananchi 184,000 wameunganishwa ingawa wazalishaji wanasema idadi ni kubwa zaidi ya hiyo.
Mjeneja wa huduma kwa wateja wa Kampuni ya Husk Powering Possibilities ya nchini, Webster Magati anasema wananchi wengi wameunganishwa na nishati hiyo kutoka kwa wazalishaji wadogo hasa maeneo ambako si Shirika la Umeme (Tanesco) wala Mradi wa Umeme Vijijini (Rea) umefika.
“Tunazo mashine zinazotumia mabaki ya mazao kama vile karanga, vumbi la mbao, pumba za mpunga au magunzi ya mahindi kuzalisha umeme jadidifu. Zinaweza zikaunganishwa na paneli za umemejua pia,” anasema Webster.

Kuongeza matumizi ya umeme vijijini, anasema kampuni hiyo inajipanga kuwakopesha wananchi vifaa vinavyohitaji nishati hiyo ili kuwaongezea utulivu na kuboresha shughuli zao.

Umemejua umekuwa mkombozi hata kwa nyumba za hadhi ya chini vijijini. Miradi inayotekelezwa na kampuni pamoja na taasisi mbalimbali za ndani na nje imeongeza usambazaji wa vifaa kwa wananchi wengi kama wanavyoonekana wataalamu hawa. Picha ya Maktaba.

Utafiti

Kati ya mwaka 2008 na 2016, ripoti inasema miradi midogo 52 imesajiliwa na kufanya jumla kuwa 109. Kati ya hiyo, inayotumia maji ni 49, 25 za nishati jadidifu wakati 19 ikitumia gesi asilia na 13 umemejua. Licha ya uchache wa miradi ya gesi asilia, ndiyo inayozalisha umeme mwingi zaidi, asilimia 93 ya miradi yote.

Uzalisha huo wa umeme unaelezwa kuwanufaisha wananchi wengi wa vijijini waliochangamkia fursa kwa kuanzisha mashine za kukoboa na kusaga nafaka, kukamua mafuta, ukataji na uchomeleaji wa vyuma, ufugaji na utengenezaji wa juisi za matunda asilia.

Licha ya kuimariska kwa maisha ya familia, huduma za jamii kama hospitali na shule nazo zimeshamiri huku wananchi wakiweza kupata taarifa mbalimbali kama za masoko ya bidhaa na usafiri.

Pamoja na mafanikio hayo, ripoti inapendekeza taarifa za mafanikio na changamoto za kuanzisha na kuendesha miradi hii ziwekwe wazi ili kuwasaidia wajasiriamali wanaovutiwa kuwekeza.

Kuongeza tija, inashauri kuwajengea uwezo wawekezaji wadogo kwenye sekta hii waweze kuwasilisha madokezo yatakayowashawishi wabia. Inashauri taarifa za mafanikio ya miradi hiyo kwa jamii kuwekwa wazi na kuendele akufanya utafiti wa kubainisha changamoto zilizopo.

NBS

Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya upatikanaji umeme nchini iliyozinduliwa Februari, inaonyesha mpaka mwaka jana, asilimia 32.8 ya nyumba zote nchini zilikuwa zimeunganishwa na umeme kutoka vyanzo tofauti.

Kati ya nyumba hizo, robo tatu zilikuwa kwenye gridi ya taifa na asilimia 24.7 kutokana na ummemejua wakati asilimia 0.3 kutoka kwa wazalishaji binafsi. Mgawanyo wa uunganishaji wa nishati hiyo unaonyesha, ni asilimia 16.9 pekee ya kaya za vijiji zimeunganishwa ikilinganishwa na asilimia 65.3 za mjini.

Ripoti hiyo inaonyesha Dar es Salaam, Rukwa, Kilimanjaro, Kigoma na Arusha ndiyo iliyounganshwa kwa zaidi ya asilimia 80 na umeme wa gridi ya taifa wakati Dodoma, Ruvuma, Katavi, Mtwara, Njombe na Lindi zikitumia zaidi umemejua.

Kama inavyosema WRI, utafiti wa NBS uliofanikishwa kwa kushirikiana na Wakala wa Umeme Vijiji (Rea) unasema wananchi wengi wa vijijini wanatumia zaidi umemejua ukifuatiwa na gridi ya taifa. Zaidi ya theluthi mbili, asilimia 64.8 wanatumia chanzo hicho.

Mchango wa umemejua umesaidia kuboresha maisha vijijini. Ripoti inaonyesha: “Wanaotumia nishati hiyo wameongezeka kutoka asilimia 6.1 mwaka 2011 mpaka 16.9 mwaka 2016.”

Ofisa Miradi wa Kampuni ya Husk, Alex Mwalyoyo anasema wananchi wengi hasa vijijini wanatumia umeme kwa ajili ya kuangaza na kuchaji simu zao. Endapo watawezeshwa kwa namna nafuu wakapata vifaa vingine vinavyotumia nisha hiyo, maisha yatabadilika kwa kiasi kikubwa.

“Kuna vijiji vinaongoza kwa kilimo cha nafaka lakini havina mashine ya kukoboa wala kusaga. Hulazimika kusafiri mamia ya kilomita kufanikisha hilo au kutumia kinu cha mkono,” anasema.

Licha ya kuongeza vifaa vya umeme, anasimu teknolojia rahisi inayoweza kufika maeneo yenye changamoto nyingi zinahitajika kufanikisha usambazaji wa nishati hiyo.

Anabainisha miinuko mkali na kutawanyika kwa nyumba vijini kuongeza ugumu wa kusambaza umeme kwa njia za kawaida. Uwapo wa jamii zisizo na makazi ya kudumu mfano wafugaji ni suala jingine. “Wapo wanaoishi mbugani au miradi iliyojengwa kwenye hifadhi za taifa pia. Huko kote, umemejua ndio unakuwa suluhisho la kudumu,” anasema Mwalyoyo na kubainisha mpango wa kampuni yake kutekeleza ujenzi wa miradi 150 ndani ya miaka mitano ijayo.

Umemejua

Wakala wa Nishati Duniani (IEA), kwenye ripoti yake ya nishati jadidifu unasema kukabiliana na changamoto zilizopo, matumizi ya umemejua yataongezeka zaidi ya mara tatu ndani ya miaka mitano ijayo.

Ripoti hiyo iliyotolewa wiki iliyopita inasema umemejua utawafikia zaidi ya watu milioni 70 wa Asia na Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara. Mpaka mwaka 2022, IEA inasema zaidi ya megawti 3,000 za umemejua zitakuwa zinazalishwa.

Kampuni kadhaa zimeongeza ubunifu kuhakikisha fursa hii inatumika ipasavyo kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye jamii. Nchini Nigeria, mtandao wa Lumos kwa kushirikiana na Kampuni ya MTN unatoa huduma ya nishati hiyo kupitia simu za mkononi.

Kwa kununua kifaa maalum kiitwacho Y’ello Box, wateja wa mtandao huo wanaweza kupata nishati hiyo bila wasiwasi huku wakifanya malipo kupitia huduma za fedha za MTN.

Mkurugenzi Mtendaji wa Lumos, Yuri Tsitrinbaum anasema umemejua ni mbadala uliopo ambao unatoa nishati salama, nafuu na ya uhakika mahali popote walipo wananchi.

“Tunabadili namna watu wanavyoweza kupata umeme. Huu ni mwanzo tu. Simu za mkononi zimeleta mabadiliko makubwa ya kiteknolojia na sasa zinafanikisha upatikanaji wa umeme,” anasema.

Wadau wa nishati wanasema upatikanaji wa umeme ni muhimu kufanikisha mapinduzi ya sekta nyingi na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Rea, Dk Lutengano Mwakahesya anasema kwa alikuwa na wakala huo ameshuhudia mabadiliko mengi kwenye vijiji vilivyopata umeme.

“Wananchi hawahitaji kuhamia mjini bali huduma bora. Kuna vijiji vimebadilika ndani ya muda mfupi tangu vilipounganishwa kwenye umeme. Endapo hili litaendelea kupewa msukumo unaotakiwa, Tanzania itabadilika kw akiasi kikubwa,” anasema Dk Mwakahesya.