In Summary

Mtamahanji mwenye miaka 23 anasema kuwa haikuwa kazi rahisi kutambua anataka kuwa nani hadi baada ya kuingia darasani ndiyo alibaini ndoto alizokuwa akiota zinaelekea kutimia.

Siyo kutokana na kusoma katika chuo bora cha masuala ya teknolojia bali kwa utashi na kutamani kufika mbali ndiko kulikomfikisha George Mtemahanji alipo sasa.

Mtamahanji mwenye miaka 23 anasema kuwa haikuwa kazi rahisi kutambua anataka kuwa nani hadi baada ya kuingia darasani ndiyo alibaini ndoto alizokuwa akiota zinaelekea kutimia.

Mkurugenzi huyo wa kampuni ya Sun Sweet Solar Limited inayojishughulisha na usambazaji wa umeme vijijini kwa kutumia nishati ya jua anasema mafanikio aliyonayo sasa yalianza mwaka 2003.

“Nilikwenda Italia kumuona mama yangu ambaye anaishi huko, nikabahatika kujiunga na shule kuu ya Ferrari Institute of Technology kusomea masuala ya uhandisi wa nishati ya jua .

“Shule hii inaendeshwa na kampuni ya Ferrari inayojishughulisha na utengenezaji wa magari ya kifahari aina Ferrari ”.

Mtemahanji anasema aliishi nchini humo kwa miaka 10.

Anasema akiwa na miaka 18, alirudi Ifakara kuangalia namna anavyoweza kuyafanyia kazi anayoyawaza, na alipopata jibu akarudi nchini Italia kwa ajili ya kujipanga kabla ya kuanza kazi.

Anafafanua kuwa baada ya kufanya tafiti hapa na pale na kujiridhisha jinsi atakavyofanya kazi mwaka 2015 kampuni yao ya Sun Sweet Solar ilianza kufanya kazi rasmi.

Anasema licha ya kufanya kazi hapa nchini wana uhusiano mzuri na makampuni yanayouza vifaa vya nishati ya jua vyenye ubora duniani ambayo ni Sun Light (Ugiriki), Victron (Uholanzi) na makampuni mengine kutoka Italia na Ujerumani.

Kazi ya kwanza

Mtemahanji anasema baada ya usajili wa kampuni yao walipata kazi ya kufunga umeme katika shule ya sekondari ya wasichana Beniginisi iliyoko nje ya mji wa Ifakara ambayo walipatiwa na taasisi moja ya nchini Uswisi iliyogharimu Sh40 milioni.

Mafaniko ya Kampuni.

Anasema kwa mujibu wa African Leadership Academy wamefanikiwa kuwa katika orodha ya kampuni bora 12 zinazoendeshwa na vijana Afrika.

“Tulipata tuzo ijulikanayo kama Anzisha Prize na ilikuwa kazi ngumu kwani kati ya vijana 500 walioshindania tuzo hiyo yeye aliiwakilisha Tanzania, ” amesema Mtemahanji.

Wakati huo huo mwaka jana alipata bahati ya kuwa mmoja wa vijana sita Afrika waliofanya mazungumzo na tajiri namba moja duniani Bill Gates.

“Katika maongezi hayo nilizungumza naye kuhusu Ifakara na akanielewa na kuahidi kutoa mchango katika Taasisi ya Ifakara Health Institute, ” anasema.

“Nilijisikia furaha kuonana na tajiri namba moja duniani huku nikijiuliza nimeweza kuonana naye kirahisi kuliko ninavyokutana na viongozi wangu wa hapa nchini.

“Kwa mfano kuonana tu na mkuu wa wilaya ya Ifakara ni mbinde, ” anasema huku anacheka.

Mtemahanji ni miongoni mwa vijana wa Afrika walio chini ya miaka 30 wanaotegemewa kuwa mabilionea kwa mujibu wa orodha iliyotolewa na jarida la Forbes.

Changamoto

Mtemahanji anasema kubwa ni uelewa juu ya kutumia nishati ya jua katika maeneo mengi hasa vijijini.

Anasema licha ya hilo bado mchango kutoka serikalini ni mdogo hasa katika kuhakikisha wanawekewa mazingira rafiki hasa miundombinu ya barabara vijijini.

“Tunaomba serikali kutupa tenda kwani ni vijana wenye nia ya kukuza uchumi wetu hasa kwa kuzingatia nishati ya umeme ni muhimu kwa maendeleo ya taifa na kufikia azma ya uchumi wa kati na viwanda, ” anasema Mtemahanji.

Mtemahanji anasema serikali hasa Brela wasikwamishe ndoto za vijana wengi wenye nia ya kuwa wajasiriamali katika kufanikisha usajili wa makampuni yao.

Malengo.

Mtemahanji anabainisha ifikapo miaka kumi baadaye anategemea kuona vijiji vyote nchini vinapata huduma ya umeme hasa kupitia kampuni yake kwa kusambaza umeme wa nishati ya jua ambao ni rahisi kwa watu wenye kipato cha chini.