In Summary

Saida Karoli ametoa wimbo mpya uitwao ‘Urugambo’, wimbo ambao kwa jicho la kawaida kabisa unatosha kuwa moja ya bidhaa zinazohitajika kwa kiasi kikubwa katika soko la muziki la Tanzania na la kisasa.

Hivi karibuni mashabiki wa muziki Tanzania walipokea zawadi kutoka kwa Saida Karoli, mwanamuziki mkongwe ambaye alipotea kwenye tasnia ya muziki kwa takriban miaka minane, na si kwa sababu aliamua kupotea, bali ni kwa sababu ‘alifulia’ kisanaa, hakuna chombo cha habari kilichokuwa kinamtazama kama msanii mwenye jipya tena na idadi kubwa ya mashabiki waliaminishwa hivyo.

Saida Karoli ametoa wimbo mpya uitwao ‘Urugambo’, wimbo ambao kwa jicho la kawaida kabisa unatosha kuwa moja ya bidhaa zinazohitajika kwa kiasi kikubwa katika soko la muziki la Tanzania na la kisasa.

Kwanza ni kwa sababu ‘audio’ ya wimbo huo imetengenezwa kwa ubora wa kufanana na nyimbo nyingi za wasanii wanaovuma katika soko kwa sasa, na pili ni video yake ambayo nayo kwa ubora inalingana na video nyingi za muziki za wasanii wanaoshika chati hapa ndani.

La tatu ambalo ni kubwa zaidi ni kwamba, ‘Urugambo’ umekuwa ni wimbo wenye kuwakilisha muziki wenye asili ya Afrika kwa asilimia 100 kitu ambacho kimekosekana kwenye kazi nyingi za wasanii wa kizazi kipya hata wanaotawala soko na vyombo vya habari.

“Orugambo” ya Saida ni somo kubwa kwa wanamuziki wa kisasa ambao wengi wamesahau ubunifu badala yake wamekuwa ni watu wa kuiga muziki wa watu wengine na wakati mwingine kufanya kazi kwa staili ya kulipua.

Namba kubwa ya wasanii wa kizazi kipya wamejikita zaidi katika kuimba miziki yenye asili ya Marekani, Kusini mwa Afrika na Afrika Magharibi, muziki kama Kwaito kutoka Afrika Kusini, fleva za kutoka Nigeria, Hip Hop na R&B kutoka nchini Marekani wakati Tanzania tuna aina yetu ya midundo ambayo ikiongezewa ubunifu na kuchukuliwa kuwa ya kisasa zaidi inaweza kuvuka mipaka na kututangaza bila maandishi.

Idadi kubwa ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya wana ndoto ya kuwa wasanii wa kimataifa lakini wanashindwa kuifanya kweli kwa sababu hawana jipya katika kazi zao.

Kama kuwa wa kimataifa kuna maanisha nyimbo zake zipigwe Afrika kote na nje ya Afrika basi ni lazima kama msanii uje na bidhaa yenye tofauti na zile zilizozoeleka kusikilizwa huko.

Tatizo letu ni kwamba wasanii wetu walio wengi wanataka kuwa wa kimataifa, wanataka nyimbo zao zichezwe kwenye vituo vya redio na televisheni za Nigeria, wakati wanaimba kama Davido, wanatamani muziki wao uchezwe kwenye klabu za Afrika Kusini wakati uimbaji wao hauna tofauti na A.K.A na Mafikizolo, na wanatamani kupata nafasi ya kufanya kazi na wasanii wakubwa kutoka Marekani ilihali kazi zao za kisanaa wanazozifanya kwa kumuiga Drake, wanaimba kama Chris Brown na kuvaa kama Rihanna kwenye video zao.

Si muziki tu, biashara yoyote ile duniani inahitaji utofauti kwa sababu akili za wanunuzi au wateja wengi zinapenda kupata vitu ambavyo si vya kawaida, vitu ambavyo ni tofauti na vile wanavyovipata kila siku.

Msanii anapoamua kuimba R&B kama ya Usher Raymond na kutaka ivume Marekani ni ujinga, ni sawa na kulima karafuu Kigoma na kwenda kuziuza Zanzibar, hakuna mteja atayejishughulisha hata kuuliza bei.

Wasanii wa Kizazi kipya hasa wanaouvuma kwa sasa na wenye ndoto za kwenda kimataifa wanatakiwa kufahamu ukweli kwamba ili wafike huko ni lazima wafanye vitu vya utofauti vya upekee na si kung’ang’ania kufanya vitu vile vile na kutegemea matokeo tofauti, hilo ndilo somo wanalotakiwa kulipata mapema kutoka katika ‘Orugambo’ ya Saida Karoli kabla haijaingia kwenye damu ya kila mpenda wa muziki.

Kwa hiyo uamuzi wa Saida Karoli kuja na ubunifu mpya bila shaka unaweza kuwaamsha wasanii wengine wakatafakari ni vipi wanaweza kuja kivingine katika soko la muziki badala ya kuangalia wasanii wa Marekani, Nigeria au Afrika Kusini wanafanya nini na kuiga kila kitu.

Kwa wanaomfahamu Saida Karoli enzi zile akitamba na albamu yake ya Kanichambua kama Karanga hapa shaka watakuwa wamekumbushwa kitu kutoka kwa msanii huyu.

Miongoni mwa mambo yaliyompa umaarufu Saida katika kibao hicho ni umahiri wake wa kulitawala jukwaa, sauti yake ya kuvutia na zaidi namna alivyozipa uhai ngoma za asili ya kabila la wahaya na kuchanganya na Kiswahili.

Vionjo hivyo ndivyo vilivyomfanya Saida kupata mialiko katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na hata Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Huo ndio wakati ambao Saida alidhihirisha ubora wake na haikushangaza alipopata mwaliko wa kufanya ziara nchini Uganda kwa mara ya pili ikiwamo kufanya onyesho maalum kwa Kabaka wa Buganda.

Kwa hali hiyo anachokifanya Saida kwa sasa kupitia Urugambo, baada ya ukimya wa muda mrefu kitoshe kuwa ukumbusho muhimu kwa wasanii wengine nchini kuthamini ubunifu.