In Summary
  • Ukiisoma haraka haraka unaweza usielewe, lakini ni ukweli usiopingika familia nyingi zinaathiriwa na jambo hili.

Inawezekana usiwe wewe au mimi lakini umewahi kusikia wanandoa waliochokana kiasi cha kutengana vitanda na hata vyumba.

Ukiisoma haraka haraka unaweza usielewe, lakini ni ukweli usiopingika familia nyingi zinaathiriwa na jambo hili.

Kuchokana kwa wanandoa kunapimwa kutokana na kila mmoja kutokuwa na hamu na mwenzake iwe ya kuzungumza, kutoka pamoja au ushirikiano wa aina yoyote.

Wengine huenda mbali zaidi na kuonyesha hili hata mbele za watu kwa kupuuza kila linalosemwa na mwenza wake.

Hali hii inapotokea huleta msukumo kwa mmoja wa wanandoa hao kutoka nje ya ndoa.

Wataalamu wamezitaja sababu tano zinazochangia wanadoa kuchokana.

Chausiku Salumu almaarufu Bi Chau anasema kuwa wanandoa wengi wanakosa baadhi ya sifa za kuwa mwili mmoja hivyo kusababisha ndoa kuyumba.

Anasema baadhi ya sifa ni pamoja na kutosomana tabia, kuwa marafiki, kutozungumza, kupeana zawadi, kualikana vyakula.

Anasema ni nadra kwa wanawake walio wengi wa Kiafrika kuwaalika au kuwanunulia zawadi wenza wao, huku mwanaume hata kama amekosea ni ngumu kukiri kosa.

Anasema wanandoa wengi wapo radhi wawaalike marafiki kwa ajili ya chakula cha jioni au nje ya nyumbani kuliko kualika wenza wao , jambo ambalo hulifanya wanapokuwa wapenzi kabla ya kuoana.

Anafafanua mbali na hilo hawasomani tabia kiasi kwamba hata faragha hukutana kwa mazoea na kusahau kila mmoja kati yao ana wajibu wa kukata kiu ya mwenza wake kwa sababu yeye ndiyo ameruhusiwa kisheria kufanya hivyo.

“Akikosa anachokipata ndani, akakosa muda wa kuzungumza kufahamu nini tatizo, akakosa wa kumuuliza mbona hauko sawa kwa sababu hajasomwa tabia yake atabaki na hayo machungu na kuamua kutafuta pa kuyatua.

“Akipata pa kuyatatua anasahau ndoa kwa mwanaume, mwanamke anakuwa na dharau kwa sababu amepata mtu anayemshughulikia atakavyo, matokeo yake ndoa inayumba au kuvunjika kabisa, ” anasema.

Anasema wanandoa pia wanatakiwa kukumbuka kusema kweli kwa yale wasiyoyapenda ni suluhisho badala ya kujidanganya wao wenyewe.

Anafafanua kuwa kuna baadhi ya mila wanawake wanapaswa kuziacha ikiwamo kuridhika wanapowaridhisha wame ao hasa faragha na kujikuta wao wakiwa watumwa wa huduma hiyo.

“Ndiyo maana nasisitiza mazungumzo kwa wenza, hapa ndiyo unatakiwa useme kila ambalo haliko sawa bila kuficha ili kulinda na kuipa heshima ya milele ndoa yako, ”anasema Bi chau.

Anafafanua kuwa ndoa ikifikia hali hii inahitaji uangalizi maalumu na daktari maalumu kwa sababu inakuwa mahututi.

Sifa hizo pia zinatajwa na mtaalamu wa saikolojia Modester Kamongi anayesema kuwa kuzungumza, kutoka kwa ajili ya matembezi, kusomana tabia ni miongoni mwa dawa zinazoimarisha ndoa.

Kamongi anasema pamoja na kuwa zipo sababu nyingi kulingana na aina ya ndoa, lakini hizo zinaweza kuwa msingi wa kubaini mengine mengi.

Anafafanua kuhusu kuzoeana kuwa ni jambo zuri kwa sababu humpa nafasi kila mmoja kufahamu mwenzake na kuwa rahisi kubaini mambo mengi.

Anaeleza kuwa udhaifu mkubwa wa wanadoa wa siku hizi ni kutosomana tabia.

Anasema siyo ajabu kuwakuta wanandoa wametimiza miaka miwili hadi mitatu lakini hakuna anayemfahamu mwenzake anapenda nini na hapendi nini.

“Hapa kila mmoja atataka tabia zake ziwe dira ya kuongoza nyumba au maisha yao, kumbe wangesoma mmoja kati yao angehama kutoka kwenye baadhi ya tabia zake na kuanisha na za mwenzake wakaenda sawa, ”anasema Kamongi.

Anayataja mazungumzo kuwa dawa na tiba ya ndoa nyingi lakini anayetaka kuyafanya na kuyatumia kwa minajili hiyo huonekana dhalili na anayekubali kushindwa kirahisi.

“Kama hakuna hii nafasi ya kukaa pamoja mkajadili hata mustakabali wa watoto utakuwa mashakani.

“Wanaweza kuumwa, kukosa ada, kujiingiza kwenye matendo maovu, kama hamzungumzi kila mmoja atajaribu kuyatatua kivyake na hapo kushindwa ni kwa asilimia kubwa, ”anasema mtaalamu huyo wa saikolojia.

Anafafanua kuwa jambo jingine wengi wao hawapo wazi katika mapenzi ikiwamo kueleza wanataka kufanyiwa nini na wakati gani, huku wanaume wakiwa wagumu kuwaeleza wenza wao kuwa wanawapenda.

Hata anapoulizwa na mwenza wake unanipenda jibu huwa la mkato “Si ndiyo maana nikakuoa”.

Anasema kuna vitu vinadumisha ndoa na kuisisimua ikiwamo kupeana zawadi, kualikana kwa ajili ya chakula na vitu hivyo havihitaji gharama kubwa zaidi ya upendo wa kweli.

Anasema wanandoa huchukuliana poa jambo ambalo ni hatari, ndoa uhitaji kuchachuliwa mara kwa mara kwa kufanya vitu hivi na vile.

“Hata ukibadili mpangilio wa nyumba, ukijipura ukang’ara kwa wanawake hii huchangia kusisimua ndoa, badala ya kukaa kihasara hasara.

“Wanaume pia vijizawadi hata kama ni kashata ya Sh 100 ukimpa mkeo anakumbuka enzi zenu mkiwa ndiyo mnakutana hiyo itamfanya aone bado unamuona mbichi, ”anasema.

Kauli hizo zinaungwa mkono na Makamu mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Utawala Fedha na Mipango Dk Zena Mabeyo anayesema sababu kubwa wengi wao hawapo tayari kusomana tabia.

Anasema wengi wao wanasahau kuwa ndoa ni maisha ya kila siku na wanapaswa kuwa mwili mmoja, badala yake wanapendana na kushirikiana kwa nyakati.

Anasema kukwepa kusomana, kukuzungumza pamoja na kupata muafaka wa changamoto, mitihani wanayopitia kunasababisha ndoa nyingi kutetereka.

Anazitaja faida za kusomana tabia na kuzungumza kuwa kunasaidia kupata ufumbuzi wa masuala mengi.

“Ukiijua tabia ya mwenzako akiwa na fedha anakuwaje, akiwa hana anakuwaje, akikwazika kazini anakuwaje, huwezi kupata shida na utabadilika kulingana na hali halisi.

“Usipomfahamu utaishia kugombana naye.

Anasema mazungumzo yatasaidia kuondoa kero ndogondogo zinazoikabilia ndoa kwa sababu kati ya wawili hao hakuna anayejigamba kushinda.

Dk Zena anasema wanandoa pia wanapaswa kutambua tabia na mienendo ya familia zao ili kukwepa kuvuruga ndoa zao kwani imebainika wanafamilia huchangia kwa kiasi fulani kuziyumbisha.

Anaitaja tiba nyingine kuwa ni wanandoa kujitahidi kuwa na subira, uvumilivu na kutambua kuna kipindi cha neema na mapito magumu.

“Hizo sababu nilizozianisha zinaweza kuwa ni ufunguo wa kufahamu mengi zaidi, ukisoma tabia ya mwenza wako akibadilika utafahamu mapema na kuzuia mabadiliko hayo.

“Akiwa na hali ngumu kiuchumi utafahamu mapema na kuishi kulingana na hali halisi, ukijadiliana naye kama una chuki naye atakubali kosa na mtaanza upya, hayo yanabaki kuwa mambo makuu katika ndoa, ” anasema.

Wanandoa wengi wanapimana ubavu, badala ya kujadili kama mwili mmoja kutatua changamoto, kila mmoja anataka kujionyesha hajali uwepo wa mwenzake na kuishia kulumbana.

Anasema wanaosababisha kuchokana katika ndoa ni wanandoa na wanaoweza kuzifanya ndoa ao kuwa mpya kila kukicha ni wanandoa na bila kuyaangalia kwa makini baadhi ya mambo yanayokwamisha nyingi zitaishia chumba cha uangalizi maalumu.