In Summary
  • Kama tunavyokitazama chakula, iko haja pia ya kuvipa umuhimu vyoo katika mazingira yoyote ya binadamu.
  • Kwa wale wenye uzoefu na ujenzi watakubaliana na ukweli kuwa, hata kabla ya kuanza kujenga nyumba, moja ya mahitaji ya msingi ni kuwa na tundu au matundu ya vyoo kwenye eneo la ujenzi kwa minajili ya kuwasitiri wajenzi.

Vyoo ni moja ya mahitaji muhimu katika maisha ya binadamu kama ilivyo chakula.

Kama tunavyokitazama chakula, iko haja pia ya kuvipa umuhimu vyoo katika mazingira yoyote ya binadamu.

Kwa wale wenye uzoefu na ujenzi watakubaliana na ukweli kuwa, hata kabla ya kuanza kujenga nyumba, moja ya mahitaji ya msingi ni kuwa na tundu au matundu ya vyoo kwenye eneo la ujenzi kwa minajili ya kuwasitiri wajenzi.

Hata hivyo, hali iko tofauti katika ujenzi wa baadhi ya shule nchini. Si jambo geni kusikia shule imefungwa kwa kipindi kisichojulikana kutokana na ukosefu wa matundu ya vyoo.

Licha ya changamoto hii kuripotiwa katika vyombo mbalimbali vya habari, bado inachukuliwa kama jambo lisilo na umuhimu.

Kwa mujibu wa miongozo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, tundu moja la choo linapaswa kutumiwa na wastani wa wanafunzi wasichana 20; na kwa upande wa wanafunzi wavulana, tundu moja la choo linapaswa kutumiwa na wanafunzi 25.

Lakini takwimu za elimumsingi mwaka 2013 zilionyesha kuwa, tundu moja la choo linatumiwa na wanafunzi wasichana 51 badala ya 20 na kwa upande wa wavulana tundu moja linatumiwa na wanafunzi 53 badala ya 25.

Kwa mujibu wa takwimu hizo kwa mwaka 2016, Mkoa wa Geita ndio ulioongoza kwa kuwa na uhaba mkubwa wa matundu ya vyoo.

Mikoa ya Kilimanjaro na Iringa pekee ndio mikoa iliyoonekana kuwa na afadhali katika idadi ya matundu ya choo, huku kiwango cha watumiaji ikikikaribia kile kilichowekwa na Serikali yaani tundu moja la choo kutumiwa na wasichana 20 na 25 kwa wavulana

Pamoja na takwimu hizi, bado tatizo ni kubwa zaidi kwani baadhi ya shule tundu moja la choo hutumiwa na wanafunzi zaidi ya 200 na shule nyingine hazina vyoo kabisa. Kwa mujibu wa takwimu hizo, kuna upungufu wa matundu ya vyoo kwa asilimia nyingi katika shule za msingi hapa nchini.

Kuongezeaka kwa idadi ya shule pamoja na wanafunzi wanaoandikishwa katika shule za msingi, ni moja ya mafanikio makubwa katika sekta ya elimu.

Lakini mafanikio haya yamesababisha uhaba mkubwa wa miundombinu ya shule hasa matundu ya vyoo.

Hivi karibuni nilitembelea baadhi ya shule katika wilaya kadhaa hapa nchini. Kimsingi changamoto hii ni kubwa kuliko tunavyofikiri, kwani imesababisha hata baadhi ya wanafunzi, hasa wasichana kuwa watoro kutokana na kukosekana kwa mazingira rafiki ya kujisitiri.

Katika shule nilizopita na kuzungumza na walimu pamoja na wanafunzi, vyoo vilivyopo vinahatarisha afya na hata maisha yao.

Vyoo vingi vilivyopo ni chakavu na havikidhi mahitaji halisi ya wanafunzi. Aidha, kutokana na uhaba mkubwa na uchavu wa vyoo hivyo, wanafunzi wengi hujisaidia vichakani au kwenye mashamba yaliyopo karibu na shule hali ambayo ni hatarishi kiafya.

Lakini pia changamoto hii inawaathiri zaidi wanafunzi wa kike hasa wale ambao walishafikia umri wa kuvunja ungo, wanaohitaji mazingira safi kujisitiri hasa wanapokuwa katika siku zao.

Inasikitisha zaidi pale ambapo hata walimu wanalalamika kukosekana kwa matundu ya vyoo ya kukidhi mahitaji yao. Hali hii inawafanya baadhi ya walimu kutumia vyoo vile vile vibovu wanavyotumia wanafunzi wao.

Madhara ya kukokuwa na matundu ya vyoo shuleni ni makubwa kuliko tunavyodhani. Walimu na wanafunzi niliozungumza nao walieleza uwepo wa magonjwa ya mlipuko kama vile; kuharisha, kutapika, minyoo na kudhoofu kwa afya za wanafunzi hasa wa madarasa ya awali, la kwanza na la pili kwani na wao hutumia vyoo hivyo hivyo vibovu.

“ Watoto kama wa darasa la awali, la kwanza na la pili,wanajisaidia huku wameshika chini. Kila siku watoto wasiopungua nane wanaugua na tunawaruhusu kwenda nyumbani, na wakienda nyumbani si wote wanaopelekwa hospitali,’’ alinieleza mwalimu mmoja.

Ukosefu ama uhaba wa vyoo, ni changamoto inayoonekana ya kawaida, lakini ni moja ya vikwazo vinavyochangia kushuka kwa uelewa wa wanafunzi darasani sambamba na ufaulu katika mazoezi na mitihani mbalimbali.

Ni dhahiri kuwa mtu anapokuwa amebanwa na haja kubwa au ndogo hawezi kutulia na kuzingatia katika kile anachokifanya.

Shime kwa Serikali, wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo, muda umefika sasa wa kuitatua changamoto hii kwa vitendo.

Kama ambavyo tumeweza kuunganisha nguvu zetu katika ujenzi wa maabara kwa shule za sekondari, nguvu hiyo pia itumike katika kuhamasisha ujenzi wa miundombinu ya vyoo, tukianzia na shule za msingi ambako kuna upungufu mkubwa.

Ni aibu kungoja vyoo vya muda vilivyopo vititie au visababishe maafa kwa watoto wetu ndipo tuchukue hatua.Hakuna muujiza wowote unaoweza kuleta mabadiliko kwenye elimu yetu.