In Summary
  • Mwalimu Nyerere alikuwa na mitizamo mbalimbali kwa mambo tofauti. Alifahamika kwa hilo kiuchumi, kisiasa na katika baadhi ya mambo ya kijamii.

Kila Oktoba 14 ni siku ya kumkumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Kwa wanaomfahamu, Mwalimu Nyerere hakuna haja ya kutoa maelezo zaidi. Kwa ambao hawamfahamu, hamna maneno ya kutosha ya kumuelezea.

Mwalimu Nyerere alikuwa na mitizamo mbalimbali kwa mambo tofauti. Alifahamika kwa hilo kiuchumi, kisiasa na katika baadhi ya mambo ya kijamii.

Kati ya mambo yanayomtambulisha Mwalimu Nyerere kuhusu umiliki wa uchumi ni siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na Azimio la Arusha la mwaka 1967. Mwalimu aliamini katika uchumi ambao njia kuu za kuzalisha mali zinakuwa chini ya umiliki wa serikali.

Njia hizi ni pamoja na viwanda, mashamba makubwa, migodi, taasisiza fedha, hoteli na kadhalika. Hili linaonekana katika Azimio la Arusha pale ulipofanyika utaifishaji wa njia kuu za uchumi.

Hizi zilitoka kwenye umiliki binafsi na kuwekwa katika mikono ya serikali. Aliamini katika uchumi hodhi wa umma. Sekta binafsi kama tunavyoielewa leo haikuwa na nafasi kubwa katika uchumi wa nchi enzi za Mwalimu. Mali za sekta binafsi zilitaifishwa.

Baadhi ya mitizamo ya Mwalimu haionekani kuwa na nafasi kubwa kwa mazingira ya leo baada ya mageuzi ya kisiasa na kiuchumi katikati ya miaka ya 1980. Mageuzi ya kiuchumi yalibadili uchumi hodhi wa serikali na kuwa wa sekta binafsi.

Majukumu ya serikali yalibadilika kuwa ya kuweka mazingira rafiki, wezeshi na ya kuvutia uwekezaji. Tofauti na mtizamo ya Mwalimu, mali zilibinafsishwa.

Kujitegemea

Mwalimu aliamini katika kujitegemea kiuchumi. Hii inatokana na kuelewa changamoto za nchi kuwa tegemezi ambazo ni pamoja na masharti magumu na wakati mwingine yasiyokubalika, misaada kutotolewa kwa wakati na kiasi kama inavyoahidiwa, nchi kutokuwa na uhuru wa kujiamulia mambo yake.

Ili kutimiza azma ya kujitegemea, ni muhimu kwa nchi kukusanya kodi ya kutosha. Kodi husaidia serikali kuwa na vyanzo vyake vya ndani vya mapato hivyo kupunguza utegemezi.

Uchumi wa viwanda

Mwalimu Nyerere aliweka misingi ya mambo mengiv ikiwamo viwanda. Tukiwa katika azma mpya ya uchumi wa viwanda, ni muhimu kukumbuka kuwa Mwalimu alifanya mengi kuvihusu.

Enzi zake mipango kadhaa ya maendeleo ilitoa vipaumbele katika uchumi wa viwanda. Hii ni mipango ya kuanzia miaka michache baada ya uhuru hadi mwishoni mwa miaka ya 1970.

Pamoja na mambo mengine, Mwalimu aliamini katika viwanda vidogovidogo, viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo, viwanda vya kuongeza ajira kupitia kufanya kazi wa mikono zaidi kuliko kwa mitambo.

Mikakati ya Mwalimu kuhusu uchumi wa viwanda ni pamoja na kuwa na viwanda vya kuzalisha bidhaa ambazo zingechukua nafasi ya zile zilizokuwa zikiingizwa kutoka nje ya nchi.

Katika zama hizi, itakuwa muhimu kujifunza na kuchota katika fikra za Mwalimu kwa kutizama nini kilifanikiwa, nini hakikufanikiwa na zaidi, kwanini. Pale ambapo fikra zake hazikufanikiwa itakuwa muhimu kujua kwanini na nini kifanyike tofauti.

Kulinda wazalishaji

Kati ya maandishi ya Mwalimu Nyerere ni yale yanayohusu kulinda wazalishaji wa ndani dhidi ya ushindani. Mwalimu alitambua kuwa wazalishaji wadogo wa ndani lazima walindwe dhidi ya ushindani kutoka nje kama nchi inataka kuwapa nafasi ya kukua.

Mjadala na uchambuzi wa jambo hili la kulinda wazalishaji ni muhimu si tu kwa wakati wa Mwalimu bali hata zama tulizonazo. Ushindani ni afya na mzuri hasa kwa walaji. Ushindani wenye afya unapaswa kuongeza ubora wa bidhaa na kupunguza bei.

Hata hivyo kabla ya kushindana ni vizuri wazalishaji wakalindwa ili wakue na kupata misuli ya kushindana. Ni muhimu kuona inaweza isiwe afya kulinda wazalishaji ambao hawataweza kukua, kuwa na ufanisi na kushindana.

Pia si afya kiuchumi kulinda baadhi ya wazalishaji bila ukomo. Baada ya muda fulani ni lazima mtoto akue, ahitimu na kwenda katika ngazi nyingine katika safari ya kukua na kushindana.

Kukusanya kodi

Mwalimu alitaka serikali ikusanye kodi kutoka kwa wananchi na kampuni makubwa pia. Hizi ni fedha zinazohitajika kuiwezesha serikali kutoa bidhaa na huduma za jamii kama vile elimu, afya, maji, miundombinu, ulinzi na usalama.

Mtizamo huu una mantiki katika zama hizi pia. Kodi huifanya serikali iweze kugharamia huduma za jamii na walipa kodi kuwa na uthubutu wa kuiwajibisha serikali.

Wananchi wakilipa kodi watakuwa na nguvu na mamlaka ya kuidai serikali huduma za jamii. Kama wananchi hawalipi kodi serikali italazimika au kukopa au kutegemea misaada. Katika hali hii, serikali itajikuta ikiwajibika zaidi kwa wakopeshaji na wahisani kuliko wananchi.