In Summary
  • Kijana huyo, 36, amenuia kupunguza utegemezi wa mapato yatokanayo na tozo mbalimbali za kampuni za ndege na kuongeza ya vyanzo vingine kutoka asilimia 31.5 ya mwaka wa fedha 2016/17 mpaka asilimia 60 miaka mitatu au minne ijayo.

Dar es Salaam. Wiki moja baada ya kuteuliwa kuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela amedhamiria kupunguza gharama za uendeshaji kampuni ya ndege.

Kijana huyo, 36, amenuia kupunguza utegemezi wa mapato yatokanayo na tozo mbalimbali za kampuni za ndege na kuongeza ya vyanzo vingine kutoka asilimia 31.5 ya mwaka wa fedha 2016/17 mpaka asilimia 60 miaka mitatu au minne ijayo.

Gharama zinazotozwa kampuni zinahusisha tozo za kutua na maegesho ya ndege, vyanzo vingine vya mapato ni pango la jingo kwa wapangaji walio na ofisi tofauti uwanjani, matangazo na ada ya maegesho ya magari kwa abiria na wasindikizaji.

Ndege zenye uzito mpaka tani 20 hutozwa Sh1,000 kwa saa 12 kwa kampuni zilizosajiliwa nchini na Dola 5 za Marekani (zaidi Sh11,000) kwa kampuni za kigeni. Zenye kati ya tani 20 hadi 60 ni Sh1,000 kwa saa sita kwa kampuni za ndani na Dola 5 kwa kampuni za kigeni. Gharama za ndege kutua katika viwanja vya ndege vya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Zanzibar na Pemba ni Dola tano.

Mayongela, baba wa watoto watatu, anasema mwaka huu wa fedha mamlaka hiyo inatarajia kuongeza mapato ya vyanzo vingine kutoka asilimia 31.5 mwaka jana mpaka asilimia 41.5 ya Sh119.62 bilioni inayotarajiwa kukusanywa. Kiwango hicho kipo chini ya wastani wa dunia ambao ni asilimia 47.

Kwa mujibu wa takwimu za mamlaka ya viwanja vya ndege, mwaka wa fedha 2016/17, kati ya Sh59.3 bilioni zilizokusanywa, tozo za kampuni za ndege zilichangia asilimia 68.5.

Hii ina maanisha kwamba kama mamlaka hiyo inataka iongeze mapato kutoka vyanzo vingine vya mapato kwa asilimia 60, inatakiwa iongeze mchango wa sasa wa mapato hayo kwa zaidi ya mara mbili.

Wakati mamlaka hiyo imevalia njuga suala la kuongeza mapato yatokanayo na vyanzo vingine, mapato hayo yamekuwa yakikua kwa wastani wa asilimia 19.1 kwa miaka mitano iliyopita, mkubwa ukiwa asilimia 28.5 ulioripotiwa mwaka wa fedha 2015/16, kabla ya kushuka mwaka uliofuata.

Kwa sasa, pango huchangia takriban asilimia 80 ikifuatiwa na tozo za maegesho za magari kwa asilimia 11.8.

“Tunafanya mapitio ya mikataba yote ili kuongeza tija. Tunatarajia kuingia mikataba mingine mipya ambayo itakuwa ya faida kwetu na tutakaofanya nao biashara,” anasema bosi huyo mpya, ambaye kabla ya uteuzi wake Septemba 25, alikuwa ni kaimu mkurugenzi wa fedha na biashara wa mamlaka hiyo.

Mayongela, ambaye kabla ya kujiunga na mamlaka ya viwanja vya ndege alikuwa mtumishi wa Benki ya Uwekezaji kwa miaka minne, anaamini utegemezi wa vyanzo vingine vya mapato tofauti kutafanya viwanja vya ndege vivutie wawekezaji binafsi hivyo kuongeza mchango wake kwenye uchumi na Pato la Taifa.

Mayongela, kutoka Wilaya ya Bariadi anasema mamlaka yake inafanya jitihada kuhakikisha mipango hiyo inatekelezeka. Amesema milango iko wazi kwa sekta binafisi kuingia ubia na serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ambayo itafanya mapato yaongezeke.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa hoteli ya nyota nne itakayogharimu Sh15 bilioni na ujenzi wa ukanda maalumu wa kiuchumi na soko kubwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Miradi mingine ni ujenzi wa hoteli na kituo cha mikutano katika viwanja vya Arusha na Mwanza na ujenzi wa hoteli ya nyota tatu katika viwanja vya Songwe na Mtwara.

Katika mikakati hiyo pia, kuna ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Msalato-Dodoma utakaogharimu Dola 200 milioni za Marekani, Uwanja wa Ndege Bagamoyo utakaogharimu Dola billion moja, maboresho ya Uwanja wa Arusha kwa Dola 125 milioni na Mtwara Dola 41.3 milioni.

Miradi mingine ni maboresho ya viwanja vya Tanga kwa Dola 30.8 milioni na Lindi Dola 38.7 milioni.

“Tumemaliza kufanya upembuzi yakinifu katika miradi yote. Milango ipo wazi kwa wawekezaji walio tayari,” anasema Mayongela.