Swali kuu sasa katika nyumba ya Muungano wa Nasa ni nani kati ya Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula na Raila Odinga anamsaliti mwenzake?

Swali hili limejiri baada ya Raila kuwashauri wafuasi wake wawe tayari kukabiliana na usaliti unaokaribia mlangoni kwao, lakini ghafla yeye akaibukia Ikulu na kufanya makubaliano ya amani ya Kenya na Rais Uhuru Kenyatta.

“Ninafahamu kuna Yudasi katika Nasa ambaye yuko tayari kunisaliti,” alisema Raila katika shughuli ya mazishi nchini humo.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Raila kuzungumza kuhusu usaliti katika muungano wake akisema wafuasi wa Nasa watasalitiwa wakati wowote na wale wanaojifanya ni marafiki kumbe ni mbwa mwitu waliovalia ngozi ya kondoo.

Akisema kimya chake kuhusu suala hili lilikuwa njia moja ya kusoma fikra za viongozi wenza wa Nasa, Raila alitumia misemo na methali kufikisha ujumbe wake kwa wafuasi wake.

Ingawa hakutaja wale watakaomsaliti, Raila alisema hatashangazwa ikiwa watu fulani wataacha safari yake ya kuleta mabadiliko si haba nchini.

Alifananisha usaliti wake na ule aliofanyiwa Yesu Kristu aliyesalitiwa na mmoja wa wafuasi wake Yudas Iskarioti aliyemuuza kwa waliomuua na kumsulubisha msalabani. Kinara huyo wa Nanasa anasema wale wanaopanga kujiondoa kutoka kwa safari ya kuelekea Kanaani ni watu waoga wasiofaa kutegemewa.

Yeye ageuka ghafla

Machi 09, 2018 Rais Uhuru Kenyatta na Rais aliyejiapisha kuongoza watu wa Kenya, Raila Odinga, walikutana katika ikulu ya Kenya kwa saa kadhaa na kisha wakafanya mkutano na wanahabari kuelezea mazungumzo yao.

Raila na Uhuru wameweka wazi kwamba mkutano wao umefanyika kwa kuweka mbele maslahi ya Wakenya na lengo lao ni kutafakari hali ya nchi, kutafuta mbinu za kuondoa migawanyiko na kurudisha mshikamano. Wamesisitiza kuwa wanahitaji kutatua changamoto ambazo zimeendelea kuukumba mfumo wa kiuchaguzi katika nchi yao.

Kwa vyovyote hatua hiyo iliushangaza umma wa Kenya na wafuasi wa Nasa. Wamebaki njiapanda wasijue la kufanya. Nani anamsaliti nani?

Tangu Raila ‘ajiapishe’ kuwa rais wa wananchi Januari mwaka huu, uhusiano wake na viongozi wenzake ulianza kuning’inia. Hii ilileta wasiwasi mwingi kwamba huenda Kalonzo, Mudavadi na Wetangula ambao hawakuhudhuria wameamua kujiunga na mrengo wa Jubilee.

Tabia ya wanasiasa kutengana ama kuungana na mahasidi wao si jambo geni. Siasa ni mchezo wa karata na yule anayeucheza kwa umakini au ujanja ndiye anashinda.

Tangu zamani, siasa za Kenya zimesheheni usaliti na Raila anafahamu bayana kuwa kusalitiwa si jambo la ajabu ama linalotokea kwa ghafla. Kwanza, wale wanaopanga kuwasaliti wenzao hujitenga na mipango ya chama au muungano wao na kuanza kutoa sababu mbalimbali.

Kwa upande mmoja usaliti dhidi ya Raila ulianza wakati anaapishwa. Ghafla, wanasiasa waliokuwa naye tangu 2013 walianza kujitenga naye. Hatimaye, yeye aliapishwa pekee yake huku Kalonzo aliyekuwa anaimba kila mara kwamba angeapishwa naye, akitoweka na baadaye kutoa sababu kuwa hangeweza kufika kwenye sherehe ya kuapishwa kwa sababu alikuwa amepokonywa walinzi. Hata Raila alipokonywa walinzi wake mara baada ya kuapishwa.

Lakini, Kalonzo akaomba msamaha akiwahakikishia wafuasi wa Nasa kuwa yeye ataapishwa “hivi karibuni” lakini hadi sasa, hajafanya hivyo. Wafuasi wa Nasa hawamsikii tena akisema lolote kuhusu kuapishwa au mipango yake ya siku za usoni katika Nasa.

Uhusiano wa Mudavadi na Gideon Moi

Uhusiano kati ya familia ya Mudavadi na Gideon ulianza kitambo mno. Babake Mudavadi, Mzee Moses Mudavadi ndiye alimkaribisha Mzee Moi katika siasa. Moi na Mzee Mudavadi wameoa kwenye familia moja na uhusiano wao wa kisiasa na kifamilia ulidumu kwa miaka mingi. Uhusiano huo wa wazee sasa unaendelezwa na watoto wao, Musalia na Gideon. Wanasiasa hao walirithi viti vya baba zao. Mwaka 1989, Musalia alichaguliwa bila kupingwa kuwa mbunge wa Sabatia katika kaunti ya Vihiga baada ya babake kufariki dunia.

Mzee Moi alipostaafu 2002, kitinda mimba wake Gideon, alichaguliwa mbunge wa Baringo ya Kati ambalo babake alikuwa akiwakilisha bungeni tangu miaka ya 60.

Pengine ni kutokana na mkorogano huo baina ya viongozi wa Nasa, ndiyo kisa Raila akaamua kuwawahi, akakutana na Uhuru na kuweka makubaliano hayo.

Hata hivyo, katika kauli zake kabla hajakutana na Rais, Raila anasema safari ya Nasa si ya watu waoga; ni ya wajasiri. Anawataka wafuasi wake wajitayarishe kwa nyakati ngumu huku wakipanga mikakati ya makabiliano mapya na Jubilee.

Mapema, kiongozi huyu alijaribu kuwarudisha viongozi wenza wake kwenye jukwaa la Nasa lakini wengine wanatapatapa. Hata hivyo, Raila hakuwakashifu wala kuwatuhumu: Aliwapa muda lakini mambo hayakwenda alivyotarajia. Baadhi ya viongozi sasa wanalalamika kwamba njia ya kuelekea Kanaani imefungwa na wanataka kurudi Misri,” alisema bila kutaja majina.

Lengo lake la kupalilia demokrasia na kurejesha uchaguzi ulio wazi na wa haki liko palepale na anasema hakuna mabadiliko yoyote yamefanyika katika mchakato huu uliojaa hatari na mateke.

“Hatutarudi Misri,” Raila aliwaambia wafuasi wake hivi majuzi.

Kwa muda wa wiki mbili zilizopita, baadhi ya wanasiasa wa Nasa wamekuwa wakitoa wito kwa uongozi wa Nasa wauvunje muungano huo mara moja ili kutoa nafasi kwa kila mmoja wa viongozi wenza kuanza michakato yao ya kuwania urais 2022.

Chama cha ODM ambacho ni mojawapo ya vyama tanzu vya Nasa kilikuwa na kongamano lake wiki jana. Katika mkutano huo, Gavana wa Jimbo la Mombasa, Hassan Joho aliwasuta Kalonzo, Musalia na Wetangula kwa kukosa kufika Bustani ya Uhuru Januari 30 kushiriki kwenye kiapo cha Raila.

Muda mfupi baadaye, Wetangula akatangaza azimio lake la kuwania urais 2022 na kuwataka Raila, Kalonzo na Mudavadi wamuunge mkono.

Katika chama cha Wiper, wanasiasa wanamtaka Kalonzo aanze mchakato mpya wa siasa ikiwa viongozi wa ODM wataendelea kumtuhumu na kumkejeli kuhusiana na kukosa kwake katika hafla ya kuapishwa kwa Raila.

Seneta wa Kitui, Enock Wambua ni rafiki wa karibu wa Kalonzo na hakupoteza muda wakati mwanasiasa huyo alipomshambulia Kalonzo. Wambua alimrukia Joho kwa maneno akisema asitarajie Wakenya wafuate Nasa kama watu waliozibwa macho.

Matamshi ya Wambua na Wetangula bila shaka yatapanua mianya inayotisha kusambaratisha Nasa na kuimaliza. Nasa haiwezi kusimama bila vyama tanzu vya Kalonzo (Wiper), Mudavadi (ANC) na Wetangula (Ford-Kenya).

Ikiwa itasambaratika, Raila atalazimika kutumia chama chake cha ODM kufikia malengo yake yote ya kisiasa yakiwamo safari ya kuelekea Ikulu anakokuita Kanaani.

Itakuwa vigumu kwa Raila kuafikia malengo haya bila viongozi hao, lakini uzuri ni kwamba ana ufuasi mkubwa zaidi kuliko Kalonzo, Mudavadi na Wetangula kwa pamoja.

Lakini muda mfupi baada ya matamshi yake ya usaliti, Raila alisisitiza kwamba Nasa iko imara. Matamshi haya yalizua sintofahamu miongoni mwa wafuasi wake.

Raila analaumu chama tawala cha Jubilee na vyombo vya habari kwa kueneza propaganda dhidi ya Muungano wa Nasa.

Je, Jubilee itafaidika vipi ikiwa Nasa itakufa? Kwa hakika ina mengi. Kumbuka, katika siasa ufuasi wa wengi ndio mwenye nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi.

Umoja wa Nasa si kitu kizuri kwa Jubilee na ikisambaratika itakuwa vigumu kwa Raila kufikia malengo yake.

Jubilee huenda inalenga kuungana na Kalonzo, Mudavadi na Wetangula 2022 na kuwagawia mamlaka mbalimbali. Hali hii itamtenga Raila na kufifisha nafasi yake ya kushinda urais. Kwa sasa, macho yote yanaangazia Nasa; Je, itasambaratika au itakuwa na umoja zaidi.