In Summary
  • Hata hivyo, Brazil inabaki kuwa taifa linaloendelea kwa sababu za kimaisha na uzalishaji kwa kutazama mchango wa Wabrazil kwa mtu mmojammoja. Vinginevyo ingekuwa inatambuliwa kuwa moja ya mataifa makubwa yaliyoendelea.

Brazil inatajwa kushika nafasi ya nane duniani kwa kuwa na uchumi mkubwa. Ndilo taifa lenye uchumi imara kuliko mataifa yote ya Amerika Kusini na Latini Amerika.

Hata hivyo, Brazil inabaki kuwa taifa linaloendelea kwa sababu za kimaisha na uzalishaji kwa kutazama mchango wa Wabrazil kwa mtu mmojammoja. Vinginevyo ingekuwa inatambuliwa kuwa moja ya mataifa makubwa yaliyoendelea.

Idadi ya wananchi ni wengi sana, kwani ina wakazi zaidi ya milioni 200, hivyo kwa kutazama Pato la Ndani la Taifa (GDP), wastani wa kipato cha mtu kwa mwaka (GDP per capita), kiwango duni cha maisha ya mwananchi wa kawaida na vifo vya watoto wachanga, ni sababu pekee inayoibakiza Brazil katika kundi la nchi zinazoendelea.

Utaona kuwa Brazil ni taifa lenye uchumi mkubwa lakini kihuduma bado lipo chini. Walishughulikia kukuza uchumi wao na kufanikiwa, kwa hiyo sasa wanaweza kujikita katika kupanua ubora wa huduma. Ukishakuwa na uchumi mkubwa, maana yake una pato kubwa, huduma bora ni gawio linganifu kutokana na kipato.

Mafanikio ya Brazil yamepatikana ndani ya miaka 20. Mwaka 1992, Brazil ilitisha ulimwenguni kwa mfumuko wa bei. Mwaka 1994, aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Itamar Franco alimteua Fernando Henrique Cardoso “FHC” kuwa Waziri wa Fedha.

Chini ya urais wa Itamar, FHC alianzisha kampeni iliyoitwa ‘Mpango Halisi’. Kipindi hicho mfumuko wa bei ulipaa mpaka kufikia zaidi ya asilimia 1,110 mwaka 1992 kisha mwaka 1993 ukapaa kwa kasi hadi kufikia 2,400. Ila Plano Real iliumaliza na nchi ikawa salama bila mfumuko wa bei.

Mwaka 1995, FHC alichaguliwa kuwa Rais wa Brazil na kuzidi kuifanya nchi hiyo kuwa imara zaidi kiuchumi. Hii inaweza kukufanya ujenge hitimisho kuwa miaka 20 iliyopita, Brazil imeitumia kujenga uchumi.

Dosari uchumi wa Brazil

Kwa kipimo cha Pato la Taifa kwa kuangalia thamani ya soko, Brazil ni nchi ya nane duniani kwa kuwa na pato kubwa lakini kwenye mchango wa nchi kwa kichwa, inashika nafasi ya 62.

GDP ya Brazil kwa kuikokotoa kupitia uimara wa sarafu yake katika manunuzi dhidi ya Dola ya Marekani, Brazil inaendelea kushika nafasi ya nane, lakini ukiipeleka kwenye GDP per capita inashika nafasi ya 76.

Tafsiri hapo ni kuwa Brazil kwa mipango yake ya kiuchumi, haikui pamoja na wananchi wake. Inaweza kutamba kuwa ni taifa lenye uchumi mkubwa kati ya mataifa nane yenye kuongoza ulimwenguni lakini kiuhalisia mwananchi wake anapata shida kuishi.

Ukisoma maudhui ya Mkakati wa Maendeleo ya Taifa kwa Qatar mwaka 2011-2016, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Maono ya Taifa la Qatar kuelekea mwaka 2030, unapata msingi kwamba uchumi wa wananchi ni ule ambao unaratibiwa kwa sera inayothamini mchango wa kila mwananchi.

Serikali inapobeba dhamana ya kuendesha nchi lazima ijipe wajibu wa kuratibu maisha ya watu, na ihakikishe kwamba kipindi taifa linapiga hatua kwa maendeleo ya kiuchumi, hakuna mwananchi anayebaki nyuma.

Umuhimu wa sensa siyo kujua tu idadi ya watu na kutangaza kama mapambo, bali Serikali inatakiwa ijue idadi ya watu wake kisha iweke mipango ya kuwahudumia kijamii, vilevile kuwatumia kama chanzo kikuu cha uzalishaji ili nchi isonge mbele.

Uchumi wa Brazil unatoa tafsiri kuwa taifa hilo limejielekeza kujikuza kwa sababu ya utajiri wa rasilimali bila kuzingatia idadi ya watu wake. Matokeo ya juu ni kushuhudia vifo vingi vya watoto , wakati viongozi wa nchi hiyo wanaketi kwenye mikutano ya mataifa makubwa yenye uchumi mkubwa.

Qatar ni nchi ya 47 kwa GDP lakini inashika nafasi ya 6 kwa GDP per capita kwa mujibu wa Benki ya Dunia. Hoja inaweza kutoka kuwa nchi hiyo ina idadi ndogo ya watu, vilevile utajiri wake wa mafuta ni mkubwa. Hata hivyo, msingi wa kuiheshimu nchi hiyo ni namna ilivyojiwekea mkakati wa kuhakikisha kila mwananchi anazalisha.

Ni kupitia mkakati huo wa Qatar, ndiyo maana jamii ya watu wasiojiweza, mayatima, wazee na wajane, wanafikiwa kwa urahisi na kupata huduma muhimu za kijamii. Kila mwananchi kwa maisha yake, anajiona anafanana na pato la taifa.

Kuzalisha ni uwekezaji

Kufikia kiwango cha wananchi kuzalisha na kupata kadirio bora la GDP per capita lenye kufanana na hali halisi, lazima kuwepo na uwekezaji mzuri, ambao unatekelezwa chini ya sera na mipango kama Qatar.

Nchi inajiwekea utaratibu wa kumfikia kila raia kupitia mamlaka zake, inamwezesha kimazingira na hata kimtaji ili aweze kuzalisha. Ni kupitia mpango huo ndipo inakuwa rahisi kuyaona matokeo ya kiuchumi kuanzia serikalini mpaka kwa wananchi katika wingi wao.

Wastani wa GDP per capita umekuwa ukipishana na hali halisi, kwa sababu GDP inakuwa na mchango wa watu wachache mno kwa kuwa wengi hawazalishi, lakini kwa vile kila mwananchi anahesabika, pato la taifa linagawiwa kwa kila kichwa na kupata takwimu.

Mathalan, ripoti ya Benki ya Dunia mwaka jana, iliontesha kuwa GDP per capita duniani ni dola 15,800, sawa na Sh35.6 milioni kwa mwaka. Katika hesabu hiyo ujue kuwa kuna Luxembourg yenye dola 102,831 (Sh231.8 milioni) na Tanzania ambayo per capita yake ni Sh1.9 milioni.

Hesabu hiyo inakupa kadirio kwamba kila mwananchi wa Luxembourg anachangia pato la taifa kila mwezi Sh19.3 milioni, wakati Mtanzania ni Sh158,000. Takwimu za mataifa hayo mawili, ikiwemo mengine ambayo kipato cha mtu mmoja ni kikubwa kama Qatar, Kuwait, Uswis, Ireland, Norway, zinakutanisha na kupata hesabu kuwa duniani, per capita ni Sh35.6 milioni kwa mwaka.

Kwa ukokotoaji huo, unapata majibu kwamba mchango wa mwananchi wa Luxembourg katika pato la dunia ni Sh231.8 milioni, wakati Mtanzania yeye ni Sh1.9 milioni, kisha per capita ya kidunia inakuwa Sh35.6 milioni

Mtiririko huo ndiyo ambao unakuwezesha kuichambua per capita ya Mtanzania Sh1.9 kwa mwaka au Sh158,000 kwa mwezi. Watanzania wapo jumla ya watu 51 milioni. Ndani ya Tanzania kuna matajiri wakubwa kama akina Reginald Mengi, Mohamed Dewji, Ally Mufuruki, Said Bakhresa, vilevile wapo ombaomba ambao hawazalishi.

Hivyo basi, kama ambavyo Watanzania walivyo na kipato kidogo katika wastani wa kipato cha mto kidunia na mataifa yenye ustawi mzuri kuathirika, ndivyo na akina Mo Dewji na Bakhresa wanavyoathiriwa na idadi kubwa ya wasiozalisha mpaka inaonekana kila Mtanzania ana kipato cha Sh1.9 milioni kwa mwaka.

Tatizo kuu

Julai 11 kila mwaka ni maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani. Inakadiriwa kwamba watu wamefikia bilioni 7.6. Wakati ongezeko la watu ni kubwa, upande wa pili shughuli za kiuchumi hazipanuki. Hapa ndipo kwenye tatizo kubwa.

Mwaka 2014, vyombo vya habari Marekani viliripoti kuwa asilimia moja ya matajiri wakuu nchini humo, wanamiliki asilimia 40 ya utajiri wote, na kwamba asilimia 80 ya Wamarekani wanamiliki utajiri asilimia 7 tu. Kwa maana hiyo, asilimia 19 ambao ni matajiri mno nyuma ya ile asilimia moja, wanamiliki utajiri asilimia 53.

Mwandishi wa masuala ya uchumi na fedha nchini Marekani, Robert Kiyosaki anayo kanuni yake ya kifedha kwamba asilimia 10 ya watu humiliki utajiri wa asilimia 90 kwenye kila nchi, wakati asilimia 90 ya watu hukimbizana kugawana asilimia 10 tu ya utajiri.

Uchambuzi zaidi kuhusu kanuni hiyo ni kuwa hata katika nchi, maendeleo yake kwa asilimia 80 hutokana na jitihada asilimia 20 za watu wake. Mwongozo huo unaleta mantiki kwamba laiti kila nchi watu wake watawekeza jitihada kwa asilimia 50 tu, maendeleo yatakuwa makubwa na dunia itastawi.

Kwa mantiki hiyo, ukuaji uchumi duniani nchi kwa nchi na jinsi ambavyo imekuwa ikitazamwa, ni dhahiri vipimo vimekaa kisiasa. Nchi inapambwa kwa ustawi wa kiuchumi lakini watu wake wapo hoi. Ustawi wa watu kinapaswa kuwa kigezo kikuu.

Hata sasa Tanzania, kelele ni nyingi. Serikali inajinasibu kuwa uchumi unakua, wapinzani wanakosoa. Binafsi nashawishika kukubaliana na Serikali, lakini swali ni moja; ikiwa vilio mitaani ni vingi kwamba hali za kimaisha ni ngumu, huo uchumi ni upi usioakisi ustawi wa maisha ya watu wake.

Biashara nyingi zimefungwa kati ya mwaka jana mpaka sasa, hoteli nyingi zimeondoka sokoni, maduka madogo na makubwa yamepigwa kufuli. Hiyo ni kuonyesha kuwa idadi ya Watanzania wanaozalisha inapingua na mzunguko wa fedha unapata athari.

Kumbe sasa, tukiacha kuridhika na vipimo vya mazoea, kwamba awamu ya nne makusanyo yalikuwa kadhaa na sasa yameongezeka na kutumia kanuni ya uchumi shirikishi, kwamba GDP ya sasa hailingani na idadi ya watu, ndipo itakuwa rahisi kubaini kuwa mambo bado na kazi zaidi lazima ifanyike ili kuupata uchumi wa wananchi.