In Summary

Kuongezeka kwa watu si changamoto bali kasi kubwa ya ongezekohilo. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Tanzania ina wastani wa ongezeko la watu wa asilimia 2.7 kwa mwaka ulinganisha na sensa ya mwaka 2002 ulipokuwa asilimia 2.9.

        Ripoti ya Benki ya Dunia (WB) mwaka 2008 inataja nchi masikini kuwa na ongezeko la watu kwa wastani wa asilimia 2.2 kwa mwaka, asilimia 1.3 kwa nchi zenye kipato cha kati na asilimia 0.7 kwa nchi zilizoendelea.

Kuongezeka kwa watu si changamoto bali kasi kubwa ya ongezekohilo. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Tanzania ina wastani wa ongezeko la watu wa asilimia 2.7 kwa mwaka ulinganisha na sensa ya mwaka 2002 ulipokuwa asilimia 2.9.

Kwa tafasiri ya haraka, Tanzania imepunguza kasi ya ongezeko la watu kwa asilimia 0.2 ndani ya miaka 10 hiyo kuanzia mwaka 2002 hadi 2012. Ukiachilia mbali vigezo vingine, itaichukua Tanzania miaka 70, mpaka mwaka 2082 kufikia uchumi wa kati kama jitihada za haraka hazitafanyika kunusuru kasi kubwa ya ongezeko la watu.

Kasi ya ongezeko la watu si kiashiria kizuri kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Hii inatokana na ukweli kuwa kasi hiyo inapokuwa kubwa kuliko ya kukua kwa huduma za kijamii na kiuchumi, nchi huendelea kuwa masikini na tegemezi.

Sensa ya kwanza nchini, baada ya uhuru, iliyofanyika mwaka 1967 ilionyesha kulikuwa na watu milioni 12.3. Makadirio ya idadi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2017 ni yanaonyesha ni milioni 51.6, hii ina maana kuna ongezeko la watu milioni 39.3 ndani ya miaka 50 iliyopita.

Tafsiri ya ongezeko ni kuwa, Serikali itaendelea kutumia sehemu kubwa ya rasilimali zake kuhudumia wananchi kwa kuelekeza kiasi kikubwa kwenye sekta za elimu, afya, maji, umeme, miundombinu ya usafiri na usafirishaji, na utawala.

Hii ni muhimu kwa sababu kila mwananchi anahitaji matibabu anapohisi mabadiliko ya mwili. Watoto wote wana haki ya kupata elimu kuanzia ngazi ya chini mpaka elimu ya juu.

Hali kama hiyo pia inajidhihirisha kwenye mahitaji ya maji kw amatyumizi ya nyumbani, uzalishaji viwandani, kilimo na ufugaji hata uvuvi. Chochote kinachofanyika kinahitaji maji hivyo Serikali kutokuwa na mbadala zaidi ya kuhakikisha inaongeza uzalishaji na usambaji wa maji kwa wananchi wote, mjini na vijijini.

Nitoe mfano rahisi, wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne na darasa la saba mwaka 2017 ni wachache ukilinganisha na wanaojiunga na darasa la kwanza na kidato cha kwanza mwaka 2018. Hii inamaanisha kila mwaka, Serikali na wadau wa maendeleo wataendelea kujenga vyumba vya madarasa, ununuzi au utengenezaji wa madawati, ujenzi wa matundu ya vyoo na miundombinu mingine.

Badala ya kuelekeza rasilimali hizo katika maeneo mengine ikiwemo kuimarisha miundombinu ya uchumi, fedha nyingi huishia katika huduma za kijamii ambazo Serikali hutoa bila malipo au kwa gharama nafuu sana.

Hamasa imeongezeka baada ya elimu kuanza kutolewa bila malipo. Uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza umeogezeka hata kuzidi matarajio. Matumizi ya wizara husika pamoja na wadau wake yameongezeka.

Pamoja na ongezeko kubwa la watu, eneo la ardhi limeendelea kuwa lilelile; kilometa za mraba 945,000 kati hizo kilomita 883,000 ni ardhi kavu. Idadi ya watu kwa kila kilometa moja ya mraba ilikuwa 14 mwaka 1967 lakini mwaka 2017 wamefika 57.

Maana yake msongamano wa watu umeongezeka ukwenye kipande kidogo cha ardhi. Wakulima wanahitaji eneo la kulima kama ilivyo eneo la kufugia na huduma za kijamii na kiuchumi.

Tanzania ina idadi kubwa ya watoto kuliko watu wazima, asilimia 50.1 ya wakazi wa Tanzania ni watoto chini ya miaka 18 wakati wazee ni asilimia 9.5. Takwimu zinaonyesha, yatima wenye kati ya miaka sifuri na 17 ni asilimia 7.7 na walemavu ni asilimia 6.03.

Idadi ya watu katika makundi haya inatengeneza asilimia 73.33 ya wakazi wote wa Tanzania ambao ndiyo nguvukazi, kwa mujibu wa sensa mwaka 2012.

Kwa tafsiri ya kawaida, watoto, walemavu, yatima na wazee ni makundi yanayohitaji kusaidiwa zaidi, ni makundi tegemezi. Makundi haya yanategemea asilimia 26.67 ya watu kuwahudumia. Wakati huohuo waliojiunga katika mifuko ya hifadhi ya jamii ni asilimia 11.3 kwa takwimu za mwaka 2012.

Ni vyema Serikali ikaamua kwa dhati kutoa elimu ya uzazi wa mpango ili kuhakikisha rasilimali tulizonazo zinatumika kuhudumia idadi ya watu inayostahimilika kuliko ilivyo sasa na inavyotegemewa kuwa.

Kama Serikali na jamii tutaruhusu ongezeko hili la watu kila mwaka, kutaendelea kupambana na maradhi, ujinga na umasikini kwa kipindi kirefu kijacho.

Kukuza uchumi wetu kwa ndoto tulizojiwekea tunahitaji kubadili mpango. Idadi ya watu idhibitiwe na waliopo wapewe huduma zinazostahili.

Elimu iimarishwe ili kuongeza uzalishaji wa kila mmoja. Miundombinu ya usafiri na usafirishaji, nishati na mazingira rafiki ya kuanzisha na kufanya biashara yawekwe.

Mwandishi na Mtakwimu na Ofisa Mipango.