In Summary
  • Wateja hawa tunaowauzia au wanaonunua bidhaa zetu tunawaita wateja wa nje. Wapo wa ndani pia. Wateja wa ndani ni wafanyakazi wa kampuni husika. Wateja hawa pia wanatakiwa kujaliwa kama ilivyokwa wale wa nje ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyowekwa ikiwamo kuwajali wateja wa nje.

        Mara nyingi linapozungumzwa suala la kumjali mteja, fikra za wengi hujielekeza moja kwa moja kwa wateja ambao wananunua bidhaa au huduma za biashara zao.

Wateja hawa tunaowauzia au wanaonunua bidhaa zetu tunawaita wateja wa nje. Wapo wa ndani pia. Wateja wa ndani ni wafanyakazi wa kampuni husika. Wateja hawa pia wanatakiwa kujaliwa kama ilivyokwa wale wa nje ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyowekwa ikiwamo kuwajali wateja wa nje.

Wateja wa ndani ambao ni wafanya kazi mara nyingi husahaulika. Menejimenti nyingi hujisahau na kuelekeza nguvu kubwa kuwahudumiwa wale wa nje bila kujali kwa kufanya hivyo hupunguza ubora wa huduma au bidhaa kwa wateja wa nje pia kwakuwa hutolewa na hawa ambao hawatoshelezwi.

Ipo imani miongoni mwa wafugaji kwamba ukilimsha ng’ombe vizuri basi tarajia kupata maziwa mengi. Vivyo hivyo kwa mteja. Kuna namna nyingi za kumjali mfanyakazi ambaye ni mteja wa ndani ili afanye kazi kwa ufanisi.

Kuweka wazi kazi na wajibu wa kila mfanyakazi ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuongeza ufanisi wa kampuni. Kila mtu anatakiwa kujua anafanya nini na kwa wakati gani na anaripoti kwa nani ili kuepuka mkanganyiko na sintomfahamu miongoni mwa wafanyakazi.

Kazi na wajibu zikieleweka vyema, kila mmoja atatekeleza majukumu yake kwa wakati hivyo kuwa kwenye nafasi nzuri ya kumjali mteja wa nje. Wafanyakazi wanapaswa kuelewa kuwa ili kazi zifanyike vizuri na kwa wakati, wote wanategemeana.

Wafanyakazi wanahitaji mafunzo au semina ili kupata uzoefu na kuongeza ujuzi. Mafunzo huwafanya wawe maahiri katika utendaji wa kazi zao za kila siku. Mafunzo yanasaidia kujenga uwezo wa ziada kiutendaji kwa wafanyakazi ambao huchangia kuongeza uzalishaji na kuboresha huduma.

Kila mjasiriamali au menejimenti ya kampuni inahitaji kujitathmini, ni mara ngapi imewapa mafunzo wafanyakazi wake ili kuwaongezea ujuzi wa masuala tofauti kwa lengo la kuboresha utendaji wao. Wafanyakazi wakionyeshwa kujaliwa nao huijali biashara pamoja na wateja wanaowahudumia.

Wakijengewa mazingira mazuri ya kazi bila mashaka watawajibika kwa ufanisi mkubwa na kwa uhakika. Mazingira ya kazi yakiwa mazuri watawafanya wateja wa nje kuwa wa kwao kutokana na huduma nzuri watakazozipata.

Wakifikia hatua ya kuwafanya wateja wa nje wajione wapo nyumbani, hiyo ni hatua kubwa na utendaji kazi wao utakuwa wa ufanisi na wa kuleta maendeleo. Mazingira ya kazi yatawafanya wajitume, wabuni na watafute suluhisho la tatizo endapo linatokea.

Ni muhimu kupima namna wafanyakazi wanavyoridhishwa na mahali pa kazi kwa kuangalia mambo mengi ikiwamo wanavyouchukulia uongozi, mawasiliano, umoja wao na mazingira ya kazi kwa ujumla.

Baada ya kupima hivyo vyote yatapatikana majibu ambayo uongozi unatakiwa kuyafanyia kazi kama njia mojawapo ya kuwajali wafanyakazi na kuboresha kazi kwa masilahi ya kampuni kwa ujumla.

Inashauriwa, unapofanya biashara na una wafanyakazi kadhaa wanaosaidia kufanikisha huduma zako, ni muhimu na lazima kuwajali kwa njia mbalimbali ili wakuletee mafanikio yanayotarajiwa kwa ufanisi mkubwa vinginevyo utapata hasara.

Kwa kutambua ubora wa huduma zako unawategemea wafanyakazi, basi hakuna namna nyingine ya kufanikisha hilo zaidi ya kuweka mazingira rafiki kwao kufurahia kazi wanazozifanya kila wanapoingia na kutoa kazini.

Wafanyakazi hukutana na wateja wa biashara hata nje ya kazi ambako wanaweza kubadilishana uzoefu wa masuala tofauti. Endapo hawatokuwa na furaha ni rahisi kwao kutoa siri za kampuni na kuiangusha hali ambayo haiwezi kutokea endapo wataridhika.