In Summary

Unajua, katika kujipendekeza, unaweza kuwa Mkristo kuliko Wakristo wenyewe, wanaharakati kuliko wanaharakati wenyewe. 

Hii misosi ya sikukuu Bwana, shida sana.  Yaani jana niliota ndoto ya ajabu sana, sijui ni kwa sababu ya shibe. Ndiyo! Shibe! Atakayesema ni kutokana na Konyagi nitamshtaki kwa uchochezi. 

Basi nilikuwa kijijini kwenye mashindano ya ngoma. Watu waliruka na kucheza ngoma ya kila aina. Ngoma nyingi zilikuwa zinaendeleza na kutukuza na kuboresha ngoma zetu za asili lakini mwaka huu hata watazamaji walikuwa wengi zaidi kutokana na tetesi ya kuzuka kwa ngoma mpya ya aina yake. Watu wote walikuwa na hamu sana kuona ngoma hii mpya.

Baada ya muda, tukasikia midundo kutoka mbali.  Midundo ambayo ilinyamazisha midundo yote iliyotangulia. Wengine walipiga ngoma kuuuubwa kama zile za kumtukuza mfalme wa Burundi.  Zilivyopigwa DUH DUH DUH, ardhi yote ilitingishika na hata nyumba na karibu zilidondoka chini kutokana na nguvu ya ile midundo. Hizi ngoma kubwa zilisindikizwa na ngoma nyingi ndogondogo. 

Tulipoanza kuzoea ili midundo ambayo kwa kweli ilifanya hata midundo yetu ya moyo kubadilika, wakaingia wachezaji. Tulishangaa kidogo maana hakukua na wimbo kabisa. Badala yake wachezaji walikuwa wanapaza sauti NGOMA ... TU ... NGOMA ... TU kulingana na kila mdundo mzito. 

Akaingia kiongozi wa ngoma. Akacheza kwa nguvu hadi sisi watazamaji wote tulishangilia kwa vigelegele na vihelehele. Alizungukazunguka kwa kasi sana na kila aliposimama mbele ya mtu, yule mtu akaanza kutoa povu na kuanguka chini.  Kumbe ngoma ile ilikuwa na madhumuni mengine ya kutoa wachawi pia. Basi kila wachawi walivyokuwa wanaanguka, wachezaji wa ngoma ile wakazidi kucheza hadi walikuwa wanarukaruka kwa namna ambayo haijawahi kuonekana.  Nakwambia, waliruka kuliko hata kiongozi wao. Wakaruka hadi wakapoteza uwiano na midundo kabisa. Watu waliwazomea lakini hawakujali ili mradi wanafanya juu chini kumfuata kiongozi wao. 

Na katika kumfuata, nao wakaanza kuzungukazunguka lakini, tofauti na kiongozi ambaye alisimama tu mbele ya wachawi wenyewe, wao walianza kuwapiga watu kichwani hadi walipoanguka wakidai kwamba ni wachawi.  Na kila walipoanguka hawa ‘wachawi’ wa kupigwa kichwani, waliruka juu na kujiviringishaviringisha kwa namna ya ajabu. Yaani ni kama kila mmoja alitaka kumwonesha kiongozi wao kwamba wao ndio zaidi, hakuna mchezaji kama wao katika ngoma ya bosi wao. 

Lakini wale waliopigwa vichwa, na hata wengine walioanguka wenyewe, walianza kuliliwa na umati wa waliokuwa pale.

‘Huyu si mchawi. Huyu si mchawi. Acheni kuwasingizia watu’

Lakini wale watu hawakujali. Wakakusanyika katikati na kunyamazisha ngoma. Kisha wakasema kwa sauti ya kutisha.

‘Anayemlilia mchawi ni mchawi

Anayemtetea mchawi ni mchawi’

Mara baada ya kutangaza hivi, wakajitokeza wachezaji wengine wa ngoma. Hawa walitisha kuliko wote maana walikuwa wamevaa nguo maalumu, wakibeba mkuki na ngao ili kuonyesha kwamba wao ni walinzi wa kiongozi. Hawakuwa na huruma aisee. Waliliaji walivutwa hadi ndani na kupigwa hadi chini huku wachezaji wakiwazunguka na kuwabeza na kuwatukana na hata kuwakanyaga. Hali ilitisha kabisa, na bado wachezaji walizidi kufanya kila wawezalo kumvutia kiongozi awaone wao. Walizidi kuruka, walizidi kupaza sauti.

NGOMA ... TU

NGOMA ... TU

Kuona hivi, wachezaji wa ngoma nyingine walionekana kuchanganyikiwa hadi wengine waliamua kujiunga na wachezaji wa hii ngoma mpya. Wenzao walipotaka kulalamika wao nao wakavutwa na wenye mkuki na ngao huku wachezaji wenyeji na wachezaji wahamiaji wakishindana kwa nguvu kabisa nani anaweza kuruka zaidi, nani anaweza kujiviringisha zaidi hadi wote walikuwa wanataka kukosea.

Mwisho walitaka hata kupigana, huku wenyeji wakidai wahamiaji wanapendelewa. Wakati huu manju alikuwa amesimama pembeni akiwaangalia wachezaji wake wa zamani na wapya. 

Unajua, katika kujipendekeza, unaweza kuwa Mkristo kuliko Wakristo wenyewe, wanaharakati kuliko wanaharakati wenyewe, mtiifu kuliko watiifu wenyewe ili mradi uonekane katika kujipendekeza kwako. Na ndivyo ilivyokuwa.  Badala ya kurukaruka mbele ya kiongozi bila kuona ishara kutoka kwake, na wakati wengine wameamua kuondoka wasije wakavutwa na kukanyagwa bila sababu, wachezaji wakaamua kwamba itabidi kujionyesha kwa namna tofauti.  Basi wacha wazunguke na kuwapiga hata wasichana waliokuwa wanawaangalia.  

Nilishangaa na kuwauliza walio pembeni mwangu kulikoni lakini kumbe wote walikuwa wametimua mbio mbele ya wenye mikuki na ngao. Duh!  Nilipiga moyo konde na kumuuliza mchezaji.

‘Hawa wasichana wamekosea nini?’

‘Wewe ni nani kuuliza? Hujui wimbo wetu.

Kupata mimba shuleni

Ni sawa na uhaini

Tunawalaza ndani

Wahalifu namba wani’

Nilitaka kuuliza kwani walifanya peke yao lakini nikakuta nashushiwa dhoruba ya makofi na mateke.  Nikapaza sauti.

‘Jamani naumiaaaaaaa’

Nikashtuka kumbe ni mke wangu ananipigia makofi ya mahaba.

‘Jamani mume wangu, tangu lini kofi ya mahaba iumize. Ulikuwa unapiga kelele utadhani mbuzi wa kafara.’

‘Lo samahani mke wangu, niliota ndoto ya ajabu sana ndiyo maana nilikuwa napiga kelele. Na wewe vipi? Mbona bado uko macho?

‘Najibizana na wenzangu kuhusu hii stori ya wasichana kutiwa ndani kwa kuwa wamebeba mimba. Kwanza wamebeba mzigo waliopachikiwa na mtu mwingine, mbona huyu mwingine haguswi? Na pili tangu lini kupewa mimba iwe ni kosa la jinai?  Nilivyojua mimi, kisheria, anayetembea na msichana wa shule ndiye mwenye kosa, msichana bado mto ... we mume wangu unafanya nini?’

Mke wangu alishangaa kuona nimemrukia na kujaribu kumfunika na mito.

‘Acha Bwana unafanya nini?’

‘Hujui mke wangu, hujui. Wako wenye mikuki na ngao, watakuja kukukamata.’

‘Unasema nini?  Nani mwenye mkuki na mgao?’

‘Huwaoni? Huwaoni? Na hawa wachezaji ngoma ya kujipendekeza?’

‘Wewe mume wangu umepata kichaa nini? Wako wapi watu wote hao? Hebu acha!’

Alivyopiga kelele ilibidi niangalie niko wapi.  Kumbe siko ngomani, niko sebuleni. Kumbe nilikuwa ninaota ... au?

Amka na kukuta matamko.