In Summary
  • Mbinu za kisayansi namna hii zinatumiwa na wanaume wa kweli.

Juzi tulikuwa kituo cha polisi, tulikwenda kumtoa jamaa yetu Samweli. Alikuwa amewekwa ndani na mke wake tangu Alhamisi mchana, akatoka Ijumaa baada ya sisi kwenda kumsaidia kuweka mambo sawa pamoja na kuzungumza na mke wake, kumshawishi amkunjulie moyo mwandani wake ili aachiwe.

Binafsi nilivyopewa taarifa kwamba eti Samweli amewekwa ndani na mke wake nilishindwa kuamini haraka; na nilipothibitisha kuwa ni kweli swali lilikojua kichwani ilikuwa ni tatizo gani liliowafikisha huko. Katika kuuliza uliza nikaambiwa eti jamaa yetu alimpiga mke wake sana tu, mke akapata wapambe, wakamjaza, akashawishika kumuweka mumewe ndani jambo ambalo kisheria alikuwa sawa kabisa.

Tulipofanikiwa kumtoa Samweli ndiyo tukakaa naye chini kuzungumza kiume tujue imekuwaje hadi kufikia hatua ya kumbonda namna ile mwanamke aliyemuoa kwa mahaba binafsi, akamlipia na mahali kabisa bila kulazimishwa, imekuwaje?

Ndiyo tukagundua kuwa kumbe chanzo ilikuwa ni kaugomvi kadogo tu ila mke wake ndiye aliyekakuza, alikuwa akichonga mdomo sana tena kwa sauti, jamaa yetu akashindwa kumvumilia akamtia mikononi na kuanza kumshushia makonde.

Lakini si unajua kawaida ya anayesimulia peke yake ni lazima awe mwanga ngoma, huvutia kule alipo; basi ndiyo alivyokuwa Samweli. Kila alichokuwa anatuambia alikuwa anajitahidi kutuaminisha kuwa mke wake ndiye alikuwa mkosefu.

Binafsi nilichogundua ni kwamba mke wa Samweli hakuwa akizungumza peke yake, alikuwa akijibizana na mumewe, na laiti kama Samweli angeamua kuwa mwanaume wa kweli wasingefikia mbali namna ile kwa sababu wanaume wa kweli hawajibizani na wake zao.

Unajua wanawake wameumbwa kujibizana, na raha ya kujibizana upate wa kujibizana naye kwa hiyo anapoengea, na wewe ukamjibu, unampa raha na kila sababu ya kuendelea kuongea.

Dawa za mwanamke anayependa majibizano ni mbili tu, ya kwanza ni kuondoka kabisa nyumbani ukiona anaanzisha majibizano, tafuta kwa kukaa, rudi jioni; utakuta ameshafunga mdomo wake.

Ya pili ni njia ya kisayansi zaidi, hii inahusisha unywaji wa maji safi na salama. Unachotakiwa kufanya ni kuchukua ‘glass’ ya maji na kunywa pindi tu mwanamke anapoanza ‘tantarira’, lakini hakikisha huyamezi maji hayo, badala yake yasukutue. Hakikisha unasukutua hadi anapomaliza kuongea, tangu hapo unaweza kuyameza na ikiwezekana muongeleshe kuhusu luku, bili ya maji au ada ya shule watoto, mada ambazo zinamkumbusha kuwa wewe ndiye mwanaume, na ndiye unayeweza mambo yote hayo.

Sayansi iliyopo kwenye hii njia ya pili ni kwamba unapokuwa na maji mdomoni maana yake huwezi kuzungumza, na kama huwezi kuzungumza maana yake huwezi kumjibu, na kutokumjibu ni sawa na kumuondolea ile raha ya majibizano kwa kuwa atakuwa anaongea mwenyewe, atajiona kama chizi hivi, basi lazima ataamua kunyamaza tu.

Mbinu za kisayansi namna hii zinatumiwa na wanaume wa kweli.