In Summary

Maarifa hayo mara nyingi hutegemewa yawe na manufaa kwa mwanafunzi na jamii inayowazunguka.

Mwalimu ni mtu aliyepata ujuzi kupitia mfumo rasmi au usio rasmi, mwenye uwezo wa kumfundisha mwanafunzi maarifa au ujuzi.

Maarifa hayo mara nyingi hutegemewa yawe na manufaa kwa mwanafunzi na jamii inayowazunguka.

Katika kitabu cha Uhuru wa Wanawake kilichoandikwa na Mwalimu Julius  Nyerere, anaeleza kuwa:

“Wazungu ambao walifikiri kuwa Waafrika ni nusu watu sasa wameanza kuamini kuwa Waafrika ni watu kwa sababu katika mieleka ya mambo ya akili imeonyesha kuwa Mzungu anaweza kuangushwa na Mwafrika na Mwafrika anaweza kuangushwa na Mzungu.”

Nyerere alieleza hayo huku akikumbusha msingi wa maarifa kwamba katika masuala yanayohusu akili, binadamu wote wamejaaliwa tunu hiyo.

Tofauti hutokea pale  kila mmoja  kwa namna yake anavyotumia akili yake. Tukumbuke msemo: “akili ni nywele kila mtu ana zake”.

Mwalimu bora huambatana na sifa kadhaa  kama vile kupenda na kuithamini kazi yake, huku akiwa hayuko tayari kujiona duni wakati wote. Huyu ni mwalimu aliyejitambua kuwa ni mwalimu; ni lazima ataambukiza mambo mazuri kwa wanaomzunguka.

Katika hili mwalimu huweza kubadilishwa yeye binafsi kutokana na aina ya masomo anayofundisha. Kwa sababu watu huwa hivyo walivyo kutokana na namna wanavyofikiri, wanavyotenda na wanayozungumza. Kwa mfano, mtu akiendekeza upuuzi kila wakati huwa mpuuzi.

Pili, anayependa kujifunza mara zote. Mwalimu bora hufanya marudio, hujitafakarisha juu ya somo, maisha, uhusiano, maendeleo na masuala mengine katika nyanja mbalimbali ambazo humpatia uwezo mkubwa wa kuendelea kuwa mshauri katika jamii yake.

Kwa mfano, mwalimu anapotekeleza majukumu yake shuleni, huvaa kofia za kada mbalimbali kama vile  usuluhishi na kutoa adhabu (uhakimu na uanasheria), uuguzi pale mwanafunzi anapopata tatizo la afya akiwa shuleni

Pia, hutoa  ushauri wa masomo, tabia na usanii pale anapohamasisha utambuzi,  ukuzaji vipawa na vipaji mbalimbali vya wanafunzi wake.

Tatu, anayefahamu kuwa kujifunza ni tendo endelevu kwa maisha yote ya binadamu.

Mwalimu bora hufahamu vyanzo vipya vya maarifa katika fani yake au masomo anayofundisha na wakati mwingine hata asiyofundisha. 

Kwa kufanya hivyo, atakuwa na uwezo mkubwa wa kupewa changamoto na kuzitatua na kufaidika na mawazo kutoka kwa watu mbalimbali kupitia vitabu au kwa njia ya majadiliano na si mabishano.

Hii ni kwa sababu mwalimu bora hutambua kuwa mabishano yaliyo mengi huwa si chanzo cha maarifa na huendeleza ujinga badala ya hekima.

Nne, anayechukua hatua na  kutekeleza kwa vitendo yale anayojifunza. Mwalimu bora anapojifunza huchukua hatua za kutekeleza kwa vitendo ujuzi mpya alioupata kwa wanafunzi wake, jamii inayomzunguka na kwa maisha yake ya kila siku.

Kwa mfano, anapofahamu matumizi ya vifaa vya Tehama ni dhahiri huweza kutumia katika kurahisisha shughuli za ujifunzaji na ufundishaji na katika kukusanya, kuandaa na kuchakata taarifa mbalimbali shuleni na katika shughuli za maisha za kila siku.

Katika hili ni dhahiri mtu akimtazama mwalimu bora, atamuona mtu apendaye kuwa rafiki wa jamii, mtu afurahiaye kufanya shughuli kwa ushirikiano kama ilivyo kwa kada za wauguzi, wanasaikolojia, washauri na viongozi wa dini.

Tano, anayethubutu kukiri kuwa hafahamu au hajui ili aweze kufahamishwa. Mwalimu bora hupenda ukweli, huuishi ukweli na huwa na mawazo au akili yenye kujihoji katika masuala mbalimbali.

Kwa kuwa ni mwanafunzi wa kudumu kila siku hutamani kuwa sehemu ya suluhisho badala ya kuwa upande wa tatizo. Hii ni kwa  sababu hufahamu kuwa nguvu ya kuuliza hushinda nguvu ya ujinga.

Kwa kuuliza pale asipofahamu, mwalimu hujikuta akiwa na kiwango kikubwa cha kujiamini na kukuza upeo wake wa kuelewa mambo tofauti. Uwezo huo humsaidia kufikiri kwa kina, kufikiri kwa umakini na kwa usahihi. 

Sita, anayekubali kuomba radhi pale anapokosea kwani naye ni binadamu. Na kuomba radhi ni kitendo cha kiungwana na wala si cha kinyonge.

Mwalimu bora hufahamu namna ya kushughulika na hisia na udhaifu wake wa kibinadamu ili kupunguza au kuondoa upendeleo, ubaguzi na upuuzaji.

 Katika hili huwa na uwezo wa kumhudumia mtu yeyote pasipo kujali historia yake ya nyuma, rangi, jinsi, kabila, hali ya uwezo wa kiuchumi kama vile ambavyo yeye angependa kufanyiwa.

Saba, anayependa kufanya mambo sahihi kwa kiwango cha juu lakini kwa kutumia njia nyepesi.

Mwalimu bora huwa na uwezo wa kurahisisha mambo kwa ubora uleule tarajiwa, hivyo hutumia njia na mbinu za kujifundisha na kujifunzia zilizo rahisi kwa wanafunzi wake kumwelewa..  

Katika hili mwalimu huweza kujitofautisha na mtu asiye mwalimu; kwa sababu si kila mtu anaweza kufundisha.

Kufundisha si kusimama mbele darasani na kuandika ubaoni; kufundisha kunaambatana na maadili, kanuni, falsafa na uwezo wa kuwasilisha ujumbe stahiki kwa wakati stahiki.  

Hivyo, Mwalimu bora ni mwanafunzi wa kudumu kwa sababu kila siku katika maisha yake huendelea kujielimisha na kutafuta maarifa mapya na kuyatumia.

Vilevile katika kutafuta mambo mapya, hupata mbinu na njia mpya za kujifunzia na kufundishia, sambamba na kuibua namna ya kufaragua zana rahisi kwa kutumia malighafi zipatikanazo katika mazingira yake, zitakazokidhi mahitaji na uwezo wa kila mwanafunzi wake.

Ni wajibu wa jamii kuendelea kutengeneza mazingira rafiki na mazuri kwa wanafunzi na walimu ili waweze kufikia malengo ya maendeleo ya taifa kwa kupitia elimu.

Ili kuendelea kufurahia uhuru wa taifa, watu hawana budi kuwa na tabia ya kuwa wanafunzi wa kudumu katika maisha ili waweze kupata maarifa mapya na ujuzi wa kukabiliana na changamoto mpya za maisha.