Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, ametangaza nia ya kuwasilisha hoja binafsi ya kuundwa kwa kamati teule ya Bunge kuchunguza matukio aliyosema yanayotishia usalama na umoja wa taifa letu.

Nionavyo mimi, japo suala lake limepata upinzani kiasi, tena kutoka kwa baadhi ya wabunge wa chama chake, ametumia njia sahihi ya kuisimamia Serikali kupitia ibara ya 63(2) ya Katiba.

Matukio hayo ni pamoja na kusinyaa kwa demokrasia na haki za binadamu, kupotea, kutekwa na kuuawa kwa raia katika chaguzi mbalimbali na matukio ya uhalifu katika medani za siasa.

Hoja nyingine ni kupigwa risasi na kuumizwa na kikundi ambacho kinaitwa “Wasiojulikana”, mauaji ya viongozi wa kisiasa na ukandamizaji wa uhuru wa raia kutoa maoni yao.

Si hivyo tu, Bashe anakusudia kulishawishi Bunge likubali kujadili na hatimaye kuundwa kwa kamati teule, kuchunguza matumizi mabaya ya sheria na ukandamizaji wa demokrasia ndani ya nchi.

Pia, haki za kikatiba na kisheria za vyama vya siasa kutoheshimiwa na tuhuma dhidi ya vyombo vya usalama na matumizi ya silaha za moto kwa raia kunakofanywa na vyombo vyenye mamlaka.

Ipo mifano mingi katika hoja za Bashe, ikiwamo kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 kwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu Septemba 7, 2017 katika eneo la makazi yake mjini Dodoma.

Kwenye suala la utekaji, hakuna ubishi hadi leo, wapo Watanzania wenzetu Ben Saanane na mwandishi wa habari, Azory Gwanda, ambao walichukuliwa na watu wasiojulikana na haijulikani wapo wapi.

Ipo mifano pia ya mauaji ya viongozi wa kisiasa si wa upinzani tu bali hata wa chama tawala tena wilayani Kibiti waliuawa zaidi ya viongozi 10 wa CCM, swali kuu likiwa ni nani wanaofanya haya?

Hoja hii ya Bashe si mpya kwani ndani ya Bunge kulishaibuliwa hoja za aina hii wabunge wakitaka chombo hicho kisimamishe shughuli zake zilizopangwa kwa siku husika ili lijadili kuongezeka kwa kitisho cha usalama.

Wapo wabunge waliokwenda mbali na kupendekeza hadi kuvialika vyombo vya kimataifa vya uchunguzi ikiwapo Scotland Yard, ili kuchunguza matukio ambayo pengine Serikali inanyooshewa kidole.

Kwa hiyo, nilitarajia leo hii wabunge wote wangemuunga mkono Bashe kwa sababu hoja yake imebeba maslahi ya umma.

Tutazame dhamira ya Bashe ya sasa, pasipo kutizama kauli zake zilizopita ambazo huenda alizitoa katika medani za kisiasa, huenda amekaa chini na kutafakari na kuona mahali alipokosea, sasa anarudi katika msitari sahihi.

Ni ukweli ulio dhahiri kuwa hofu imetawala kwa baadhi ya Watanzania kutokana na mwenendo wa matukio aliyoyataja Bashe, ambayo mengine yamesababisha damu za Watanzania kumwagika.

Kwanza inabidi tumpongeze mbunge huyo kwa ujasiri wake huu ambao hakika naamini, ni wabunge wachache wa CCM wangethubutu kulifanya hili. Hata kama haitaungwa mkono, lakini ujumbe utakuwa umefika.

Anachokifanya Bashe, ni kutumia chombo sahihi ili Watanzania wapate majibu sahihi ya hoja zake nane ambazo, kwa Mtanzania yeyote mwenye akili timamu, atajua ndizo zinazolitafuna taifa kwa sasa.

Wabunge na wananchi wanaomkosoa Bashe leo wanaweza kujiona wako salama sana, lakini wanaweza kukumbuka shuka wakati kumekucha. Bashe amewasilisha kile kilicho katika mioyo ya Watanzania. Hakuna ubishi kwamba umoja na mshikamano wetu umetikiswa na unaendelea kutikiswa na matukio aliyoyaorodhesha Bashe, ninaamini hoja yake itasaidia kuisafisha Serikali yetu inayonyooshewa kidole.

Kwa mtazamo wangu, huu ni wakati ambapo Serikali ingempa ushirikiano mkubwa Bashe ili kupitia Bunge, wale wanaoinyooshea kidole wakose cha kusema pale itakapobainika haina mkono wake.

Ndio maana nasema, tumuunge mkono Bashe, hoja yake ina mashiko.