In Summary

Ripoti za Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha Tanzania itaendelea kukua kwa zaidi ya asilimia sita kwa miaka mitano hadi 10 ijayo.

       Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi duniani. Unakua kwa zaidi ya asilimia sita kwa mwaka, na kutafsiriwa huenda ukasaidia kuiingia kwenye daraja la kipato cha kati.

Ripoti za Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha Tanzania itaendelea kukua kwa zaidi ya asilimia sita kwa miaka mitano hadi 10 ijayo.

Wastani huo wa ukuaji utaifanya Tanzania kuendelea kushika nafasi ya juu miongoni mwa nchi zinazokua kwa kasi, japokuwa mikakati ya kupunguza umaskini bado ni changamoto kwani ukuaji huo haujaonyesha matokeo chanya kwa wananchi, hasa maskini.

Wataalamu wanasema iwapo Tanzania inataka kufikia uchumi wa kipato cha kati basi inatakiwa kukua kwa zaidi ya asilimia 10 kwa miaka 10 mfululizo.

Ripoti ya Benki ya Dunia iliyotolewa mwezi uliopita inaonyesha, pamoja na changamoto mbalimbali ukiwamo ukame, ukosefu wa umeme wa uhakika, uduni wa miundombinu na ubanaji wa sera za fedha, bado uchumi unakua kwa kasi nzuri.

Mchumi mwandamizi wa Benki ya Dunia Afrika, Dk Albert Zeufack wakati wa kuwasilisha ripoti ya tathmini ya mwenendo wa uchumi wa Tanzania mwaka huu, alisema kasi ya ukuaji bado inaridhisha japokuwa kiwango chake hakitaweza kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa, katika kipindi kifupi na kati.

Hii ina maana kwamba Tanzania haitaweza kupunguza idadi ya masikini milioni 12 waliopo kwa sasa na huenda wakaendelea kuongezeka miaka ijayo kutokana na kutokuwa na uwiano baina ya ukuaji na ongezeko la idadi ya watu.

Wakati Tanzania ikisifiwa na mashirika mbalimbali ya kimataifa kwa kasi yake ya ukuaji uchumi, kasi hiyo haijaleta matumaini kwa Watanzania wengi hasa wanaoishi vijijini.

Hii ni kutokana na sera zilizopo kuelekezwa katika kujenga miji na majiji makubwa kwa kuyapamba kwa miundombinu ya kisasa wakati maeneo ya vijijini yakisahaulika.

Dira ya Maendeleo inalenga kuifanya Tanzania kuwa yakipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kwa kuongeza kipato cha kila Mtanzania kufika wastani wa Dola 4,500 za Marekani kwa mwaka (Sh10 milioni) kutoka takriban Dola 1,000 (Sh2.3 milioni) za sasa.

Kwa kuzingatia malengo ya dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025, pato la taifa kwa kila mtanzania linatakiwa kukua zaidi ya mara tatu ya sasa, katika kipindi cha miaka nane ijayo, suala ambalo wachambuzi wanasema huenda likawa ndoto kutokana na changamoto za uchumi wa dunia.

Wakati haya yakitokea, ongezeko la watu bado halitiliwi maanani sana katika mipango ya maendeleo. Japokuwa takwimu zinatolewa kila mwaka, ukuaji wa uchumi haujaweza kutosheleza kubadilisha maisha ya wananchi wa kawaida.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha idadi ya watu inatakiwa kuzingatiwa zaidi katika upangaji wa sera za kiuchumi kwani ndiyo walengwa zaidi, Serikali inatakiwa kuangalia masuala yanayowagusa Watanzania wengi, hasa walioko vijijini.

Ripoti ya hivi karibuni iliyochapishwa na Taasisi ya Uhusiano wa kimataifa na kimkakati (IRIS) inaonyesha Tanzania ni nchi ya 17 duniani kwa kuwa na kiwango kikubwa cha vifo vya akima mama na watoto, hasa maeneo ya vijijini ambako huduma za afya ni duni.

Changamoto ya ongezeko la watu, pia inaongeza ugumu katika kugawa rasilimali za kiuchumi. Matokeo yake maeneo ya mijini yanaendelea kushamiri kwa kupewa huduma bora za kijamii, huku watanzania wa vijijini wakiendelea kungojea huruma na utashi wa kisiasa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Novemba, kasi ya ongezeko la watu unaifanya Tanzania kuwa na wananchi wenye wastani wa miaka 15 ikimaanisha idadi kubwa ya Watanzania wana chini ya miaka 15 ambao miaka minane hadi 10 ijayo watakuwa kwenye soko la ajira na chachu ya maendeo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania.

Kwa kuwa Watanzania wengi wana wastani wa miaka 15, hata sera za kiuchumi na kijamii zinatakiwa kuelekezwa kwenye sekta ambazo watu hawa wapo. Kwa umri huo, wananchi wengi ni watoto ambao baada ya miaka 20 hadi 30 ijayo watakuwa wazazi, wafanyakazi, wafanyabiashara na viongozi nchini.

Kuboresha elimu

Kwa kuwa Watanzania wengi wana chini ya miaka 15, sera za kiuchumi na kijamii zinatakiwa kuelekezwa kwenye sekta ya elimu hasa ya awali na msingi. Maboresho ya mfumo wa elimu hii yatawasaidia watoto wengi kupata mafunzo bora ambayo yatawawezesha kushindana kwenye soko la ajira na kiuchumi.

Ni dhahiri, wigo wa elimu ya awali na msingi hasa shule za umma umeendelea kupanuliwa kwa kuandikisha watoto wengi zaidi baada ya malipo yote yaliyokuwa awali kufutwa.

Lakini cha kusikitisha, ripoti mbalimbali za Twaweza, shirika lisilo la serikali linalohusika na utafiti, shule nyingi za msingi za umma bado hazitoi elimu itakayoweza kumkomboa mtoto wa Kitanzania.

Ukosefu wa madarasa ya kutosha maeneo mengi ya vijijini na uchakavu wa majengo ya shule pamoja na ofisi na nyumba za walimu, vimesababisha baadhi ya wanafunzi kusomea chini ya miti.

Pia, shule nyingi hazina waalimu na hata zile zenye waalimu, ubora wa ufundishaji pia umekuwa ni changamoto kwani, baadhi ya waalimu wanafanyakazi kwenye mazingira magumu bila motisha.

Ubora wa elimu nao umekuwa ukitajwa kama changamoto itakayosababisha watoto hawa kushindwa kushindana na mataifa mengine.

Imeelezwa, badala ya Serikali kukuza biashara, kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji na kujenga majengo makubwa ya kibiashara, kasi kubwa inatakiwa kuelekezwa kuendeleza elimu. Iwapo rasilimali fedha nyingi itaelekezwa kwenye sekta ya, basi tutaweza kuwaandaa Watanzania wenye ushindani.

Hii ina maana, uwekezaji mkubwa unatakiwa kufanywa kwa watoto wenye chini ya miaka 15 ambao ni takriban asilimia 50 ya Watanzania wote.

Sekta ya Afya

Kwa kuwa Watanzania wengi wana chini ya miaka 15, msisitizo wa sera za uchumi wa Tanzania kwa sasa na baadaye unatakiwa kuelekezwa kwenye sekta ya afya.

Hii ni kuhakikisha wajawazito wanajifungua wakiwa salama pamoja na watoto wao hawapotezi maisha.

Ripoti za Shirika la Afya Duniani (WHO) inasema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua. Inaeleza wajawazito 36 katika kila 1,000 hufariki kila mwaka kiwango ambacho ni cha juu zaidi duniani.

Hii inatokana na uhalisia kwamba maeneo mengi bado yanakabiliwa na upungufu wa huduma za afya na vifaatiba kwa ajili ya kundi hilo.

Uwekezaji wa kipaumbele kwenye sekta ya afya utasaidia kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika, kuboresha afya za watoto ambao pia itawasaidia kujenga ubongo timamu kufikiri.

Uboreshaji wa huduma za afya ni muhimu zaidi ya uboreshaji wa huduma nyingine za kukuza biashara kwani husaidia kuwa na watu wenye siha njema, ambao watasaidia kusukuma ghurudumu la maendeleo.

Kwa kuwa afya na elimu vimetajwa kuwa ni chachu ya Tanzania kufikia kiwango cha uchumi wa kati, Serikali ina sababu ya kuwekeza zaidi kwenye maeneo hayo kuhakikisha hospitali, zahanati na vituo vya afya pamoja na shule zinakuwa na vifaa na wataalamu wa kutosha ili kuandaa wasomi mwenye afya nje kwa miaka ya baadaye.