In Summary
  • Hii ni mara yangu ya pili kumzungumzia Profesa huyu kutoka Mombasa, Kenya nikitumia maandiko yaliyomo katika kitabu chake: Cultural Forces in World Politics.

Leo, Oktoba 12 inatimia miaka mitatu tangu kufariki kwa Profesa Ali Mazrui, msomi aliyefundisha Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda na vingine kadhaa Marekani.

Hii ni mara yangu ya pili kumzungumzia Profesa huyu kutoka Mombasa, Kenya nikitumia maandiko yaliyomo katika kitabu chake: Cultural Forces in World Politics.

Si vibaya kuyarudia maandiko hayo kwa kuyahusisha na mkakati wa Serikali ya awamu ya tano kujenga uchumi wa viwanda.

Kwa vyovyote itakavyokuwa, ili dhana ya Tanzania ya viwanda iwe na maana ni lazima soko la ndani liwe na nguvu, lithaminiwe na si kutegemea soko la nje pekee.

Watanzania wenyewe wawe na utayari wa kununua bidhaa zinazozalishwa kabla ya kutegemea soko la nje ambalo kimsingi ni gumu na lenye ushindani mkubwa hasa kwa nchi changa ikiwamo Tanzania.

Viwanda vingi vilivyowahi kuwa gumzo nchini miaka ya nyuma mfano Kiltex, Urafiki, Mwatex, Sungura Textile, Sunflag na vinginevyo vinasuasua na vingine vimekufa. Moja ya sababu inaweza kuwa ushindani wa kibiashara au kutokuwa makini kwa uongozi wa viwanda hivyo.

Sababu nyingine ambayo naiona kubwa ni utayari wa Watanzania kununua bidhaa zinazozalishwa na viwanda hivyo. Nani amesahau namna fulana za viwanda hivi zilivyokuwa zikifanyiwa dhihaka na anayevaa kuonekana amepitwa na wakati baada ya nguo za mitumba kuanza kuingia kwa wingi?

Pamoja na ubora wa fulana hizo kuwa chini ukilinganishwa na zile za mitumba, bado zilibaki kuwa fulana ambazo mtu angeweza kununua na kuzivaa bila ya kudhihakiwa.

Katika dhana hiyo hiyo ya kutukuza vitu vya nje, Profesa Mazrui anasema Waafrika wamechukua kila kitu walichokiona na kukisikia kutoka nchi za Magharibi na kukikumbatia.

Anatolea mfano wa saa ya mkononi ya bei mbaya ambayo mtu anaona fahari kuivaa lakini hajali muda. Kwa maana nyingine mtu huyo anaweza akawa wa hovyo kuliko wote katika kujali muda.

Kwa maana nyingine kauli ya Profesa Mazrui inatoa msisitizo wa kutumia kitu chochote kutokana na umuhimu wake na si ufahari kama inavyokuwa kwa mwenye saa ya thamani kubwa.

Katika hali ya kawaida huna sababu ya kuvaa saa iliyotengenezwa Japan na kuikataa ya bei rahisi iliyotengenezwa Tanzania (kwa mfano) wakati hujali muda.

Ni hivyo hivyo kwa simu kila mtu anataka simu ya bei mbaya lakini si kila mwenye nayo anaithamini katika dhana ya mawasiliano.

Leo ikitokea Mtanzania akaamua kila siku katika maisha yake awe mwenye kuvaa fulana inayotengenezwa na kiwanda cha ndani iwe Mwatex au kingine chochote, hatopewa sifa ya mzalendo mwenye kusaidia pato la viwanda vya ndani badala yake atafanyiwa dhihaka na kuonekana hana kitu.

Dhana ya kwamba unavaa nguo kutokana na umuhimu wake haipo badala yake ni fursa ya kujionyesha na kukifanyia dhihaka kile ambacho kinaonekana kuwa cha hadhi ya chini.

Ubepari

Dhana ya uchumi wa viwanda inaleta picha ya ubepari ambao pamoja na Tanzania kutofuata sera zake ukweli ni kwamba ndio unaokumbatiwa na kuonekana kuwa na maana katika uchumi wa viwanda. Wakati baadhi ya watu wakiamini ubepari ni kitu kibaya, Profesa Mazrui anasema tatizo la Afrika ni kuchukua maudhui yasiyo sahihi kutoka kwenye mfumo huo, kuamini katika faida pekee na si ujasiriamali (profit motive but not entrepreneurial spirit).

Kuelekea Tanzania ya viwanda, dhana ya ujasiriamali bado haijapata mwamko. Watanzania wengi bado hawajawa tayari katika jambo hili. Wapo Watanzania wanaona ufahari kuwa na mashamba makubwa lakini hawayatumii kijasiriamali.

Mtu anaweza kuwa na shamba kubwa ambalo hajalitembelea hata kwa miaka miwili au zaidi, wakati mwingine hajawahi kupanda japo matunda yakamuingizia kipato au akapata ya kula au akatumia eneo hilo kuanzisha shughuli yoyote ya kumuingizia kipato. Ni kwa sababu dhana ya ujasiriamali haipo.

Profesa Mazrui pia anasema Waafrika wameibeba tamaa ya ubepari lakini hawana utayari wa kuthubutu kufanya jambo (risk taking). Hili nalo ni tatizo. Kwa Tanzania ya viwanda lazima kuwe na utayari wa kuthubutu kufanya jambo bila hofu ya kinachoweza kutokea.

Kingine ambacho Profesa Mazrui amekizungumza ni upotoshaji kuhusu ubepari na kutolea mfano wa kuamini katika kukua kwa miji bila ya kukua kwa viwanda. Kwa maana nyingine, kadri miji inavyokuwa na kupata hadhi hali hiyo iende sambamba na kukua kwa viwanda ambavyo vitakuwa chanzo cha ajira.

Upotoshaji mwingine, Profesa Mazrui anasema ni kuamini katika kutoa elimu isiyoendana na mafunzo ya uzalishaji (verbal education without productive training). Hili ni eneo jingine muhimu kwa Tanzania ya viwanda. Ni lazima kuwe na vyuo vya ufundi ambavyo vitatoa elimu ya uzalishaji kwenye viwanda, vinginevyo dhana nzima itakuwa ngumu kutekelezwa kwa maana wataalamu watalazimika kutoka nje.

Katika hali ya aina hiyo viwanda vitaingia gharama za ziada za wazalishaji ambazo zingeweza kupungua kwa kuajiri wenyeji ambao pia wangeweza kuanzisha viwanda vyao vidogo.

Anasema dhana ya viwanda, Japan walianza kuhubiri ukuaji wake tangu mwaka 1868.

Wajapan walitambua wanatakiwa kuiga kutoka magharibi lakini walikuwa makini katika mkakati huo.

Walitambua kwamba wanahitaji viwanda kwa kuiga baadhi ya mambo kutoka magharibi hivyo wakaja na kauli mbiu ya ‘mbinu za magharibi, ari au nafsi/ ya Kijapani.’