In Summary

Anasema safari yake ya ujasiriamali ilianza muda mrefu. Kabla hajaanza kutengeneza mbilimbi ambazo sasa anaziuza mpaka China, alishajaribu kuuza ubuyu, pochi, viatu na magauni ya harusi kisha akalima alizeti na mafuta yake.

       Dar es Salaam. “Wakati naanza biashara nililazimika kugawa mzigo wote bure ili kutengeneza jina. Nilitaka kuonyesha tofauti iliyopo kati ya pilipili waliyoizoea na yangu,” anasema Bertha Mleke, mhadhiri msaidizi katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere jijini hapa.

Anasema safari yake ya ujasiriamali ilianza muda mrefu. Kabla hajaanza kutengeneza mbilimbi ambazo sasa anaziuza mpaka China, alishajaribu kuuza ubuyu, pochi, viatu na magauni ya harusi kisha akalima alizeti na mafuta yake.

Licha ya yote aliyokuwa akifanya, kiu yake ilikuwa kumiliki kampuni ya usambazaji bidhaa anayoizalisha mwenyewe. Kutimiza ndoto hiyo, mbilimbi imefungua milango na kumuweka alipopataka.

“Ukiiona mbilimbi shambani huwezi kufikiri kuwa ni kitu ambacho kinaweza kukuingizia kipato kikubwa. Baadhi ya watu wanazidharau zinapokuwa mtini mpaka zinadondoka na kuoza,” anasema.

Anasema kosa linalofanywa ni kutoongeza thamani ya vitu vingi vinavyoonekana ni vya kawaida. Anasema leo anao uwezo wa kusimama sehemu na watu wengi wakaitambua bidhaa yake, Bero Mbilimbi aliounza Oktoba mwaka jana baada ya kufundishwa na rafiki yake, Rose Rugimbana aliyekuwa akipika aina hiyo ya pilipili bila kuivundika.

Alivutiwa kisha akajifunza na kuitangaza bidhaa hiyo. Mwanzo aliigawa bure ndipo akaanza kupata soko. Kwanza walikuwa wanafunzi wake kabla hajaanza kusambaza madukani na kuvuka mipaka ya nchi. Alianza kwa mtaji wa Sh300,000.

Licha ya kupika na kuisambaza bure mtaani bila ya kupata faida yoyote, hakukata tamaa bali alifuatilia vibali muhimu kutoka TBS, TFDA na akapata barcode ya bidhaa yake . “Haikuwa ngumu kupata vibali jambo lililonisaidia kuuza bidhaa zangu kwenye supermarket mbalimbali nchini,” anasema Bertha.

Kufika hapo, anasema aliitangaza mtaani pamoja na kuwaelimisha kuwahamasisha wateja wake ambao wengi walikuwa wanatumia mbilimbi isiyovundikwa. Alifanya hayo ili kukabiliana na ushindani uliopo sokoni.

Kufanikisha matangazo yake, anaitumia mitandao ya kijamii kupitia akaunti za watu wenye wafuasi wengi zaidi. Hata hivyo, kuna changamoto ya kutumia mfumo huo kuwafikia wateja wake. “Baadhi ya watu wanachukua hela na kula bidhaa bila kuitangaza,” anasema.

Baada ya kuona soko la ndani limekua kidogo alijaribu nje. Anasemma: “Sasa hivi nauza mpaka China, nilijaribu lakini matokeo yake sijaamini kwa kweli, zinagombaniwa.”

Huwa ananunua ndoo moja ya mbilimbi mbichi kwa Sh25,000 ingawa bei hupanda zinapoadimika lakini akizitengeneza kwa kuongeza pilipili, karoti, pilipili hoho na vitunguu huuza katoni moja yenye makopo 24 kwa Sh72,000.

“Kwa wiki natengeneza hadi mara tatu na oda ya chini kabisa huwa ni makopo 600 lakini inaweza kubadilika,” anasema Bertha.

Kutokana na mafanikio madogo aliyonayo anasema wakulima wa mazao anayoyatumia wanapata soko pia hivyo kuimarisha kipato kutokana na shughuli za mikono yao.