In Summary

Hoja ilisukumwa upya na Balozi Asha-Rose Migiro alipokutana na Watanzania, katika kanisa la Monrovia, Hornsey Jumamosi iliyopita.

Ubalozi Tanzania umemulika tena hoja muhimu ya wazalendo wakazi London kuuungana badala ya kuwa na migongano ya kijumuiya.

Hoja ilisukumwa upya na Balozi Asha-Rose Migiro alipokutana na Watanzania, katika kanisa la Monrovia, Hornsey Jumamosi iliyopita.

Akigawa faida za umoja, mafungu matatu, Mheshimiwa Migiro alisisitiza : “Urahisi wa kujenga nchi yetu nje na ndani kwa sauti moja, fursa ya kusaidiana kwa mazuri na shida, na wepesi wa mawasiliano ya kila aina.”

Akilinganisha Watanzania waishio maeneo mengine ya Uingereza kama Wales, Birmingham, Leicester na Milton Keynes , Balozi alisema haoni sababu gani ishindikane London.

Miaka ya karibuni zimejengeka hitilafu baina ya makundi ya London na kukosekana uongozi mmoja. Awali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisisitiza haja hiyo. Naye, Balozi wa awali , Mheshimiwa Peter Kallaghe, akasimamia kuundwa Tume ya kuunda katiba (“ Task Force London”) iliyomaliza kazi yake.

Balozi Migiro alisema hawezi kuunda umoja ila kuwa mlezi , mshauri na msimamizi wake hivyo motisha utaanzia kwa Watanzania wenyewe.

Mkutano huu uliodumu takriban saa tatu na nusu, uliitishwa na baadhi ya Watanzania wenye uchungu wa kuungana akiwemo Bwana Saidi Surur na Mariamu Kilumanga. Lilikuwa kusanyiko la kwanza kwa wakazi wa London tangu ujio rasmi wa balozi mwezi Juni 2016. Miezi ya karibuni Dk Migiro ametembelea Watanzania wa maeneo mbalimbali Uingereza ikiwemo kuzindua Jumuiya ya Wasanii Watanzania Uingereza (WASATU) Northampton, Aprili 2017.

Baada ya maongezi Mheshimiwa alifuturu na Watanzania. Kidesturi kila mwaka Watanzania hujumuika usiku mmoja kufungua na Waislamu chini ya usimamizi wa Ubalozi.

Mada ya tatizo la muungano wa Watanzania London, ilikuwa kati ya nyingi zilizoamshwa na maswali ya walio hudhuria.

Zingine ni kuhodhi ardhi , uraia pacha na umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa watoto na familia zetu ughaibuni.

Swali la ardhi na uraia pacha liliulizwa na mwanatamthiliya na mtayarishaji filamu , Simon Mzuwanda aliyeomba ufafanuzi wa kipengele cha kunyang’anywa mashamba ifikapo 30 Juni. Kama mwanataaluma wa sheria na kiongozi wa awamu mbalimbali za serikali, Dokta Migiro, alitathmini sheria ya umilikaji, haja ya kulipia kodi shamba ulilo nalo na kuwajibika kwa yeyote anayehodhi.

Akichanganua mada nyeti ya uraia pacha, Balozi Migiro alihimiza tena haja ya kuungana , akadai: “Ikiwa mlio Ughaibuni mtasimama kwa sauti moja na kupeleka dai kwa pamoja serikalini, bila shaka mtasikilizwa.”

Akichangamkia ulizo la Kiswahili (“ninakipenda sana Kiswahili”), lililorushwa na Bi Zuweina Kayugwa kuwa Watanzania ugenini hatusisitizi kuwafundisha watoto wetu lugha mama, Balozi alisisitiza lugha ni sehemu ya utamaduni. Mada iliungwa mkono na Patricia Mpangala aliyeeleza uzoefu wake jela za Uingereza zenye vijana wengi wa Kitanzania. Balozi alihimiza, fahari na mila zetu (kikiwamo Kiswahili) kunaweza kuchangia sana kuwazuia watoto wetu wasiende mstari mbaya wa kihalifu na kupotea potea, Majuu.