In Summary
  • Kila kocha ana shauku kubwa ya kutaka majina makubwa ya wachezaji wanaovuma kwa lengo la kuimarisha kikosi katika usajili wa majira ya kiangazi.

London, England. Msimu wa majira ya kiangazi umewadia kwa klabu za Ulaya kuingia vitani kuwania saini ya wachezaji nyota kuanzia Januari Mosi hadi 30.

Kila kocha ana shauku kubwa ya kutaka majina makubwa ya wachezaji wanaovuma kwa lengo la kuimarisha kikosi katika usajili wa majira ya kiangazi.

Majina makubwa yanayotawala midomoni mwa makocha maarufu ni Philippe Coutinho na Alexis Sanchez.

Coutinho anayewika Liverpool amekuwa akitakiwa kwa udi na uvumba na klabu ya Barcelona iliyomtupia ndoano mara tatu bila mafanikio.

Baada ya kushindwa kumsajili majira ya kiangazi, Barcelona imeongeza dau hadi kufikia Pauni 134 milioni zinazoonekana kukubaliwa na klabu hiyo ya Liverpool.

Pia Sanchez ameiteka dunia tangu alipoweka ngumu kumwaga wino Arsenal akishinikiza kutaka kuondoka kabla ya klabu hiyo kumbania.

Arsenal imemuwekea ngumu mchezaji huyo wa kimataifa wa Chile kuondoka licha ya kuwekewa mzigo wa maana na matajiri wa Etihad Manchester City.

Mbali na washambuliaji hao, libero wa Southampton Virgil van Dijk anaumiza vichwa vya makocha wengi Ulaya, baada ya kucheza kwa kiwango bora msimu huu.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, amekuwa na mapenzi makubwa na beki huyo wa kati kutoka Uholanzi akitaka kuimarisha ngome.

Usajili wa wachezaji hao umekuwa gumzo kutokana na umuhimu wa nyota hao ambao wote waligoma kutia saini mkataba wa kubaki katika klabu zao.

Usajili wa majira ya kiangazi, unatarajiwa kuiteka dunia kwa kuwa makocha wengi wameingia vitani kuwania saini za nyota wanaotaka kwenda kuimarisha vikosi vyao.

Philippe Coutinho (Liverpool)

Ni kiungo mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil ambaye amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu.

Mchango wake Liverpool umekuwa mkubwa tangu alipojiunga na kigogo hicho kutoka Inter Milan ya Italia. Barcelona ina amini Coutinho ndiye chaguo sahihi wa kuziba pengo la Neymar aliyetimkia Paris Saint Germain (PSG).

Coutinho amejenga kombineshi bora Liverpool licha ya kushambulia na kufunga mabao, lakini amekuwa chachu ya mafanikio ya nyota Sadio Mane na Mohamed Salah.

Alexis Sanchez (Arsenal)

Arsenal inahaha kumbakiza Sanchez majira ya kiangazi, baada ya kugoma kuongeza mkataba licha ya kuahidiwa nyongeza ya mshahara na posho.

Kocha Arsene Wenger alimsajili Sanchez akiwa na nia ya kuwaziba mdomo mashabiki waliokuwa wakimdhihaki baada ya kumpiga bei nahodha wake Robin Van Persie kwenda Manchester United.

Baada ya kutamba katika msimu wa kwanza akitokea Barcelona kiwango cha Sanchez kimeporomoka baada ya kuibua mzozo wa kutaka kuondoka majira ya kiangazi msimu uliopita.

Manchester City imeingia vitani kuwania saini ya nyota huyo katika usajili mpya wa majira ya kiangazi ikitaka kujaribu tena bahati yake.

Kocha wa Man City, Pep Guardiola aliyewahi kuinoa Barcelona, ni shabiki mkubwa wa Sanchez na ameapa kula sahani moja na Arsenal. Klabu hiyo ilitenga Pauni 50 milioni.

Virgil van Dijk (Southampton)

Southampton imeapa kutompiga bei beki huyo wa kati kutokana na ubora wake katika safu ya ulinzi akiwa mmoja wa vitasa mahirin duniani.

Licha ya Liverpool kutoa Pauni 60 milioni, lakini klabu hiyo ilimuwekea ngumu majira ya kiangazi msimu uliopita kabla ya libero huyo kugoma.

Van Dijk aligoma kuitumikia klabu hiyo na alirejea nyumbani Uholanzi wakati timu hiyo ikiwa katika maandalizi ya mechi za kirafiki za kujiandaa na msimu ujao.

Hata hivyo, Liverpool imedai itapambana kufa au kupona kuhakikisha beki huyo wa Southampton anangoka majira ya kiangazi msimu ujao.

Riyad Mahrez (Leicester City)

Misimu miwili iliyopita, iliibuka klabu moja kutoka King Power, Leicester City isiyokuwa na jina katika medani ya soka kwenye Ligi Kuu England.

Kocha Mtaliano Claudio Ranieri, aliibuka shujaa wa aina yake baada ya kuipa ubingwa wa Ligi Kuu England kwa kuvipiku vigogo vya soka nchini humo.

Ranieri aliyetua Nantes baada ya kufukuzwa ndiye aliyewaibua kina Riyad Mahrez ambaye amekuwa gumzo duniani kutokana na ubora wake.

Mahrez, mchezaji wa kimataifa wa Algeria, alikuwa nguzo ya Leicester City na mabao yake yalikuwa chachu ya mafanikio ya klabu hiyo.

Baada ya klabu za England kushindwa kupata saini yake msimu uliopita, Real Madrid imeingia vitani kutaka huduma yake msimu ujao wa majira ya kiangazi.

Zidane ambaye ana asili ya Algeria, anamtaja kiungo huyo wa pembeni ni mchezaji mwenye sifa ya kucheza Santiago Bernabeu kama anavyomtaja Harry Kane.

Ross Barkley (Everton)

Bila shaka Ronald Koeman atakuwa kwenye lawama kubwa baada ya kugoma kumpiga bei kiungo huyo.

Barkley alipambana sana kuondoka Makao Makuu Goodison Park, lakini kocha huyo aliyetimuliwa alimwambia ‘No’.

Chelsea ilitaka kwa udi na uvumba, lakini Koeman alimwambia huondoki ng’o huku akitishia kumuweka benchi endapo ataendelea kumsumbua.

Bila shaka dau lake la awali kutoka Pauni 25 milioni linaweza kuongezeka baada ya kufukuzwa Koeman.

Tottenham Hotspurs imerusha ndoano kutaka saini yake katika majira ya kiangazi huku ikimuahidi nyongeza ya mshahara kutoka Pauni 100,000 anaolipwa Everton.

Jonny Evans (West Brom)

Beki hakuwa na jina kubwa Manchester United licha ya kupewa nafasi katika safu ya ulinzi akicheza pacha na Chriss Smalling au Phil Jones.

Baada ya kupigwa bei kujiunga na West Ham Brom, thamani ya beki huyo wa kati imeongezeka na sasa anawindwa kwa nguvu Ulaya.

Manchester City imejaribu mara mbili kupata saini yake bila mafanikio, lakini msimu ujao wa majira ya kiangazi bila shaka itaongeza kasi kumng’oa West Brom.

Pep Guardiola anamtaka Evans kuziba pengo la nahodha Vincent Kompany na kwenda kuongeza nguvu katika safu ya mabeki wa kati akicheza sanjari na John Stones na Nicolas Otamendi.