Upole, unyenyekevu na kutojivuna ni sifa za pekee zinazombeba mwanamuziki mkongwe na nyota, Abwene Mwasongwe.

Nyimbo zake zenye kugusa mioyo ya watu na kutoa suluhisho na magumu yanayowapata wengi ndizo zilizomuinua zaidi mwanamuziki huyo.

Mwasonge ni kati ya waimbaji wa nyimbo za injili ambao wamefanikiwa sana kuihubiri injili kwa njia ya nyimbo

Baadhi ya nyimbo maarufu za mwanamuziki huyo ni  kama vile Tulikotoka ni mbali, Majaribu ni mtaji, Misuli ya imani, Tangulia Mbele, Elia, Ombi Langu na  nyinginezo nyingi.

Hivi karibuni Ambwene alifungua ukurasa mpya wa maisha yake baada ya kumvisha pete ya uchumba mwanadada Jaquelyn Walter wakitarajia kufunga ndoa yao mapema mwakani.

Bambika 101 ilifanya mahojiano na Mwanamuziki huyu nguli, endelea kufuatilia.

Tumaini; Hongera kwa hatua uliyoifikia ya kumvisha pete ya uchumba mwanadada Jaquelyn.

Ambwene: Asante namshukuru Mungu kwa hatua hii, uchumba tulitangaza tukiwa nyumbani kwao Kiluvya Dar es Salaam na Mungu akipenda mwakani tutafunga ndoa.

Tumaini: Miongoni mwa sifa zinazokubeba ni kutokuwa na majivuno tofauti na baadhi ya wanamuziki hasa wa injili ambao wamekuwa wakilalamikiwa. Nini siri ya kuwa hivyo?

Ambwene;  Siri kubwa ni asili ya kazi yenyewe ninayoifanya, unawezaje kujivuna wakati unapoifanya kazi ya Mungu? Sisi ni watumishi tusio na faida.

Tumeagizwa kunyenyekea na kuona wengine ni bora zaidi yetu. Binafsi nimeamua kumtumikia Mungu na nitaishi atakavyo yeye.

Tumaini: Ni yepi mafanikio uliyopata tangu uanze huduma hii ya muziki?

Ambwene: Watu kumjua Mungu kupitia huduma hii ni mafanikio makubwa mafanikio namba moja, pia kujulikana kwa watu binafsi naona ni upendeleo mkubwa.

Mambo hayo mawili yaani huduma kuwafikia wengi na kujulikana yamesababisha milango mingi ya maisha ya kimwili na kiroho kufunguka zaidi. Namshukuru Mungu kwa mafanikio haya makubwa kwangu.

 

Tumaini: Una mikakati ipi siku za baadae?

Ambwene; Nina mipango mingi hasa baada ya kumaliza digrii yangu ya uhasibu, nadhani ni muda muafaka kwa sababu sasa nataka kuwekeza kwenye eneo la usambazaji wa nyimbo za Injili ili kutoa fursa ya kuwasaidia wenzangu.

Ambwene: Changamoto ipo kwenye kuelewa muda sahihi wa kufanya kazi hii maana inahitaji kujitoa na kumtafuta Mungu sana ili ujue anataka nini.

Gharama ya kufanya jambo hilo ni kubwa zaidi kuliko zote japo inazo faida nyingi sana.

Hizi changamoto nyingine za kimwili wala hazina shida maana hata wasio mjua Mungu wanazo.

Tumaini: Wengi wangependa kujua safari yako kimuziki! Ambwene ametokea wapi?

Ambwene: Nilianza kuimba tangu nikiwa na miaka 14 baada ya kumaliza darasa la saba. Mwaka 2002 baada ya miaka mitatu nikatoa albamu ya kwanza inayoitwa Majaribu Ni Mtaji.

Albamu hii ilifanya vizuri na ndiyo iliyonitambulisha kwenye ulimwengu wa muziki wa injili.

Mwaka 2009 nilitoa kazi nyingine inayoitwa Heshima ya Mrefu ni Mfupi na mwaka 2012 niliachia kazi inayoitwa Misuli ya Imani.

Kwa sasa najiandaa kuleta albamu mpya hivi karibuni.