In Summary
  • Wastara alifanikiwa kwenda kwenye matibabu hayo, Februari 3, mwaka huu  baada ya kupata michango kutoka kwa watu mbalimbali akiwemo Rais John Magufuli aliyemchangia Sh15 milioni.

Msanii wa Filamu, Wastara Juma,  anatarajia kutua leo nchini, akitokea Mumbay nchini India alipokuwa anapatiwa matibabu ya mgongo na mguu.

Taarifa kutoka ndani ya familia yake zinasema Wastara anatarajiwa kuwasili majira ya saa saba mchana  katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.

Wastara alifanikiwa kwenda kwenye matibabu hayo, Februari 3, mwaka huu  baada ya kupata michango kutoka kwa watu mbalimbali akiwemo Rais John Magufuli aliyemchangia Sh15 milioni.

Kilichosababisha hadi afikie hatua ya kuchangiwa ni kutokana na Januai 4, mwaka huu, msanii huyo aliyekuwa mke wa marehemu Sajuki, kuandika ujumbe mrefu kwenye ukurasa wake wa Instagram kuomba msaada wa fedha Sh. Milioni 37, ili aweze kwenda kutibiwa baada ya kuhangaika kuzisaka bila ya mafanikio.

Katika kumpa faraja tayari Chama Cha Waigizaji Kinondoni ( Tdfaa Kinondoni ), kimewajulisha wana Filamu na watanzania kuwa kutakuwa na Mapokezi  ya Mwanatasnia mwenzetu  huyo.

“Chama kinawaomba waigizaji na wadau wote wa Tasnia ya Filamu tujitokeze kwa wingi kumlaki muigizaji mwenzetu na mpendwa wetu wastara juma  kwa furaha baada ya kufanikiwa katika matibabu yake’ Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu - pamoja tunajenga tasnia yetu’,lilisoomeka tangazo hilo lililosainiwa na Masoud kaftany, Afisa Habari, Uenezi , Mahusiano na Umma wa chama  hicho.

Ikumbukwe siku aliyeondoka kwenda nchini India wasanii wachache walijitokeza kumsindikiza ukilinganisha na idadi waliopo hali iliyozua maswali mengi miongoni mwa watu wanaofautilia tasnia hiyo ya filamu.