In Summary

Jibu la swali hili linajibiwa na Christian Bella, anayeweka wazi kwamba tayari wamepika wimbo wa pamoja, wanaotarajia kuuachia mara baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Dar es Salaam. Christian Bella anasifika kwa kuwa na tungo makini na sauti nzuri yenye matamshi mwanana ilhali Alikiba ni maarufu kwa tungo na sauti inayowavutia wengi. Itakuwaje wawili hawa wakikutana pamoja?

Jibu la swali hili linajibiwa na Christian Bella, anayeweka wazi kwamba tayari wamepika wimbo wa pamoja, wanaotarajia kuuachia mara baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mwimbaji huyo wa “Nani Kama Mama” alisema licha ya kutunga nyimbo nyingi zinazopendwa, ameamua kutunga wimbo maalum na kuimba na msanii huyo ili kutoa ladha ya muziki wa dansi wa kisasa kwa mashabiki wake wanaomwamini.

“Nimeshajijengea mashabiki kote Afrika Mashariki hata nje. Video ya “Nashindwa” imenitambulisha vizuri hivyo, nahakikisha kila nitakachokipika kwa mara nyingine, kiwe zaidi ya kile kilichotoka awali,” alisema Bella.

Alisema baada ya Ramadhani anatarajia kuachia kolabo yake mpya “Namgharimia”, aliyomshirikisha Alikiba.

“Kolabo hii imefanyika katika studio za Chedaz Records,” alisema Christian Bella akionyesha ‘umwamba’ mwingine wa tungo za mapenzi kwa kuachia simulizi tamu ya namna anavyomgharamia mpenzi wake.