In Summary

Bella ambaye alishindwa kufurukuta katika vipengele vyote alivyowania tuzo huku wimbo wake maarufu ‘Nani Kama Mama’ nao ukishindwa kutwaa tuzo kwa mwaka huu, amebainisha kwamba anachokifikiria kwa sasa ni kolabo za kimataifa na siyo za ndani.

Dar es Salaam. Siku tano tangu kutolewa kwa tuzo za Kilimanjaro KTMA, mteuliwa wa tuzo hizo na mwimbaji wa muziki wa dansi, Christian Bella amesema kuwa ndoto yake kwa sasa ni kurekodi muziki kwa kushirikiana na mwanamuziki nyota, Chris Brown.

Bella ambaye alishindwa kufurukuta katika vipengele vyote alivyowania tuzo huku wimbo wake maarufu ‘Nani Kama Mama’ nao ukishindwa kutwaa tuzo kwa mwaka huu, amebainisha kwamba anachokifikiria kwa sasa ni kolabo za kimataifa na siyo za ndani.

Mkali huyo ambaye anasiemama kama ‘solo artist’, akiimbia pia Bendi ya Malaika, alisema kuwa kwa muda mrefu alikuwa na ndoto hizo na sasa anaamini zitatimia kwa kuanza na wanamuziki wa Afrika.

“Nina ndoto za kufanya kazi na wanamuziki wa kimataifa,” alisema.

Bella alibainisha kwamba ameamua kuanza kufanya kazi na wasanii wenye majina makubwa akiwa na imani kwamba yote yatawezekana iwapo atapata meneja mzuri, atakayeweza kupambana na soko la muziki la nje.

“Kikubwa huwezi kukurupuka kama anavyofanya Diamond. Yeye tayari ana uongozi makini, wewe ukifanya hivyo itakuwa unakosea. Siku moja nikipata meneja kama Babu Tale na Fella, nitakuwa mbali, lakini kwa sasa ni ngumu,” alisema Bella na kufafanua:

“Nikiwa na meneja wa aina hiyo itanisaidia mambo mengi. Kama meneja watakuwa na uwezo wa kufanya baadhi ya mambo, ukichanganya na akili yangu na kipaji nilichonacho, nitaitangaza Tanzania kimataifa. Fikra zangu ni kuanza na Fally Ipupa, baadaye Chris Brown. Lazima uanzie chini, upate ujuzi ndipo upande juu.”