In Summary
  • Yalikuwa mashindano yaliyotengeneza umaarufu, fursa, ajira na kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa kwa ujumla. Lakini tangu kutokea kwa sakata lililohusisha ushindi wa Sitti Mtemvu mwaka 2014 na kukosekana kwa zawadi ya mshindi wa mwaka 2016 kuliyatia doa mashindano hayo.

Zawadi hewa, udanganyifu wa washiriki, kukosa wadhamini ni baadhi ya matukio yaliyoshushia hadhi mashindano ya Miss Tanzania. Kabla ya mwaka 2013, Miss Tanzania yalikuwa mashindano makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Yalikuwa mashindano yaliyotengeneza umaarufu, fursa, ajira na kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa kwa ujumla. Lakini tangu kutokea kwa sakata lililohusisha ushindi wa Sitti Mtemvu mwaka 2014 na kukosekana kwa zawadi ya mshindi wa mwaka 2016 kuliyatia doa mashindano hayo.

Sakata hilo lilikuwa gumzo nchini kabla ya mrembo huyo kukubali kulivua taji hilo na kukabidhiwa mshindi wa pili Lilian Kamazima.

Kampuni ya Lino International ambayo ilikuwa ikisimamia mashindano hayo, iliingia tena katika kashfa nyingine ya kushindwa kumkabidhi zawadi mshindi wa mashindano hayo wa mwaka 2016 /17, Diana Edward hadi pale Serikali ilipoingilia kati na kujikuta anapewa gari lililokwishatumika ambalo ni tofauti na aliloahidiwa.

Matukio kama hayo ndiyo yaliyosababisha Septemba 25, 2017 Serikali kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kuyapiga marufuku mashindano hayo.

Dk Mwakyembe katika kuyafungulia alitoa masharti kwa atakayekuwa tayari kuyaandaa mashindano hayo kuhakikisha zawadi wanazoahidi kuwapa washindi zinafikishwa kabisa ofisini kwake.

Ilipofika Februari 28, waandaaji wa mashindano hayo walitangaza rasmi kuacha kuandaa mashindano na kuikabidhi kampuni ya The Look chini ya Mkurugenzi Basilla Mwanukuzi ambaye aliwahi kuwa Miss Tanzania mwaka 1998.

Akizungumza wakati wa kutangaza hatua hiyo, Mkurugenzi wa Lino International Agency, Hashim Lundenga alisema uamuzi huo umetokana na malengo ya kutaka mashindano hayo kusimamiwa na damu changa kwa lengo la kuleta chachu katika tasnia ya urembo.

Ni kutokana na hatua hiyo, Aprili 7 kampuni hiyo ya The Look ilizindua tena kwa mara nyingine mashindano hayo katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es Saalam huku mgeni rasmi akiwa Dk Mwakyembe.

Katika hotuba yake, Waziri Mwakyembe anakiri kwamba mashindano hayo yalikuwa yametawaliwa na uhuni kwa miaka ya hivi karibuni na alitaka kuyafuta kabisa.

Anasema alikaa na Basilla na kuzungumza naye na kwamba, wameona mwelekeo wa yeye kutaka kuyarudishia heshima yake mashindano hayo ambayo yalikuwa na wapenzi wengi kipindi cha nyuma na kuwashauri wazazi kuwakubalia watoto wao warembo kushiriki.

Pia, katika Serikali kuweka mkono wake, waziri huyo anasema watamsaidia kutafuta wadhamini pale atakapokwama ikiwemo kuzishirikisha taasisi za umma.

Wakati kwa upande wa warembo, anasema angependa kuona wakimaliza mashindano hayo wapate ajira moja kwa moja kama ilivyo malengo mojawapo ya uanzishaji wa mashindano hayo ambapo anaahidi kuongea na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) badala ya kutafuta warembo mtaani wawachuke wanaotoka Miss Tanzania. “Binafsi naona warembo wanaoshiriki mashindano ya Miss Tanzania wana kila sababu ya kuajiriwa katika shirika hilo ukizingatia kwamba wana miondoko ambayo inatakiwa kwa wahudumu ya ndege,” anasema Dk Mwakyembe.

“Kinachotakiwa ni kwenda kufanyiwa mafunzo ya miezi mitatu au minne katika chuo chetu cha usafirishaji (NIT) na kuajiriwa, kwani tunataka kuona mashindano haya yanakuwa chanzo cha ajira na hatuoni haja ya kuajiri watu wengine wakati watoto wetu wapo.”

Basilla alivyojipanga

Akizungumza katika hafla hiyo, Basilla alisema lengo lake la kwanza ni kurudisha heshima ya mashindano hayo iliyokuwa imepotea.

Anasema anakumbuka enzi zake hata kama mtu hakwenda ukumbini kushuhudia mashindano hayo, lakini ilikuwa ukimuuliza Miss Tanzania ni nani anamjua na kueleza kwamba hiyo ni kuonyesha namna gani yalivyokuwa yanafuatiliwa.

Pia, anasema sababu nyingine iliyofanya shindano hilo lipendwe ni suala la kufanya kazi za kujitoa katika jamii kwa mrembo aliyeshinda lilikuwa kubwa ukilinganisha na sasa ambapo si kwa kiasi hicho.

Kuhusu ubabaishaji wa zawadi, anasema hawezi kuvumilia vitu kama hivyo kwani hata yeye aliposhiriki Miss Kinondoni alipata tatizo hilo na anajua uchungu wake, hivyo hatakubali litokee tena chini ya usimamizi wake.

“Ili kuhakikisha hilo halifanyiki nitahakikisha nawasimamia mawakala wote watakaochaguliwa kuandaa mashindano hayo katika ngazi ya zote,” anasema mrembo huyo.

“Pia kwa kuwa ubabaishaji mwingi wa zawadi hutokea ngazi ya vitongoji nimeamua kuvifuta na sasa watakutana ngazi ya mkoa na kisha kuelekea Taifa,” anasema Basilla.

Kwa upande wa warembo, amesema watahakikisha wanasimamia nidhamu zao ili wasichafue jina la mashindano hayo ambalo limepitia katika misukosuko.

Kuhusu mrembo gani angependa kumuona mwaka huu, Basilla anasema huo ni uamuzi wa wananchi kwa namna watakavyoshiriki kumpata, kwani si yeye anayemchagua, bali anapitia katika michujo mbalimbali na hii inaanza katika ngazi ya familia kwa wazazi kuwaruhusu watoto wao warembo kushiriki.

Maoni ya wadau na matarajio yao

Katika uzinduzi huo wadau mbalimbali walitoa maoni yao akiwemo Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza aliyesema baraza limefurahi kuona waliokuwa wanaanda awali wamekubali kunyoosha mikono.

Mngereza anasema hata walipoamua kulirudisha, waliona mikakati ambayo Basilla kaiweka na kuridhika nayo na kuongeza kuwa kwa namna alivyojipanga wanaona namna gani ataweza kurudisha imani kwa Watanzania.

Katibu huyo anasema kwa kuonyesha dalili nzuri hata kamati iliyopo sasa hivi ina usawa wa kijinsia tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo wanaume walikuwa wengi wakati kazi waliyokuwa wakiisimamia ilikuwa inahusisha watoto wa kike.

Naye mwanamitindo, Ally Rehmtullah aliyefanya kazi na waratibu wa mashindano hayo kwa miaka minane akiwavalisha washiriki, anasema anatarajia kuona vitu vikubwa zaidi na warembo bora.

Rehmtullah anasema mambo ambayo angependa yafanyiwe kazi ni pamoja na kuwepo kwa uratibu mzuri ikiwemo suala zima la shughuli kuanza kwa muda, kwani miaka ya hivi karibuni utaratibu huo haukuwa mzuri kiasi cha kuwakera watu.

Mdau mwingine ni aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2016, Diana Edward anasema katika uzinduzi huo ameona dalili nzuri ikiwemo wadhamini na anadhani siku za mashindano wataongezeka zaidi.

“Suala la wadhamini limeonekana kuwa shida, hivyo nashauri wengi wajitokeze siku itakapowadia kwa kuwa ni mashindano mazuri yenye kuzalisha ajira na kuitangaza Tanzania ndani na nje ya nchi,” anasema Diana.

Miss Tanzania mwaka 2010, Genevive Mpangala anasema ana imani na Basilla kwa kuwa ni mrembo ambaye anazijua vyema changamoto zilizopo kwenye mashindano hayo na anaamini zilizopo ndani ya uwezo wake atazifanyia kazi.

“Kwa kweli nampongeza Basilla na nina imani mashindano haya yatakuwa na utofauti mkubwa na ile chachu yake iliyoanza tangu mwaka 1994 wakati yanaanza kurudi,” anasema.

Mwanamitindo Fideline Iranga, anasema anaamini Basilla atafanya vizuri kwa kuwa anaijua vyema tasnia ya urembo, kwani kabla hajawa Miss Tanzania mwaka 1998 alikuwa mwanamitindo, hivyo anajua nini mashabiki wanakitaka katika shindano hilo.