In Summary
  • Ofisa Mtetezi wa Walaji Mwandamizi wa Tume ya Ushindani (FCC), Joshua Msoma alisema wateja wa bidhaa wanapaswa kuwa wadadisi ili kubaini bidhaa bandia zinazoingizwa kinyemela au kutengenezwa kwa kuiga.

Wateja wa bidhaa mbalimbali nchini wamepewa mbinu itakayowanusuru kujikuta wakinunua vitu vilivyokwisha muda wake, ikiwa ni katika kuhakikisha kwamba Watanzania wanadhibiti bidhaa bandia zilizozagaa.

Ofisa Mtetezi wa Walaji Mwandamizi wa Tume ya Ushindani (FCC), Joshua Msoma alisema wateja wa bidhaa wanapaswa kuwa wadadisi ili kubaini bidhaa bandia zinazoingizwa kinyemela au kutengenezwa kwa kuiga.

Alisema hilo likifanyika, litasaidia kuzibaini bidhaa hizo na kuziteketeza kwa mujibu wa sheria, kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha afya za walaji.

Msoma alibainisha kwamba umakini utasaidia kulinda masilahi ya walaji ambao wanapaswa kusoma maelekezo ya bidhaa kabla ya kuzinunua na kuzitumia. “Watanzania wengi wananunua bidhaa kwa kuwa wana fedha. Hawatafuti taarifa za bidhaa kama bei halisi, ubora, ila hulalamika wanapobaini tofauti na walichokitarajia. Ni wajibu wao kufahamu kila kitu kuhusu chochote wanachonunua,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa Utetezi wa Mlaji na Bidhaa Bandia, Godfrey Gabriel alisema watengenezaji au wafanyabiashara wengi wa bidhaa bandia hulenga zile muhimu au zinazotumika zaidi.

“Vifaa vya ofisini (stationery) bandia vinaongoza sokoni kwa asilimia 23 vikifuatiwa na vya ujenzi kwa asilimia 18 na umeme asilimia 16. Aina za bidhaa ambazo zinaongoza kwa kughushiwa ni wino wa printa, simu na televisheni,” alisema.