In Summary

Makamu wa Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani wa Hesabu Nchini (IIA), Gabriel Mwero aliwaambia wanahabari jana katika mkutano wa tatu wa taasisi hiyo kuwa mifumo iliyopo hususan serikalini, inakwamisha utendaji wao wa kazi.

Arusha. Wakaguzi wa ndani wa hesabu nchini wametaka kupatiwa uhuru katika utendaji kazi kwenye taasisi za umma na binafsi kwa kuripoti kazi zao moja kwa moja kwenye bodi zao.

Makamu wa Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani wa Hesabu Nchini (IIA), Gabriel Mwero aliwaambia wanahabari jana katika mkutano wa tatu wa taasisi hiyo kuwa mifumo iliyopo hususan serikalini, inakwamisha utendaji wao wa kazi.

Alisema Mwongozo wa kimataifa wa utendaji wa wataalamu (IPPF) wakiwapo wakaguzi wa ndani ambao umeridhiwa na Bodi ya Uhasibu wa Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), unataka wakaguzi wa ndani wapatiwe uhuru wa kuwajibika kwa bodi zao ili kuongeza ufanisi.

Awali, Mjumbe wa bodi ya mashirika nchini, lIkiwapo la PSI, Nada Margwe alisema kukosekana kwa uhuru wa wakaguzi wa ndani imekuwa ikichangia taasisi na mashirika mengi nchini kushindwa kufanya vizuri.

Margwe ambaye pia ni Mshauri wa masuala ya mahesabu, alisema nafasi ya ukaguzi wa ndani wa mahesabu inapaswa kupewa uhuru na vitendea kazi ili kuleta ufanisi katika taasisi husika.