In Summary

Kilio hicho kwa Rais kimekuja kufuatia agizo lililotolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama baada ya kufanya ziara kwenye vijiji mbalimbali vilivyopo wilayani humo kikiwamo kijiji hicho.

Pwani. Wafugaji wa jamii ya kimasai wa Kijiji cha Minazimikinda wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani, wamemuomba Rais John Magufuli kuangalia uwezekano wa kuwasaidia ili waendelee na ufugaji kijijini hapo kwa kuwa hawana sehemu ya kwenda kama Serikali ilivyowaamuru.

Kilio hicho kwa Rais kimekuja kufuatia agizo lililotolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama baada ya kufanya ziara kwenye vijiji mbalimbali vilivyopo wilayani humo kikiwamo kijiji hicho.

Mkuu huyo wa wilaya aliwaagiza wafugaji wote wawe wamehamisha mifugo yao kabla ya Oktoba 15, mwaka huu ikiwa ni mkakati wa kumaliza migogoro ya ardhi kati yao na wakulima ambayo huibuka mara kwa mara.

Wakizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo jana, wafugaji hao walisema agizo hilo limekuja ghafla na mpaka sasa hawajui sehemu watakakoelekea ikizingatiwa wameishi maeneo hayo kwa zaidi ya miaka 10.

“Tunamuomba mheshimiwa Rais asikie kilio chetu atusaidie tuendelee kuishi kwenye maeneo haya au kama kuna uwezekano Serikali itutengee maeneo na iturasimishie kwa hati miliki kulingana na mahitaji, tuko tayari kulipa ili tuendelee na shughuli zetu,” alisema Mwenyekiti wa Wafugaji kutoka kata za Kikongo na Ruvu, Charles Ole Masaya.

Mfugaji, Maneno Sangara alisema kumuomba Rais aingilie kati suala hilo si kwamba wanadharau mamlaka iliyotoa agizo hilo, bali wameamua kutafuta njia maridhawa itakayowasaidia huku wakiamini kuwa kiongozi huyo wa nchi ana uwezo mkubwa wa kusaidia kadri itakavyompendeza.

“Tunamuomba Mkuu wa nchi atuangalie kwa jicho la huruma na muda umekaribia wa agizo linalotutaka tuhamishe mifugo yetu.

“Ombi letu ni tutengewe maeneo maalumu, tuko tayari kulipia na kama miongoni mwetu watatokea watakaokikuka sheria tutakazowekewa basi wachukuliwe hatua,” alisema.

Akiwa kwenye ziara ya kikazi hivi karibuni katika vijiji vya Dutumi, Kwala na Minazi Mikinda, Mkuu wa Wilaya, Mshama alisema agizo lake halilengi kuwafukuza wafugaji bali wanatakiwa wahamishe mifugo yao kwenye maeneo hayo ili kumaliza migogoro iliyodumu kwa muda mrefu.