In Summary

Ushauri huo ulitolewa na Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Morogoro, Bertha Luzabiko alipozungumza na mwananchi. Alisema vibali vinasaidia wachimbaji kutambulika na kupata haki zao za msingi.

Morogoro. Wachimbaji madini wadogowadogo mkoani Morogoro, wametakiwa kuomba vibali maalumu vya uchimbaji vinavyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini ili watambulike kisheria.

Ushauri huo ulitolewa na Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Morogoro, Bertha Luzabiko alipozungumza na mwananchi. Alisema vibali vinasaidia wachimbaji kutambulika na kupata haki zao za msingi.

Luzabiko alisema kumekuwa na wimbi la wachimbaji wadogo wadogo kuendesha uchimbaji bila vibali maalumu kutoka wizarani, huku wakijua ni kosa.

Pia, ofisa huyo alisema kufanya hivyo ni kosa lakini wanajinyima haki zao za msingi, ikiwamo kukosa fursa zinazotoka serikalini.

“Serikali hutoa fursa ikiwamo mikopo mbalimbali, bila kibali ina maana utakuwa hujajisajili hivyo huwezi kuwa miongoni mwa wanufaika,” alisema Luzabiko.

Alisema wachimbaji wadogo wanatakiwa kuelewa kuwa vibali vya madini vinatolewa na Wizara ya Nishati na Madini, hivyo wawe makini katika uombaji.

Mchimbaji mdogo wa dhahabu mkoani hapa, Yahya Mkude aliiomba wizara hiyo kuwapa kipaumbele wachimbaji wa zamani kupata fursa zinazotolewa na Serikali.

Mkude alisema wachimbaji wa zamani wanaweza kuingizia Taifa pato tofauti na wanaochipukia, ambao wamekuwa wakipata ruzuku bila kukidhi vigezo.

Hata hivyo, Mkude alishukuru wizara hiyo kwa kuwajali wachimbaji wadogo ingawa changamoto ni nyingi zinazowakabili.

Utafiti unaonyesha Morogoro ina madini ya aina mbalimbali; rubby, spinal, dhahahu, mawe meusi na graphite.

Kupatikana kwa madini ya Graphite Kijiji cha Epanko wilayani Ulanga, kunaelezwa kutachochea kukua kwa uchumi wa mkoa huo.