In Summary

Benki hiyo kwa kushirikiana na taasisi yake ya fedha (IFC), imewaunganisha zaidi ya watu milioni 20.5 Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara huku ikiwa na lengo la kuwafikia milioni 250 ifikapo mwaka 2030.

Dar es Salaam. Wakati jitihada za kuwaunganisha zaidi ya wananchi milioni 6.5 kwenye umemejua zikipewa msukumo, Benki ya Dunia (WB) imesema wananchi wengi hawajui kutofautisha bidhaa halisi na bandia.

Benki hiyo kwa kushirikiana na taasisi yake ya fedha (IFC), imewaunganisha zaidi ya watu milioni 20.5 Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara huku ikiwa na lengo la kuwafikia milioni 250 ifikapo mwaka 2030.

Mwakilishi Mkazi wa IFC, Dan Kasirye alisema tangu mwaka jana mpango huo ulipozinduliwa wadau muhimu wameshirikishwa kuona namna ya kuufanikisha kwa tija inayohitajika.

“Tuna mpango wa kuwaunganisha wananchi milioni 6.5 ambao hawajafikiwa na gridi ya taifa kwa kutumia umemejua. Changamoto iliyopo ni uelewa mdogo wa wananchi juu ya ubora wa bidhaa hizi. Wachache wanaweza kutofautisha bidhaa bandia na halisi,” alisema Kasirye.

Alifafanua kuwa kwa utafiti walioufanya Mwanza na Arusha wamegundua ni asilimia saba ya wateja ndio wanaoweza kuzitofautisha bidhaa hizo na wauzaji watatu tu katika kila 10, wanaweza kufanya hivyo.

“Hii inamaanisha wauzaji wanapokwenda kununua bidhaa huangalia zinazouliziwa zaidi au za bei ndogo. Kutokana na hili, tunahitaji kutoa elimu ya kina kwa wananchi,” alisema.

Mpango huo wa Benki ya Dunia ulianza kutekelezwa kwa majaribio nchini Kenya mwaka 2008 kabla ya kupelekwa mataifa mengine 10 ya Afrika. Kabla haujaanza kutekelezwa nchini mwaka jana, tayari ulikuwa Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ethiopia, Kenya, Liberia, Mali, Nigeria, Rwanda, Senegal na Uganda.

Katika kufuatilia hilo, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeahidi kuongeza nguvu za kuwaelimisha wananchi kuhusu kuzingatia ubora wa bidhaa za umeme jua ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Mkurugenzi Mtendaji wa TBS, Profesa Egid Mubofu alisema shirika lake lina jukumu la kukagua bidhaa zote zinazoingia nchini na kubainisha kuwa IFC imeliwezesha kujenga maabara ya kisasa kukagua ubora wa vifaa vya umemejua. “Tunategemea vipimo vya maabara kupata uhakika wa ubora,” alisema Profesa Mubofu.