In Summary

Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alisema hayo kwenye mahafali ya wahitimu wa cheti cha weledi kutoka Taasisi ya Taaluma za Benki Tanzania (Tiob).

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania imezungumzia umuhimu wa maadili katika taasisi za fedha nchini, huku ikiwataka wahudumu kuendelea kujifunza ili kuboresha huduma za wateja wao.

Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alisema hayo kwenye mahafali ya wahitimu wa cheti cha weledi kutoka Taasisi ya Taaluma za Benki Tanzania (Tiob).

Profesa Ndulu aliwaambia wahitimu 141 walioshiriki mahafali ya 17 ya Tiob ambao walitunukiwa vyeti vya ngazi mbalimbali kuwa, ili kuwalinda wateja ni vyema wakasimamia maadili ya kazi zao. “Wateja wa benki hawawezi kuwa na imani na taasisi hizo kama wahudumu hawana maadili mazuri kumridhisha mteja,” alisema Profesa Ndulu.

Pia, aliwakumbusha wahitimu hao kuwa bila kujali kiwango cha elimu walicho nacho, maadili ndicho kitu muhimu katika kuwahudumia wateja na kutunza rasilimali za benki.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tiob, Patrick Mususa alisema wafanyakazi wengi wa benki zaidi ya 50 nchini hawana vyeti vya weledi wanavyopaswa kuwa navyo ili kuboresha utekelezaji wao.

Takwimu zilizopo zinaonyesha ni wafanyakazi 674 (sawa na asilimia 4.9) kati ya 15,000 waliopo kwenye benki hizo nchini wana vyeti hivyo. “Kati yao, 59 ni wanachama wa Tiob na wana leseni kutoka Benki Kuu ya kuendesha shughuli za benki,” alisema Mususa.

Utambuzi wa Tiob upo katika ngazi tatu ambazo ni cheti kinachotolewa kwa watu wenye elimu kuanzia kidato cha nne wakiwa na ufaulu mzuri kwenye masomo ya Hisabati na Kiingereza.

Mwingine ni Certified Professional Banker (CPB) kinachotolewa kwa waajiriwa wenye walau shahada, huku mameneja wakipewa Specialist Certificates.