In Summary
  • Wakati taarifa za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zikionyesha kuongezeka kwa makusanyo tangu Julai mpaka Septemba, ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mwaka ulioishia Julai inaonyesha iliongezeka kwa asilimia moja pekee.

Dar es Salaam. Licha ya mapato ya Serikali kuongezeka ndani ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha, mikopo ya sekta binafsi imeendelea kusuasua.

Wakati taarifa za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zikionyesha kuongezeka kwa makusanyo tangu Julai mpaka Septemba, ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mwaka ulioishia Julai inaonyesha iliongezeka kwa asilimia moja pekee.

Ripoti ya Agosti ya BoT inayoonyesha mwenendo wa mikopo ya benki za biashara kwenda sekta binafsi, ilipungua ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 15.2 uliokuwapo kipindi kama hicho mwaka jana.

“Kupungua kwa mikopo hiyo, kulitokana na tahadhari zilizochukuliwa na benki za biashara kukichangiwa na kupungua kwa rasilimali zake na amana za wateja,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti inafafanua kuwa sekta nafuu kidogo inajidhihirisha kwenye ujenzi na ukandarasi, hoteli na mighahawa ambazo ziliimarika.

Ripoti inaonyesha baada ya Juni kupungua kwa asilimia 22.1, mikopo ya sekta ya uchukuzi na mawasiliano kwa Julai ilishuka kwa asilimia 25.

Pia, hali kama hiyo ilijionyesha kwenye kilimo ambacho kwa Julai mikopo yake ilipungua kwa asilimia 9.4, baada ya kupungua kwa asilimia 0.2 Juni.

Baada ya kupungua kwa asilimi 5.8 Juni mwaka jana, mikopo binafsi iliongezeka kwa asilimia 8.3 wakati ile ya hoteli na migahawa ikiongezeka kwa asilimia 24.4, baada ya kukua kwa asilimia 7.9 Juni.

Ukuaji ujenzi, ukandarasi

Ujenzi na ukandarasi nayo ilikua kwa asilimia 16.7 Julai baada ya kufanya hivyo kwa asilimia 5.5 Juni.

“Mikopo ya biashara ilikuwa mingi zaidi, asilimia 20 ikifuatiwa na binafsi kwa asilimia 19.7,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Hata mwaka ulioishia Juni kwa ujumla, mikopo ya ndani iliyotolewa kwa sekta binafsi na umma ilipungua kwa Sh887.1 bilioni ikilinganishwa na ongezeko la Sh4.192 trilioni kwa mwaka ulioishia Juni 2016.

Hata hivyo, mwaka ulioishia Julai, BoT inasema mikopo ya Serikali kutoka benki za biashara iliongezeka kwa Sh1.246 trilioni.