In Summary

Homera amewatumia salamu viongozi hao kuwa watakamatwa muda si mrefu, lakini pia amefurahi kwa wakulima mkoani Ruvuma kufanikiwa kukusanya Sh79 bilioni zilizotokana na mauzo.

Tunduru. Wakati mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera akifurahia mafanikio ya kilimo cha korosho msimu huu, bado hajawaacha viongozi wa ushirika ambao hawajawalipa wakulima kilicho chao.

Homera amewatumia salamu viongozi hao kuwa watakamatwa muda si mrefu, lakini pia amefurahi kwa wakulima mkoani Ruvuma kufanikiwa kukusanya Sh79 bilioni zilizotokana na mauzo.

Fedha hizo zimetokana na mauzo ya tani 20,897 kwenye minada 13 iliyofanyika wilayani Tunduru.

Mkuu huyo wa wilaya ameliambia gazeti hili kuwa, kutokana na mauzo hayo wakulima wamefanikiwa kuboresha maisha kwa kuanzisha biashara, kusomesha watoto, kujenga nyumba bora na kuachana na zile za nyasi pamoja na kununua vyombo vya usafiri.

Amesema msimu huu kumekuwapo na ongezeko la uzalishaji ikilinganishwa na msimu wa 2016-2017 ambapo tani 15,800 ziliuzwa.

Homera amewataka wananchi ambao wana malalamiko ya kutolipwa fedha zao kuanzia mnada wa kwanza hadi wa 11 wavute subira, huku akiwataka viongozi wa vyama vya msingi katika wilaya za Tunduru na Namtumbo kuhakikisha wanawalipa wakulima wote madeni wanayodaiwa katika kipindi cha siku 11 kinachoishia Machi 8.

Kauli hiyo ameitoa kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakulima kutolipwa fedha zao ingawa tayari Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (Tamcu) kimekwisha viingizia fedha vyama vyao hadi za mnada wa 11 na kubakiza minada miwili kati ya minada 13 ya korosho.

Mkulima wa zao hilo, Hemed Abdallah alimshukuru mkuu wa wilaya kwa kubaini matatizo yanayowakabili wakulima kwa kuwa wengi wanategemea kupata fedha za malipo ya korosho ili waweze kutatua matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanyia shuguli za maendeleo.