In Summary

Uwekezaji huo, umekamilika baada ya pande zinazohusika kukubaliana juu ya masharti ya uhusiano huo mpya. Kwa uwekezaji huo, Barrick itakuwa inamiliki asilimia 15 ya hisa za kampuni hiyo ya nchini Canada.

       Dar es Salaam. Kuongeza uwekezaji wake, kampuni ya Barrick imenunua hisa milioni 48 za kampuni ya uchimbaji madini, Reunion Gold Corporation zenye thamani ya Dola 9.12 milioni za Canada (zaidi ya Sh16.12 bilioni).

Uwekezaji huo, umekamilika baada ya pande zinazohusika kukubaliana juu ya masharti ya uhusiano huo mpya. Kwa uwekezaji huo, Barrick itakuwa inamiliki asilimia 15 ya hisa za kampuni hiyo ya nchini Canada.

Kutokana na uwekezaji huo, Barrick itakuwa na haki ya kupendekeza mjumbe mmoja wa bodi ya wakurugenzi, kushiriki kwenye uamuzi wa uwekezaji wa kampuni hiyo utakaofanywa na kupinga uuzaji wa mradi wowote wa kampuni ya Reunion. Vilevile, Barrick itawajibika kupendekeza mjiolojia mmoja ambaye atasimamia uzalishaji kwa muda wote kwenye migodi ya kampuni hiyo.

Mwenyekiti wa kampuni ya Reunion, David Fennell aliikaribisha Barrick na kusema uamuzi wa kuwekeza kwenye kampuni hiyo ni heshima kubwa kwao.

“Uwekezaji huu ni kura ya uaminifu kwetu, wafanyakazi na kampuni kwa ujumla. Tunatarajia kutoa ushirikiano wa kutosha kukuza biashara yetu na kuongeza thamani ya fedha ya kila mwanahisa wetu,” alisema Fennell.

Kwa zaidi ya miaka 20, Barrick imewekeza nchini kwenye uchimbaji na usafirishaji wa dhahabu. Ikiongoza kwa biashara hiyo, shughuli zake zinatekelezwa na kampuni ya Acacia inayoendesha migodi mitatu; Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi.

Kutokana na uwapo wa tuhuma za udanganyifu uliofanywa kwa muda mrefu nchini kabla kamati mbili zilizoundwa na Rais John Magufuli hazijaubaini, marekebisho ya mkataba yamefanywa na mazungumzo yanaendelea ili kufidia sehemu ya kodi iliyokwepwa kwa miongo miwili ya uwapo wake nchini.