In Summary

Hata hivyo, pamoja na Acacia kuanza kulipa kodi, inaidai Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dola za Marekani 120 milioni (zaidi ya Sh240 bilioni za sasa) ikiwa ni malimbikizo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Dar es Salaam. Mgodi wa dhahabu wa North Mara ulioko Tarime, Mara unaomilikiwa na kampuni ya Acacia umeanza kulipa kodi ya mapato ikiwa ni mara ya kwanza tangu ulipopata leseni ya uzalishaji miaka 16 iliyopita.

Hata hivyo, pamoja na Acacia kuanza kulipa kodi, inaidai Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dola za Marekani 120 milioni (zaidi ya Sh240 bilioni za sasa) ikiwa ni malimbikizo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Akijibu maswali ya mwandishi wa habari hizi kuhusu utaratibu wa kampuni hiyo kulipa kodi ya mapato, Makamu wa rais wa Acacia, Deo Mwanyika alisema wameshalipia nusu ya kodi ya Dola za Marekani 20 milioni (Sh43 bilioni) inayotakiwa kwa mwaka huu na endapo bei ya dhahabu itaongezeka kwenye soko la dunia, kodi hiyo inaweza kuongezeka mpaka Dola 30 milioni (zaidi ya Sh60 bilioni).

Mgodi huo ulioanzishwa mwaka 1996 na kampuni ya AMGM ya Australia ulinunuliwa na kampuni ya Placer Dome Inc ya Canada mwaka 2004 na mwaka 2006 ukamilikiwa na kampuni ya Barrick Gold Mine pia ya Canada kabla ya kuuzwa kwa Acacia. Mgodi huo uliopata leseni ya uchimbaji mwaka 2000 unatarajiwa kufungwa miaka saba ijayo.

Akieleza sababu za kuchelewa kulipa kodi hiyo, Mwanyika alisema: “Uwekezaji wa mgodi ulihitaji gharama kubwa mwanzoni. Mwaka jana ndiyo tumerudisha gharama za uwekezaji na mwaka huu tuliweka malengo ya kulipa kiasi hicho,” alisema.

Kuhusu malimbikizo ya VAT, Mwanyika alisema mwaka 2009, Serikali ilianzisha kodi hiyo kwa kampuni za madini na mpaka 2012 ilikuwa inaidai TRA fedha hizo za malimbikizo ya kodi hiyo.

“Kimsingi hili ni deni tunalotakiwa kuliingiza kwenye gharama za uzalishaji, lakini tumeamua mwaka huu tuanze kulipa kodi. TRA wanatakiwa watulipe lakini haijasema ni kwa njia gani itakuwa ikilipa,” alisema Mwanyika.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo amekiri kuwa mgodi huo umeanza kulipa kiwango kilichokadiriwa. “Hata hivyo siwezi kukuambia ni kiasi gani walichoanza kulipia,” alisema.

Pia, Kayombo amekiri TRA kudaiwa na Acacia, lakini hakutaka kulifafanua deni hilo kutokana na matakwa ya Sheria ya Kodi yanayomzuia kutoa taarifa za mlipakodi. “Katika VAT kuna kudai na kudaiwa, ni kawaida kila mwezi, ni gharama kati yetu na mteja iwe tunamdai au anatudai na siwezi kujadili zaidi ya hapo,” alisema.

Meneja wa Ukaguzi na Uchambuzi wa Hesabu za Migodi wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), Michael Kambi alisema mgodi hutambua hasara au faida baada ya kuzingatia hesabu za kikodi kwenye kampuni tofauti na zile za kihasibu zinazotumika kwenye taasisi za kawaida.

Hivi karibuni, wakati akizungumza na wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Wizara ya Fedha na Mipango, Rais John Magufuli alizitaka kampuni za madini kuanza kulipa kodi na kuachana na visingizio kwamba zinapata hasara kila mwaka.