In Summary

Hayo yalielezwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Godwin Gondwe kwenye kikao cha wafanyabiashara wa madini na wachimbaji wadogo.

Handeni. Imeelezwa kuwa Serikali huenda ikapoteza Sh5.1 bilioni katika machimbo mbalimbali ya madini wilayani Handeni, kutokana na usimamizi mbovu wa kanuni na sheria za ukusanyaji mapato.

Hayo yalielezwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Godwin Gondwe kwenye kikao cha wafanyabiashara wa madini na wachimbaji wadogo.

Gondwe alisema baada ya kuripoti ofisini alifanya utafiti kuhusu mapato yanayopatikana katika sekta hiyo na kubaini kuna upotevu. Alisema aliwaita baadhi ya viongozi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, ambao walimthibitishia kuwa, kwa mwaka mmoja wa fedha Handeni imepoteza Sh1.7 bilioni.

Mkuu huyo wa wilaya alisema chanzo cha kupotea kwa mapato hayo, ni usimamizi mbovu wa ukusanyaji mapato na mianya ya rushwa.

Alisema wamefanya hesabu kuanzia mwaka 2014 mpaka 2016, iwapo hatua za kudhibiti hali hiyo hazitachukuliwa Serikali itapata hasara ya Sh5.1 bilioni.

Ofisa Madini Mkazi wilaya za Handeni na Kilindi, Frank Makyao alikiri kutofikia malengo ya ukusanyaji anayowekewa na Serikali kutokana na baadhi ya madini kusafirishwa bila kufuata taratibu na kwamba, zaidi ya Sh42 milioni hupotea kwa mwezi.

Mchimbaji na muuzaji madini ya ujenzi, Twaha Said alisema hali hiyo hutokana na kutokuwapo mikakati mizuri kati ya ofisi ya madini na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri, kila mmoja ana sheria yake ya ukusanyaji mapato hivyo kujikuta wanapoteza.

Said alisema wamekuwa wakitozwa ushuru kwenye zaidi ya mageti matatu ambako hulipa Sh20,000, hivyo ndani ya eneo moja wanalipa Sh60,000 kinyume na taratibu hali ambayo ikiendelea wanaweza kuacha kufanya shughuli hizo. Mwezi uliopita, Gondwe alikamata malori saba huku mawili yakitoroka yakiwa na madini ya ujenzi yaliyokuwa yakisafiri usiku bila ya kulipa kodi.

Baada ya kuyakamata aliamuru kupelekwa maeneo husika ili walipe ushuru kwa mujibu wa sheria.