In Summary
  • Juni mwaka jana, Serikali ilizuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya vyama pamoja na maandamano ikisema wakati wa kupiga kampeni umekwisha na kinachofuata ni kuchapa kazi na siasa za majukwaani zitarejea 2020.

Juzi, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Bahame Nyanduga alitoa ushauri kwa wanasiasa wanaonyimwa haki ya kukusanyika kwenda mahakamani kudai haki hiyo ambayo ipo wazi katika misingi ya sheria na Katiba.

Juni mwaka jana, Serikali ilizuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya vyama pamoja na maandamano ikisema wakati wa kupiga kampeni umekwisha na kinachofuata ni kuchapa kazi na siasa za majukwaani zitarejea 2020.

Katika kufikia uamuzi huo, ilisema hata katika nchi zilizobobea katika demokrasia, siasa huwa zinasimama mpaka wakati wa uchaguzi na kuwataka Watanzania wafanye kazi huku ikiwaasa wanasiasa kuhimiza kazi na kusubiri Uchaguzi Mkuu wa 2020 ambao kila mmoja atawaeleza wananchi kitu alichofanya katika kipindi hicho cha miaka mitano.

Hatua hiyo ya Serikali imekuwa mwiba kwa wanasiasa na wananchi waliokuwa wamezoea kuwasikia viongozi wao wa vyama wakizungumza majukwaani kuelezea masuala mbalimbali ya kitaifa.

Tangu wakati huo, wanasiasa wamekuwa wakilalamikia kunyimwa vibali vya kufanya mikutano ya hadhara ili kuzungumza na wapiga kura wao na kutafuta wanachama wapya na kuhakikisha wale walionao wanaendelea kuwakubali na kuwafuata.

Wanasiasa hao wamekuwa wakisimamia hoja kwamba ustawi wa vyama vya siasa ni muhimu kwa mustakabali wa ukuaji wa demokrasia na maendeleo. Wanadai kuwa vyama vya siasa hutumika kama mdomo wa wananchi kwamba kuna masuala ambayo hupenda kuyapigia kelele na kujua utekelezaji wake.

Pia, wamekuwa wakilalamika kwamba chama hakitakiwi kulala na viongozi wake kujifungia maofisini na katika vikao vya ndani tu.

Wanasema chama kinatakiwa kuongeza wanachama kila uchao kwa kuwashawishi kupitia utekelezaji wa sera na mikutano ya hadhara ya ufafanuzi.

Kwa nyakati tofauti wanasiasa mbalimbali wamejikuta wakiingia matatani kwa kufanya mikutano ya kisiasa kinyume cha taratibu, kufanya siasa nje ya majimbo yao ya uchaguzi na kutaka kufanya maandamano mambo ambayo wanasema yapo kisheria.

Hata waliopata vibali na kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao, nao wamekuwa wakilalamikia vitendo vya kukamatwa na polisi na kuhojiwa kwa kauli zao za kisiasa.

Hayo ni baadhi tu ya malalamiko ambayo yamemsukuma Nyanduga kuyatolea ufafanuzi na kuwataka wanasiasa kuacha kulalamika kwa kuwa wanaelewa vyema sheria ambayo inawaruhusu kwenda mahakamani kama wanaona kwamba wanakosa haki yao ya msingi.

Nasi tunadhani ni vyema wakafanya hivyo badala ya kufanya mikutano ya kiasiasa huku wakiwa na hofu ya kushushwa majukwaani au kukamatwa.

Kama Nyanduga alivyosema, “Haki ya mtu inapopokwa, sehemu ya kukimbilia ni mahakamani na wanasiasa wanajua hilo. Hili suala si la kuiachia tume peke yake, vyama vya siasa vinatambua fika haki hiyo ambayo iko wazi kisheria kama ilivyoainishwa kwenye Ibara ya 26(2) ya Katiba inayomtaka kila Mtanzania kuilinda Katiba.

Tukiunga mkono ushauri huo wa Nyanduga, nasi tunawashauri wanasiasa kwamba badala ya kufanya mambo ambayo yatahatarisha usalama wao na wafuasi wao, ni vyema wakafuata taratibu za kisheria kudai kile wanachoamini kuwa ni haki yao.

Kufanya mkutano bila kibali au wakati kuna zuio ni kukiuka sheria na madhara yake ni pamoja na hayo kupoteza muda mwingi katika mikono ya sheria.