In Summary
  • Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 baada ya wageni kutangulia kufunga na wenyeji kusawazisha.

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, juzi ilikuwa na mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Malawi uliochezwa jijini Dar es Salaam. Mchezo huo ulikuwa sehemu ya mechi za Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa.

Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 baada ya wageni kutangulia kufunga na wenyeji kusawazisha.

Lakini lengo hapa si kuzungumzia mchezo huo, tunachokiona hapa ni ushirikishwaji wa wachezaji katika kuweka mipango ya timu.

Kila Mtanzania shabiki wa soka anasikilizia kwa sasa nini kinaandaliwa kwa ajili ya kuifikisha Taifa Stars Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 zitakazofanyika Cameroon.

Kwanza, timu zimeongezeka kutoka 16 hadi 24. Hii ni nafasi sasa kufanya kila liwezekanalo kutumia fursa hiyo ya kuongezeka kupata tiketi ya kwenda Cameroon.

Tunaweza kusema kiu ya miaka zaidi ya 39 ni kubwa. Wenzetu wa Uganda wameshakata kiu yao baada ya kushiriki fainali zilizopita, ikiwa ni mara ya kwanza tangu wafuzu mwaka 1979 nchini Gabon.

Wiki iliyopita, nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta alihojiwa na redio moja, na kitu kikubwa alichosema ni mikakati ya kuisaidia Tanzania kufika kwanza fainali za michuano ya timu zinazoundwa na wachezaji walio katika ligi za nyumbani kwao, CHAN, zitakazofanyika Cameroon mwaka 2019.

Mbwana alisema kocha lazima aelekeze nguvu kwa wachezaji wanaocheza soka ya kulipwa nje ya Tanzania kwa kuwa hakuna taifa linalofika mbali kwa kutegemea wachezaji wa ndani pekee, lakini akatahadharisha kuwa mafanikio kama hayo yatachukua muda mrefu.

Pia alizungumzia mipango ya muda mrefu na mfupi, na kipindi cha mpito kuelekea mafanikio ni kuhakikisha wachezaji wa nje wanakuja Tanzania bila kujali yuko vipi.

Alisema hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kwa kuwa huko waliko wanakuwa na ladha tofauti na kinachotakiwa ni muunganiko kidogo tu wa kucheza.

Cha pili ni maendeleo ya vijana. Samatta alisema kwa sasa uwekezaji kwenye timu za vijana, hauwezi kufikia malengo ya muda mfupi.

Vijana watumike lakini kwa malengo ya muda mrefu ambayo yakisimamiwa yanaweza kutoa mwelekeo mzuri. Hakuna ubishi kwamba, mataifa mbalimbali yanawekeza kwenye soka ya vijana.

Tunapongeza ushauri wa nahodha huyo wa Taifa Stars ambao unaonyesha kwamba wapo wachezaji wengi nje ya nchi wanaoweza kuanza kutumiwa kwa ajili ya kutengeneza mazingira mazuri ya maendeleo.

Ni muhimu kwa watu waliopewa dhamana ya maendeleo ya soka Tanzania wakachukulia ushauri huo na utakaotolewa na wachezaji wengine katika kutafuta njia bora ya kuendeleza soka letu ambalo ni kama limedumaa.

Samatta amewakilisha idadi kubwa ya wachezaji ambao wanaumizwa na kudumaa kwa soka letu waka anaona kuwa kuna uwezekano wa kulikwamua kwa njia za muda mrefu na mfupi.

Tunahitaji kuunganisha mawazo ya wadau wengi zaidi badala ya watu wachache kujifungia ofisini na kutoka na mkakati ambao si shirikishi na hauakisi mazingira yetu, hali ambayo inaweza kuufanya ukwame mapema kwa kuwa watekelezaji hawatakuwa sehemu ya mkakati huo.