In Summary
  • Hivi ndivyo alivyofanya Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza na ajenda yake ya “kilio cha mazingira”.

Sauti ya kiongozi yeyote wa dini inapanda mbegu kwenye mioyo ya waumini na matunda ya kazi hiyo yanaweza kufurahiwa hata na vizazi vingine.

Hivi ndivyo alivyofanya Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza na ajenda yake ya “kilio cha mazingira”.

Sauti yake imekuja katika kipindi ambacho misitu iko kwenye shinikizo kubwa la binadamu, anayeikata kukidhi mahitaji ya kuni na mkaa, huku akiteketeza misitu kwa ajili ya kilimo.

Umasikini unachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira.Wananchi wanaendelea kutegemea misitu, ili kuendesha maisha yao ya kila siku hali inayoongeza tishio zaidi kwa mazingira.

Sio mara zote ajenda za aina hii hupata nafasi kwenye nyumba za ibada, licha ya ukweli kuwa athari za uharibifu wa mazingira zinagusa moja kwa moja masilahi ya waumini.

Sehemu ya muda wake wakati wa uzinduzi wa majengo na miudombinu ya Chuo Kikuu cha Karagwe(Karuco) Askofu Bagonza aliutumia kuonya juu ya athari za uharibifu wa mazingira.

Aliwaeleza waumini na wananchi waliohudhuria tukio hilo katika kijiji cha Kishoju, kuwa tabia zetu zinachangia kuleta majanga ya mazingira na kutaka kila mmoja kuwajibika kwa nafasi yake.

Alikumbusha kuwa tabia zetu ndizo zimesababisha mabadiliko ya tabia nchi na kuwa chanzo cha ongezeko la majanga yanayosababisha maangamizi ya watu na mali kila kona ya dunia.

Alionya kuhusu uharibifu wa mazingira. Alisisitiza ni chanzo cha mafuriko na ukame. Alikumbusha kuwa mazingira salama yanaongeza thamani na utu wetu.

Ili ajenda yake iwe endelevu, Askofu Bagonza ni mwasisi wa wazo la kuanzisha chuo Kikuu cha Karagwe ambacho kitafundisha kilimo na stadi za mazingira baada ya taratibu kukamilika.

Nchi nyingi duniani tayari zimeonja madhara yatokanayo na athari za uharibifu wa mazingira ambapo katika nchi masikini majanga ni makubwa zaidi.

Majanga ya mafuriko na ukame yanasabisha maafa makubwa zaidi, kwa kuwa nchi nyingi hazina uwezo wa kukabiliana na matokeo yake ikilinganishwa na nchi zilizoendelea.

Ukirejea kwenye ajenda ya Askofu Bagonza, ni wazi kuwa kila mtu ana wajibu wa kutekeleza ili kulinda na kuhifadhi mazingira kwa ajili yetu na vizazi vijavyo.

Katika hatua hii viongozi wa dini wana nafasi na sauti kubwa zaidi ya kufanikisha mapambano dhidi ya uhifadhi wa mazingira kupitia kwa waumini na wafuasi wao.

Mara nyingi sauti za viongozi wa dini zinasikika wakati wa kutuliza mawimbi pale zinapoonekana dalili za kutoweka kwa amani na kuibuka chuki na ulipizaji visasi.

Hata hivyo, sauti za kundi hili zinahitajika zaidi katika ajenda ya mazingira kwa kuwa athari za uharibifu wake ni mzigo mzito kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa.

Nguvu ya viongozi wa dini inaweza kusaidia kuwa na kinga dhidi ya uharibifu wa mazingira, badala ya kusubiri kutumia gharama kubwa kupambana na matokeo ya uharibifu.

Hivi sasa Serikali inaangalia uwezekano wa kufunga ziwa Victoria kwa muda, ili samaki waweze kuongezeka baada ya kukithiri kwa uharibifu wa mazingira ya ziwa.

Kupungua kwa samaki katika ziwa hilo ni matokeo ya athari za kimazingira, ambazo zilitakiwa kudhibitiwa mapema kwa kutumia sauti za viongozi wa dini na makundi mengine.

Ni wazi kuwa uharibifu wa mazalia ya samaki usingekuwa mkubwa kama ilivyo sasa, kama suala hilo lingekuwa sehemu ya mahubiri ya viongozi wa dini. Tayari Serikali imetunga sheria ya usimamizi wa mazingira kama njia ya kuhakikisha upatikanaji wa maendeleo endelevu kupitia usimamizi mzuri wa mazingira katika maeneo yote nchini.

Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya mazingira nchini ya mwaka 2014 iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, maelfu ya hekta za misitu zinateketezwa kila mwaka kutokana na shughuli za binadamu.

Kati ya mwaka 1990 na 2000 Tanzania ilipoteza wastani wa hekta 413,000 za misitu.Takribani asilimia moja ya eneo la misitu sawa na hekta 400,000 hupotea kila mwaka.

Ni kweli tunaweza kuwa na sheria nzuri za kusimamia na kudhibiti uharibifu wa mazingira ingawa kwa upande wa pili tuwekeze elimu kwa wananchi ili mazingira yawe na kinga ya kudumu.

Elimu hii inaweza kutolewa kupitia majukwaa tofauti zikiwamo nyumba za ibada na kuanzia hapo wananchi wenyewe wanaweza kudhibiti shughuli za binadamu zinazoathiri mazingira katika maeneo yao.

Phinias Bashaya ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi mkoani Kagera. 0767489094