In Summary
  • Aliyataja mazao hayo kuwa ni korosho, tumbaku, chai, kahawa na pamba. Haya kwa miaka mingi yamekuwa tegemeo kubwa kwa uchumi wa Taifa lakini kutokana na sababu mbalimbali uzalishaji wake umeshuka na athari zake zinaonekana sio katika hazina ya nchi pekee, bali hata kipato cha mkulima mmojammoja.

Mwishoni mwa wiki, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikaririwa na vyombo vya habari akisema Serikali imeamua kufufua mazao makuu matano ambayo yanaingiza kwa wingi fedha za kigeni nchini.

Aliyataja mazao hayo kuwa ni korosho, tumbaku, chai, kahawa na pamba. Haya kwa miaka mingi yamekuwa tegemeo kubwa kwa uchumi wa Taifa lakini kutokana na sababu mbalimbali uzalishaji wake umeshuka na athari zake zinaonekana sio katika hazina ya nchi pekee, bali hata kipato cha mkulima mmojammoja.

Katika hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka 2017/2018, waziri wake, Dk Charles Tizeba alisema, “Katika msimu wa mwaka 2016/2017, uzalishaji wa mazao makuu ya asili ya biashara ambayo ni korosho, miwa, pamba, mkonge, kahawa, chai, tumbaku na pareto umepungua na kuongezeka kwa viwango tofauti ingawa uzalishaji wa jumla kwa mazao hayo umeongezeka kufikia tani 881,583 ikilinganishwa na tani 796,502 mwaka 2015/2016. Uzalishaji unaoendelea kwa mwaka 2016/2017 na matarajio kwa mwaka 2017/2018 ni kuzalisha jumla ya tani 953,825.”

Alisema uzalishaji wa mazao ya bustani ambayo ni matunda, mboga, maua na viungo umeongezeka kutoka tani 5,931,906 mwaka 2015/2016 hadi tani 6,216,145 mwaka 2016/2017 na kwamba hali hiyo imetokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa matunda na mboga yakiwamo parachichi, nyanya na matikiti.

Kwanza tunapongeza hatua ya Serikali kuzinduka na kuamua kuyavalia njuga mazao. Tunaamini kwamba hatua hiyo ni mwelekeo mzuri, si tu wa kuliingizia Taifa fedha za kigeni, bali kuinua uchumi wa mkulima kama tulivyoeleza lakini pia kufanikisha mkakati wake wa viwanda.

Ili mpango huo wa Serikali ufanikiwe, mambo manne hayana budi kutiliwa maanani; kuhakikisha kunakuwa na pembejeo bora ambazo zinapatikana kwa wakati, kuwapo kwa miundombinu ya uhakika kwa ajili ya kilimo chenyewe na usafirishaji wa mazao, kupanua wigo wa masoko na mwisho ni kuhakikisha hakuna mazao yanayouzwa nje yakiwa ghafi pasi na kuchakatwa.

Tunafahamu, suala la pembejeo limekuwa donda sugu kila msimu wa zao fulani unapowadia, wakulima wamekuwa wakikosa zana muhimu za mazao au kuzipata nje ya wakati hivyo kuwakwaza katika uandaaji wa mashamba na ukuzaji wa mazao kwa tija.

Tunaamini Serikali ikilivalia njuga hili na kulimaliza, tutakuwa tumepiga hatua moja katika azma hiyo.

Kadhalika, habari kwamba kuna mazao yameozea shambani kutokana na kukosa usafiri si ngeni masikioni mwetu, barabara zinazounganisha sehemu za mashamba na zile kuu ni muhimu katika kuwahakikishia wakulima masoko na hili ni jambo muhimu mno katika kuwavutia wananchi kuchangamkia sekta hii.

Jambo la mwisho ni uchakataji wa bidhaa. Hili lina umuhimu wa kipekee kwani ni sawa na kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Tukichakata mazao yetu hapahapa nchini tutawahakikishia wananchi wetu ajira na pia tutayaongeza thamani.

Mathalani, nyuzi zinazotengenezwa kwa kilo moja ya pamba zinaweza kuwa na thamani ya hata mara tano au zaidi kama bidhaa hiyo ingeuzwa ikiwa ghafi.

Kwa bahati nzuri, siku hizi kuna teknolojia rahisi kwa bei na hata matumizi ambazo zinaweza kusaidia katika kuongeza thamani ya mazao yetu na huo ndiyo mwelekeo tunaotakiwa kuuchukua.