In Summary
  • Ajali hiyo imekuja ikiwa ni takriban wiki moja tangu Watanzania wengine 15 wapoteze maisha kwa ajali ya lori iliyotokea mkoani Rukwa Septemba 4.

Juzi, Watu 12 walifariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya basi dogo walilokuwa wakisafiria kutumbukia ndani ya Ziwa Victoria baada ya ya breki kushindwa kufanya kazi eneo la kivuko cha Kigongo mkoani Mwanza

Ajali hiyo imekuja ikiwa ni takriban wiki moja tangu Watanzania wengine 15 wapoteze maisha kwa ajali ya lori iliyotokea mkoani Rukwa Septemba 4.

Katika ajali hiyo, watu 15 walifariki dunia papo hapo na wengine tisa kujeruhiwa baada ya lori walilokuwa wakisafiria kupinduka eneo la Ntembwa ndani ya Hifadhi ya Lwafi wilayani Nkasi mkoani Rukwa. Ajali hiyo ilitokea saa mbili usiku baada ya lori aina ya Fuso lililokuwa limebeba abiria na magunia ya mahindi likitokea Kijiji cha Mvimwa kuelekea Kijiji cha Wampembe kupinduka.

Baada ya ajali hiyo, wadau mbalimbali walielezea masikitiko yao akiwamo Rais John Magufuli ambaye katika salamu zake za rambirambi kwa mkuu wa mkoa wa Rukwa, Zelothe Stephen alizitaka mamlaka zinazohusika na usalama barabarani kuongeza juhudi zitakazowezesha kukabiliana na matukio ya ajali ili kuokoa maisha ya watu na mali.

Hata hivyo, tukio la ajali hiyo lina viashiria vingi vya kutozingatiwa usalama wa abiria kwa kuwa lori hilo lilikuwa limepakia pia magunia ya mahindi na mashuhuda wameeleza kwamba lilikuwa katika mwendokasi na hivyo kumfanya dereva ashindwe kulimudu.

Tukio hilo na lile la kivuko cha Kigongo hayatofautiani sana. Tofauti iliyopo ni ya kimazingira, lakini magari yote mawili yalikuwa na abiria na pia yalikuwa katika mwendo wa kasi.

Katika tukio la Kigongo, inaelezwa kwamba basi hilo aina ya Toyota Hiace lilipata hitilafu mita chache kutoka geti la kivuko, hali iliyosababisha kugonga mageti mawili na kutumbukia ziwani.

Gari hilo lilikuwa likitokea Nyegezi jijini Mwanza kwenda Busisi wilayani Sengerema.

Ajali hii ina sura mbili; kwanza kuna uzembe uliofanywa na dereva ukiwa ni ule wa kuendesha kwa kasi bila kuzingatia eneo alilokuwa na bila kujali kwamba alikuwa na roho za watu.

Lakini suala la pili ni kwa mamlaka za Serikali kutotenga eneo maalumu ambalo magari yote ya abiria yatalitumia kama kituo cha kushusha na kupakia abiria mbali kidogo na kivuko.

Tunasema hivyo kwa sababu magari yote ingawa hayaruhusiwi kuingia ndani ya kivuko yakiwa na abiria, huwashusha abiria mita chache tu kutoka kivuko kinapoegeshwa.

Hii ni hatari hasa kama gari likipata hitilafu ya breki kwa kuwa linaweza kusababisha vifo vya watu wengi kwa kusererekea ziwani kama ilivyotokea juzi.

Ni vyema mamlaka husika zingeweka kituo cha kushukia abiria mita 200 au zaidi kutoka eneo la vivuko kwa kuwa ni eneo lililo mbali, umbali ambao ungewasaidia hata madereva kuanza kuchukua tahadhari wakiwa mbali kabla hawajafika katika kituo hicho.

Kwa nia ya kuhakikisha usalama zaidi, mageti yaliyopo eneo la kivuko yasogezwe mbali ikiwezekana geti la kwanza liwe umbali wa mita 600 na linalofuata kabla ya kuingia kivukoni liwekwe mita 400 kutoka eneo la kivuko. Hiyo inaweza kuwa ni kinga ya ajali kama iliyotokea juzi. Hata hivyo, kama alivyosema Rais Magufuli ni vyema mamlaka zinazohusika zikachukua hatua zaidi kudhibiti ajali za barabarani na majini.