In Summary

Tafiti zimegawanyika katika makundi mawili ambayo ni tafiti za msingi na za matumizi.

        Kwa tafsiri ya kawaida na rahisi, utafiti ni uchunguzi unaotumia mbinu za kisayansi katika kutafuta taarifa juu ya jambo fulani, ili kupata ufumbuzi pamoja na kuongeza maarifa.

Tafiti zimegawanyika katika makundi mawili ambayo ni tafiti za msingi na za matumizi.

Kwa mfano, tafiti za matumizi hutumika katika kufanya uamuzi au kutatua tatizo ambalo limejitokea katika jamii au taasisi.

Tafiti ni nyenzo muhimu katika kusukuma gurudumu la maendeleo kwa nchi yoyote.

Tafiti hutoa dira ya jambo linalokusudiwa kufanywa pamoja na kutoa njia sahihi za kufanikisha jambo hilo.

Leo mathalani tunapoona maendeleo makubwa na ya ajabu ya nchi za dunia ya kwanza kama zinavyoitwa, ni lazima tutambue kuwa tafiti na uvumbuzi ndizo zilizotumika kuwafikisha hapo.

Mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda kwa nchi kama Marekani na China yametokana na uvumbuzi na ugunduzi uliofanywa na wazawa, ambao waliwekeza muda na maarifa katika kuvumbua teknolojia kwenye uzalishaji.

Kwa sisi Tanzania, wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikitekeleza mpango wa kujenga uchumi wa viwanda, utaona kuna umuhimu wa kuongeza nguvu katika masuala ya tafiti, ili wananchi waweze kuzitambua fursa zilizopo kupitia uchumi huo.

Ni kweli tunahitaji kuwa na viwanda vya kutosha ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi nchini.

Lakini wakati tukitekeleza mpango huo kuna haja ya kutilia mkazo suala la kufanya tafiti zitakazosaidia kufanya maamuzi yenye tija.

Ili watu waweze kuendana na kasi ya uchumi wa kati, ni muhimu wajulishwe juu ya fursa zilizopo na kuzitumia kwa manufaa yao.

Pia, kwa wananchi watakaoanzisha viwanda ni lazima wafanye tafiti ili kuwa na uzalishaji wenye tija, endelevu na unaozingatia viwango.

Kwa mfano, mwaka huu wakulima wa zao la mbaazi wameingia hasara kutokana na kutegemea kuuza mazao nje ya nchi, hasa India.

Kama kungekuwapo na viwanda vya ndani, kwa hakika vingeweza kuongeza thamani ya zao hilo na mwishowe kuuza kama bidhaa badala ya kuuza mbaazi ghafi.

Hata hivyo, njia pekee ya kuwa na viwanda huru na vitakavyowanufaisha Watanzania, ni kupitia teknolojia ya ndani inayotokana na wabunifu na wasomi wazawa.

Teknolojia ya nje, inaweza isiendane na mazingira kwa kuwa hutengenezwa kwa kuzingatia uwezo wa nchi hizo kuanzia matumizi ya nishati pamoja na gharama za uzalishaji.

Kwa miaka mingi tumekuwa wanunuzi wa teknolojia kutoka mataifa ya nje. Lakini teknolojia hizo hazitufikishi kokote kwa sababu ya kukosekana kwa watalamu wa ndani.

Matumizi ya teknolojia yanazidi kuongezeka kila uchwao. Hatuna budi kuwa na teknolojia zetu imara ambazo zitawezesha nchi kujiendesha kwa uhakika. Na tafiti hizi zitatokana na utafiti.

Tafiti zinaweza kufanyika kwa kuangazia ni maeneo gani yanahitaji uwekezaji wa viwanda kulingana na upatikanaji wa malighafi kwa urahisi.

Pia, kuchambua masuala ya upatikanaji wa masoko ya bidhaa ambazo zitazalishwa viwandani.

Tafiti pia zinaweza kufanyika ili kuangalia hali ya upatikanaji wa nishati ya umeme, kulingana na mahitaji pamoja na kuangalia nishati mbadala.

Baada ya kujua mahitaji wanasayansi na kuwawezesha, wanaweza kuanza kutafuta njia mbadala kwenye maeneo yenye mahitaji.

Kwa mfano, badala ya kutegemea umeme wa maji, wanaweza kuja na njia mbadala ya kutengeneza umeme rafiki wa jua, upepo au gesi.

Lakini kwa nini tunashindwa kufanya tafiti? Kwa mujibu wa kaimu mkurugenzi mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Dugushilu Mafunda, changamoto kubwa ni ufinyu wa bajeti.

Anasema tume hiyo inategemea misaada ya wahisani katika kufanya tafiti, na kwamba kwa kiasi fulani, imeathiri usimamizi wa tafiti pamoja na kusimamia wabunifu.

Mbali na hilo alisema tafiti nyingi hazina matokeo chanya kutokana na kujikita katika masuala ya kitaaluma na si maeneo ya mahitaji.

Kwa sababu hii, nitoe rai kwa Tume kuhakisha wabunifu waliopo wanajengewa uwezo, kwa ajili ya kufanya ugunduzi mpya wa kiteknolojia ili kukidhi mahitaji ya viwanda ambavyo kwa sasa ndio mwelekeo wa nchi yetu.

Aidha, Serikali ina wajibu wa kuiwezesha tume na watafiti kwa jumla kwa kutenga angalau asilimia moja ya Pato la Taifa(GDP) kwa ajili ya kusimamia shughuli za tafiti.

Hatua hiyo itawasaidia wabunifu wa ndani katika kufanya tafiti nyingi ambazo zitakuwa na tija katika kukuza na kuendeleza viwanda.

Cledo Michael ni mwandishi wa Mwananchi